Serikali yazitaka benki kuwafikia wafanyakazi

Muktasari:


  • Serikali imezitaka taasisi za fedha ikiwemo benki ya NMB kuhakikisha inawafikia watumishi husasani walimu ili kuwasaidia kujiendeleza kimaisha.

Serikali imezitaka taasisi za fedha ikiwemo benki ya NMB kuhakikisha inawafikia watumishi husasani walimu ili kuwasaidia kujiendeleza kimaisha.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Jenista Mhagama wakati akizungumza na walimu wa Shule za Msingi na Sekondari wa Kanda ya Kati jijini Dodoma kwenye Siku ya Mwalimu iliyoandaliwa na benki hiyo.

Siku hiyo iliyopewa jina la ‘Mwalimu Spesho’ imeandliwa na NMB na kushirikisha idadi kubwa ya walimu ambao walijikita kuzungumzia maboresho ya mikopo na suluhisho mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo huku walimu wakipongeza huduma hizo kuwa inakwenda kuboresha maisha.

Jenista alisema mpango huo mzuri usiishie kwa walimu 5,000 tu badala yake angetamani uwafikie watumishi wengi zaidi kwenye kada mbalimbali ili kuwajengea uwezo na kuwa chanzo cha kuwaandaa viongozi na wataalamu wa baadaye.

Hata hivyo, ameitaka NMB kusimama na walimu wakati wote ili kuwajengea uwezo akieleza kuwa jumla ya walimu 6,800 wamepandishwa madaraja hivyo ni fursa mpya kuingia kwenye mikopo hasa kupitia benki ambayo ina mifumo mizuri ya uendeshaji.

“Lakini nanyi walimu, najua NMB inaweza kuwajengea uwezo, nendeni mkajishughulishe na biashara zingine huku mkiwajibika kikamilifu katika kada yenu. Usichukue mkopo ukaanza biashara halafu ukasahau kuwajibika, hilo siyo sawa,” alisema Waziri Mhagama.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi, Filbert Mponzi alisema walikusanya walimu viongozi 350 kwa ajili ya kubadilishana mawazo ili kuboresha zaidi huduma za kibenki na kuangalia namna bora ya kutumia fursa za kifedha zilizopo.


“Tunaamini, walimu hawa zaidi ya 350 watasaidia kupeleka elimu watakayoipata hapa kwa wenzao na hata familia zao na jamii kwa ujumla juu ya huduma nzuri zinazotolewa na NMB, lengo ni kumfanya mwalimu kuwa maisha bora wakati wote,” alisema Mponzi.


Wakati hayo yakijiri, wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walikuwa wakijadili fursa na umuhimu wa benki hiyo katika kuleta mabadiliko chanya.


Wakichangia katika hotuba ya bajeti kuu, kwa nyakati tofauti wabunge hao walizungumzia namna ambavyo benki hiyo inakuwa karibu na wananchi hasa wanyonge.


Hoja hiyo ilianzia kwa mbunge wa Viti Maalumu, Dk. Teya Ntala ambaye aliomba mabenki mengine kuiga mfano wa benki hiyo kwani imekuwa ni sehemu ya kupigiwa mfano kwa wanyonge.


Mbunge huyo alizungumzia Sh200 bilioni zilizotengwa na benki hiyo kwa ajili ya kuwasaidia mikopo kwenye elimu kwamba kiasi hicho kinakwenda kuwabeba wanyonge kwa kiasi kikubwa.


 “Hizo Sh200 bilioni si kiasi kidogo, kama benki zingine zitaweza kutenga kiasi kidogo naamini Tanzania ingekuwa na wasomi wengi na watoto wa masikini kwa mpango huu wanakwenda kupata elimu ya juu kwa sababu mfumo uliotengenezwa ni mzuri na ulipaji wake una unafuu mkubwa,” alisema Dk Ntala.


Naye Mbunge wa Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya alipongeza hatua ya kuwakumbuka wajasiriamali ambayo ni sehemu ya kutoa ajira kubwa kwa vijana wa Tanzania na kujiongezea kipato.


Manyanya alisema katika jimbo lake waliamua kujenga na kubiresha soko na kuwaandaa kwa ajili ya kufanya biashara lakini akasema kuwa wengi wamekopa kwenye benki hiyo na kuongeza kipato.


Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri alisema mikopo hiyo inakwenda kuwarahisishia maisha walimu na kuwafanya wasiwe na hofu hivyo kuwahi makazini kwani wanakuwa na uhakika wa maisha yao na familia zao.