Serikali yatoa Sh33 bilioni ujenzi vyuo 54 vya maendeleo
Muktasari:
- Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa Sh33 bilioni kwaajili ya ujenzi, ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi Tanzania bara.
Morogoro. Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa Sh33 bilioni kwaajili ya ujenzi, ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi Tanzania bara.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mosha Kabengwe, amesema hayo leo Jumanne Juni 21, 2022 wakati akifungua mkutano mkuu wa Wakuu wa Vyuo Vya Maendeleo ya Wananchi unaofanyika mjini Morogoro.
Kabengwe ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali watu wa wizara hiyo, amesema kuwa ukarabati huo umefanyika katika awamu tatu.
Amesema kwa muda mrefu vyuo hivyo vilikuwa katika hali mbaya kama Magofu lakini akawataka wakuu hao wa vyuo waende wakasimamie ukarabati kwa lengo la kuhakikisha wanaongeza soko la ajira nchini kulingana na mahitaji ya soko.
Kaimu Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia, amesema tayari kupitia mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19 kiasi cha Sh6.8 bilioni kimeshatengwa kwaajili ya kununua vifaa hivyo vya kufundishia na kujifunzia kwa kuanzia na vyuo 34.
Awali Kaimu Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi kutoka wizara hiyo, Margaret Mussai amesema vyuo hivyo vya Maendeleo ya wananchi vilikuwa na hali mbaya lakini baada ya kukarabatiwa vimeweza kubadilisha muonekano wa majengo hayo na kuvutia wanafunzi.