Serikali yatangaza mfumuko wa bei

Serikali yatangaza mfumuko wa bei

Muktasari:

  • Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Dk Ashatu Kijaji ametangaza ongezeko wa mfumuko wa bei wa vyakula mbalimbali ikiwemo mchele, viazi mviringo, maharage na sukari.

Dodoma. Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Dk Ashatu Kijaji ametangaza ongezeko wa mfumuko wa bei wa vyakula mbalimbali ikiwemo mchele, viazi mviringo, maharage na sukari.

Mfumuko huo pia unahusisha vifaa vya ujenzi ambavyo vimepanda kati ya Julai na Agosti mwaka huu pamoja na sabuni za kufulia.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini Dodoma, Dk Kijaji alisema kutokana na ongezeko la malighafi za kutengenezea sabuni zinazoagizwa kutoka nchi za Indonesia na Malaysia, bei za sabuni za kufulia za mche zimeongezeka.

“Bei zimepanda kutoka wastani wa Dola za Marekani 500 hadi 600 kwa tani hadi Dola za Marekani 1,800 hasa baada ya Indonesia kuweka zuio la kusafirisha nje malighafi hizo,” alisema.

Alisema kutokana na ongezeko hilo la bei ya malighafi, bei ya mche wa sabuni ni kati ya Sh3,000 hadi Sh4,500.

Alisema sabuni ya kufulia ya unga inauzwa kati ya Sh1,000 hadi Sh4,500 kwa kilo huku sabuni aina ya Omo ikipatikana kwa kati ya Sh8,000 na Sh8,200.

Kwa upande wa sukari, Dk Kijaji alisema katika kipindi cha Julai na Agosti, bei ya rejareja kwenye maeneo mengi nchini ilikuwa kati ya Sh2,400 hadi 3,000 na katika maeneo machache hasa ya pembezoni ni Sh3,000 kwa kilo kutokana na ongezeko la gharama za usafirishaji.

Waziri Kijaji alisema bei ya maharage imepanda kutoka Sh1,650 na Sh2,600 kwa kilo hadi kufikia Sh1,800 na Sh2,600 wakati mchele umepanda kwa asilimia saba kutoka Sh1,600 na Sh2,800 hadi kufikia Sh1,700 na Sh3,000 kwa kilo.

Dk Kijaji alisema katika bidhaa za ulezi, ngano, uwele, mahindi na unga wa mahindi pamoja na vifaa vya ujenzi, hakuna mabadiliko ya bei katika kipindi hicho cha miezi miwili.

Alisema kwa upande wa mafuta ya kula, bei zilishuka kidogo Agosti ukilinganisha na Julai ambapo lita moja iliyosafishwa mara moja ilishuka kutoka Sh5,000 hadi Sh4,500 huku iliyosafishwa mara mbili ikishuka kutoka Sh9,000 hadi Sh8,000.

Hata hivyo, Dk Kijaji alisema vyakula viko vya kutosha nchini, hivyo wakulima waendelee kuuza huku wakizingatia akiba yao.

“Napenda kusisitiza kauli ya mheshimiwa Waziri wa Kilimo (Hussein Bashe) hatutafunga mipaka kwa wananchi wetu kuuza mazao nje ya nchi, kwa sababu bado tuna chakula cha kutosha ndani kinachohitajika ni wakulima wetu kufikia bei ya mazao nzuri, huku wajihakikisha wanabakiza chakula cha kutosha ndani,” alisema.


Hatua zinazochukuliwa

Dk Kijaji alisema Serikali imeendelea kuchukua hatua kuwapunguzia wananchi athari zinazotokana na kupanda kwa bidhaa muhimu.

Alizitaja hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuimarisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa mbalimbali, ili kupunguza utegemezi wa kuagiza mahitaji muhimu kama chakula kutoka nje ya nchi.

Hatua nyingine ni kuthibiti upandaji holela wa bei na hivyo bei ya bidhaa kwenye soko la ndani zimeendelea kuwa na utulivu, kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa wazalishaji wa ndani wa mafuta ya kupikia yaliyosafishwa kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Alisema pia Serikali inahamasisha jitihada za uzalishaji wa mbegu za mafuta ya kupikia nchini hasa za alizeti na michikichi.

Hatua nyingine ni kuondoa VAT kwa wazalishaji wa mbolea kwa kipindi cha mwaka mmoja, kutoa ushuru wa asilimia 30 au Dola za Marekani 150 kwa tani kwenye usafirishaji wa bidhaa za shaba na chuma chakavu nje nchi.

Dk Kijaji alitaja hatua nyingine ni kupunguza ushuru kwa malori yanayosafirisha bidhaa kutoka Dola za Marekani 16 kwa kila kilometa 100 hadi Dola za Marekani 10 kwa kila kilometa 100.

Julai 14 mwaka huu gazeti hili liliandika kuhusu kupanda kwa bei ya vyakula katika mikoa mbalimbali nchini na lilibaini ongezeko la kati ya Sh200 hadi 400 kwa kilo katika nafaka mbalimbali.

Vyakula hivyo hivyo ni pamoja na maharage, sukari, mchele,dagaa, unga wa sembe na mafuta ya kula.