Serikali yatoa injini sita za Sh58.7 milioni kwa wavuvi

Muktasari:

  • Vyama sita vya ushirika wa wavuvi kutoka Mikoa ya Lindi, Mwanza, Kigoma, Rukwa na Mtwara yakabidhiwa na Serikali injini sita za boti zenye thamani ya Sh58.7milioni kwa ajili kuboresha shughuli zao uvuvi.

Dar es Salaam. Serikali imekabidhi injini sita za kupachika kwenye boti zenye thamani ya Sh58.7 milioni kwa ajili ya vyama sita vya ushirika wa wavuvi huku ikisisitiza kuendeleza sekta hiyo kwa kununua zana bora.

Taarifa iliyotolewa leo Jumapili Septemba 12, 2021 na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imeeleza kuwa mashine hizo zimekabidhiwa na waziri wa wizara hiyo, Mashimba Ndaki akisema lengo la Serikali kuhakikisha shughuli za uvuvi zinakuwa endelevu na kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja.

Ndaki amesema vyama ni pamoja na Kabwe (Rukwa), Mwamgongo (Kigoma), Msanda Mkuu (Mtwara), Kilwa Kivinje (Lindi) Igombe na Chembaya vya mkoani Mwanza. Amesema hiyo sehemu ya fedha iliyoadhinishwa na Serikali kwa ajili ya kuwasaidia wavuvi.

“Kwa mwaka jana na mwaka huu Serikali imetenga Sh200 milioni kununua vifaa na zana mbalimbali za uvuvi kwa ajili ya wavuvi. Nia ya Serikali ni kuona mchango wa pato la taifa katika sekta ya uvuvi unakua kwa kujenga mazingira mazuri ya kuvua rasilimali za uvuvi zilizopo.” amesema Ndaki

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewataka wadau wa sekta ya uvuvi nchini kuwa mchakato wa  kukabidhi injini hizo za kupachika kwenye boti uwe chachu ya wao kujipanga vyema  katika shughuli zao akisema fursa zipo nyingi kwenye  sekta hiyo.

Serikali yatoa injini sita za Sh58.7 milioni kwa wavuvi

Ulega amewataka wadau hao kuhakikisha vyama vyao vya ushirika wa wavuvi vinakuwa imara na kufanya kazi kwa utaratibu uliowekwa.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayeshughulikia sekta hiyo  Dk Rashid Tamatamah amesema wizara imekuwa ikitoa injini hizo mara kwa mara kwa vyama vya ushirika wa wavuvi ambavyo vimesajiliwa na kutambuliwa kisheria kila fedha inapopatikana

 Akizungumza kwa niaba ya wabunge kutoka kwenye majimbo yaliyotoa vyama sita vya ushirika wa wavuvi, Mbunge wa Ilemela,  Dk  Angeline Mabula ametaka kuwepo kwa elimu zaidi kwa kulinda maeneo yanye mazalia ya samaki na kuwepo uvuaji wa samaki kwa vipindi.