Serikali yatakiwa kuruhusu kitalu C kufanya kazi

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc), Dk Samuel Gwamaka (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukuta unaozunguka madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

Kitalu C kilichopo Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara kimesitishwa kufanya kazi kwa muda wa zaidi ya miaka miwili sasa

Mirerani. Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc), Dk Samuel Gwamaka ameishauri Serikali kuruhusu machimbo ya madini ya Tanzanite kitalu C Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro mkoani Manyara kufanya kazi.

 Awali kitalu hicho kilikuwa kinamilikiwa kwa ubia wa kampuni ya Sky Group Associates kupitia TanzaniteOne kwa asilimia 50 na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kwa asilimia 50.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea eneo hilo, Dk Gwamaka amesema Serikali inapaswa kutoa hilo ili lifanyiwe kazi upya.

Amesema kwa zaidi ya muda wa miaka miwili iliyopita eneo hilo halifanyiwi kazi hivyo miundombinu iliyopo inaoza na kuzidi kushuka thamani yake kwa kutotumika.


Amesema baada ya muda watu wakifanya tathimini ya kitalu C thamani yake itashuka kutokana na miundombinu iliyopo kuzidi kuharibika kwa kutotumika kwake.

"Maamuzi yanapaswa kufanyika kwani uwekezaji uliowekwa hapo ni mkubwa ila unazidi kuharibika kutokana na kutotumika kwa miundombinu ya eneo hilo," amesema Dk Gwamaka.

Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Mashaka Jororo amesema Serikali igawe eneo hilo ili lifanyiwe kazi na wachimbaji walipe kodi kuliko libaki hivyo hivyo.

"Serikali iwape wachimbaji wadogo na kama kuna watu wanaingia kwa chini kuangalia chochote ni sawa na kuona pilau huku una njaa inakubidi uibe tuu," amesema.