Serikali yatoa Sh250 milioni ujenzi kituo cha afya Musoma

Serikali yatoa Sh250 milioni ujenzi kituo cha afya Musoma

Muktasari:

  • Serikali imetoa Sh250 milioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika kata ya Makojo, ambapo fedha hizo za awali zinatarajiwa kutumika kujenga jengo la maabara na la wagonjwa wa nje.

Musoma. Serikali imetoa jumla ya Sh250 milioni kwa awamu ya kwanza kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika kijiji cha Makojo Wilaya ya Musoma vijijini mkoani hapa kitakachokuwa kituo cha rufaa kwa kata nne zilizopo jirani.

Kata zinazotarajiwa kunufaika na kituo hicho ni pamoja na Makojo, Bukumi, Rusoli na Bwasi ambazo wakazi wake hulazimima kutembea umbali mrefu kwaajili ya kutafuta huduma za rufaa zikiwemo za upasuaji kwa akinamama wajawazito.

Akizungumza baada ya kukagua eneo la ujenzi wa kituo hicho leo Oktoba 20, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi amesema kuwa ujenzi w akituo hicho ni moja nia ya serikali katika kuboresha huduma za afya.

"Serikali inataka changamoto zote zitatuliwe, na kwenye sekta ya afya inataka kuhakikisha kuwa uzazi sio adhabu tena na ndio maana hapa kitajengwa kituo cha afya chenye huduma zote ikiwemo huduma ya upasuaji hivyo ile hali ya mama mjamzito kuhangaika hadi kule mkoani kutafuta huduma ya operesheni haiatakuwepo tena," amesema Hapi.

Amezitaka kamati zinazohusika na usimamizi wa mradi  huo kuhakikisha kuwa wanasimamia mradi huo ukamilikwe kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha huku akisema kuwa uzoefu unaonyesha kuwa kamati nyingi zinashindwa kutimiza wajibu wao katika usimamizi wa miradi.

Hapi pia ameagiza uongozi wa halmashauri hiyo kuanza mara moja mchakato wa kupima eneo hilo ili hati ya ardhi iweze kutolewa hatia ambayo itasaidia katika kuepuka migogoro ya umiliki wa ardhi unaoweza kutokea kati ya serikali na wananchi

Awali Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Halfan Haule amesema kuwa mvutano wa wapi kituo hicho kijengwe ulichangia kwa kiasi kikubwa ucheleweahaji wa mradi huo kuanza licha ya serikali kutoa fedha Mwezi Juni mwaka huu.

"Mwenyekiti wa kijiji leo umekuja nikuombe tuendelee hivi hivi, ile hali iliyotokea majuzi hadi ukazira kikao kati yako na mkurugenzi sio nzuri.  Wewe ndiye tunakutegemea katika kufanikisha miradi hapa kijijini, hebu tuangalie tusiwe kikwazo cha miradi hiyo kutejelezwa" amesema Dk Haule.