Seth, Rugemalira na siku 1349 mahabusu

Muktasari:

  • Wafanyabiashara wawili maarufu nchini Tanzania, Harbinder Sethi na James Rugemalira wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, wakituhumiwa kujipatia fedha  katika akaunti ya Tegeta Escrow wana siku 1349 mahabusu sawa na miaka mitatu, miezi nane na siku nane hadi leo Jumamosi Februari 27, 2021.

Dar es Salaam. Wafanyabiashara wawili maarufu nchini Tanzania, Harbinder Sethi na James Rugemalira wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, wakituhumiwa kujipatia fedha  katika akaunti ya Tegeta Escrow wana siku 1349 mahabusu sawa na miaka mitatu, miezi nane na siku nane hadi leo Jumamosi Februari 27, 2021.

Wapo mahabusu kwa kuwa wanakabiliwa  na mashtaka yasiyodhaminika, huku upelelezi wa kesi yao ukiwa haujakamilika.

Seth na Rugemalira walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Juni 19, 2017 wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 27/2027 yenye mashtaka 12.

Ukiwaona wawili hawa walivyo sasa ni tofauti na siku ya kwanza walivyofikishwa mahakamani kwa sababu kwa nyakati tofauti walikumbana na changamoto mbalimbali.

Desemba 20, 2019 aliongezeka mshatakiwa katika kesi hiyo ambaye ni aliyekuwa mwanasheria wa kampuni ya  kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Joseph Makandege na alifikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kuisababishia hasara Serikali ya dola 980,000.

Makandege ambaye aliwahi kuwa katibu wa IPTL na  wakili Joseph Sungwa.

Siku ya kwanza mahakamani

Siku ya kwanza wanafikishwa mahakamani walionekana ni wenye afya njema.

Rugemarila ambaye kiumbo ni mrefu na mwenye mwili wa wastani, hakuwa mnene lakini hakuwa mwembamba bali alikuwa na mwili wa wastani, mwenye kitambi cha kawaida maana hakikuwa kikubwa kulinganisha na alivyokuwa mwenzake, Sethi.

Siku hiyo alivaa suruali aina ya kadeti ya rangi ya kaki  akiwa ameifunga kwa mkanda mweusi na kuifanya ikae sawasawa kiunoni.

Shati la mikono mifupi la rangi nyeupe iliyofifishwa na michirizi mingi ya bluu na ya njano, alikuwa amelichomekea vema.

Shingoni mwake akining’iniza rozari , huku kwenye mfuko wa shati akiwa ameipachika kalamu  yenye mfuniko mweusi. Miguuni alivaa viatu vya wazi vya mikanda vya rangi ya kahawia.

Kichwa alikuwa na nywele fupi zenye mvi kwa mbali na hakuwa na ndevu.

Usoni alionekana mchangamfu na mara kadhaa akiwa anatabasamu na kuangazaangaza macho ndani ya chumba cha mahakama, kuwaangalia watu waliokuwemo na hata wapiga picha.

Namna alivyokuwa akipiga hatua katika kutembea ilidhirisha pasi na shaka kuwa timamu kimwili yaani akionekana kuwa na nguvu au uimara wa mwili.

Hali hiyo ilidhihirishwa na jinsi alivyokuwa na uwezo wa kunyumbulika kiurahisi.

Kwa mfano siku hiyo walipotolewa mahabusu, kupelekwa katika chumba cha mahakama, askari polisi waliwaamuru kuchuchumaa kabla ya kupelekwa mahakamani kusomewa mashtaka.

Rugemalira aliweza kufanya hivyo mara moja kwa urahisi bila taabu, tofauti na mwenzake, Sethi.

Seth, siku hiyo hakuwa mchangamfu kama alivyokuwa Rugemalira, bali usoni alionekana mwenye mawazo, huku muda mwingi akiwa ameinamisha uso wake chini, akiunyanyua mara moja moja kwa kwa wastani wa sekunde zisizozidi tatu na kuendelea kuinama.

Hata hivyo kimwili   alionekana kuwa imara, kwa jinsi alivyokuwa akitembea vema.

Seth ambaye ni mfupi kwa kimo, alikuwa mnene na mwenye kitambi kikubwa na mashavu yaliyojaa. Siku hiyo wakati walipoamuriwa na askari polisi kuchuchumaa kabla ya kupelekwa katika chumba cha mahakama kusomewa mashtaka yao, alionekana kupata shida sana kufanya hivyo.

Alijaribu mara kadhaa kuchuchumaa kama mwenzake Rugemalira alivyokuwa amefanya, lakini akashindwa na kuamua kupiga magoti.

Siku hiyo alivaa suruali ya rangi nyeusi na shati jeupe la mikono mirefu bila kuchomekea.

Alivaa viatu vya ngozi vya kufunika vya  rangi nyeusi huku mkononi akiwa ameshikilia koti fupi la rangi ya kijivu.

Kichwani alikuwa amefunga kitambaa cheusi kilichokunjwa maridadi na kuonekana kama kofia, huku mashavu yake na pamoja na kidevu vikiwa vimefunikwa kwa ndevu nyeusi tii, zenye urefu wa kati ya nchi sita na nane.

Seth, Rugemalira na siku 1349 mahabusu

Siku hiyo walisomewa mashtaka sita ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za uwongo, kujipatia fedha kwa udanganyifu, uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh358 bilioni.

Seth, Rugemalira na siku 1349 mahabusu

Julai 3, 2017,waliongezewa mashtaka mengine sita na kufikia mashtaka 12 yakiwemo ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana.

Seth, Rugemalira na siku 1349 mahabusu

Jinsi walivyo sasa

Kadri siku zilivyozidi kusogea mbele ndivyo washtakiwa hao walivyozidi kupitia mabadiliko katika nyanja mbalimbali kiasi cha kuwafanya sasa hivi kuwa na mwonekano tofauti na walivyokuwa siku ya kwanza walipopandishwa kizimbani.

Kama mwananchi lilivyowashuhudia mahakamani hapo katikati ya wiki hii maumbile yao si kama ya mara ya kwanza.

Rugemalira amezidi kuwa mwembamba na hana tena kitambi na si imara kama alivyokuwa miaka miwili iliyopita.

Kwa sasa hata hatua zake akitembea si za ukakamavu kama awali, mvi zaidi kichwani lakini ndefu pia zenye mvi.

Sethi pia umbile lake limekuwa dogo na ndevu zake zimejaa mvi.

Hadi sasa hatima ya usikilizwaji wa kesi yao na hatimaye uamuzi bado ni giza nene kwani haijajulikana itaanza kusikilizwa lini kwa sababu upande wa mashtaka wameieleza Mahakama kuwa upelelezi haujakamilika.

 Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 11, 2021 itakapotajwa.

Maombi mahakamani

Februari 13, 2020 Rugemarila alimuomba Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania( DPP) kumuondoka katika kesi hiyo kwa sababu ameshawasilisha nyaraka za watu wanaotakiwa kushtakiwa.

Alidai kuwa kelele alizopiga zitasaida kukamatwa kwa wezi waliohusika katika kesi .

Pia, mshtakiwa huyo aliwasilisha notisi kwa taasisi kubwa tisa nchini Tanzania, akimtaka DPP amuondoe kwenye kesi hiyo na asipofanya hivyo atawasilisha maombi rasmi ya kuiomba mahakama imuondoe katika kesi hiyo.

Alidai notisi hiyo inahusu matatizo yalivyo kuhusiana na kesi hiyo na kwamba kuna vipengele vya kisheria ambavyo havitekelezwi, kutokana na hali hiyo anaomba DPP amuondoe katika kesi hiyo.

Aliwasilisha taarifa hiyo mbele ya hakimu mkazi mkuu wa mahakama hiyo, Huruma Shaidi baada ya upande wa mashtaka kueieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon alidia kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado unaendelea.

Wakili Simon baada ya kueleza hayo, Rugemalira alinyoosha mkono akiashiria kuwa anaiomba mahakama imruhusu kuongea.


Aliporuhusiwa na mahakama kuongea alidai kuwa alitarajia siku hiyo angeachiwa huru na kuondolewa katika kesi hiyo.

" Unajua mheshiwa hakimu nilitoa notisi sehemu mbalimbali ikiwemo kwa DPP, DCI na nyingine na tayari zimepokelewa  hivyo leo hii nilitegemea naachiwa  kwa kuondolewa katika shauri hili.”

"Lakini pia, nilitegemea Jamhuri(upande wa mashtaka) waje na ufafanuzi kuhusu barua niliyoandika kuhusu Benki ya Standard Chartered kukwepa kodi, sheria haitekelezwi, lakini nimetoa notisi na kuisambaza kwa taasisi hizo na tayari imepokelewa kote, "alidai.

Hata hivyo, Hakimu Shaidi, alimuuliza hiyo nitisi ametoa kwa nani?

Rugemarila alijibu kuwa amewasilisha notisikwa DPP, DCI, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Mkurugenzi wa Takukuru, Gavana wa Benki Kuu(BoT), Kamishna TRA, Wakili Mkuu w Serikali na Kamishna wa Magereza.

Alidai notisi hiyo inahusu matatizo yalivyo kwa ujumla kuhusiana na kesi hiyo na kwamba kuna vipengele vya sheria havitekelezwi, hivyo kutokana na hali hiyo anaomba DPP amuondoe katika kesi hiyo.

Pia siku hiyo hiyo, mshtakiwa huyo aliieleza mahakama hiyo kuwa barua aliyomuandikia gavana wa BoT, ameeleza kuwa hakupata hata shilingi moja kutoka akaunti ya Escrow.

" Barua niliyomuandikia Gavana  wa BoT nimeeleza kuwa mimi sijapokea hata shilingi moja kutoka katika akaunti ya Escrow, hela nilizopokea mimi ni zile za PAP zilizotolewa kwa amri ya mahakama,” alidai Rugemarila.

Wakati Rugemarila alieleza hayo, washtakiwa wenzake walikuwa wakimtazama tu, licha ya kuruhusiwa na mahakama aongee akiwa amekaa kwenye benchi, yeye alionekana muda mwingi akisimama huku akifungua rundo la nyaraka mbalimbali na kuzirudishia katika mfuko, kabla ya  kuipatia mahakama.

Alijibu hoja hizo, Wakili Simon alidai kuwa kama mshtakiwa ana hoja anatakiwa kuziwasilisha mahakamani.

Mahakama yaruhusu maombi

Februari 27, 2020 mahakama iliamuru Rugemarila kuwasilisha hoja zake za kutaka mahakamani hiyo imuondoe katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili.

Mshtakiwa huyo aliwasilisha hoja hizo wakati shauri hilo lilipoitwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.

Maahakama hiyo ilipokea hoja hizo na upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon waliomba kuwasilisha majibu yao kwa maandishi, Machi 12, 2020

Wakili Simon baada ya kueleza hayo, wakili wa utetezi John Chuma aliyemwakilisha Rugemarila alidai mahakamani hapo kuwa mteja wake aliwasilisha hoja ya pingamizi la awali ambayo mpaka siku hiyo hawakupata majibu yoyote.

Akijibu hoja hiyo Simon alikiri kupokea nyaraka mbili kutoka upande wa utetezi moja ikiwa inamhusu Rugemarila lakini alitaka kujua kama nyaraka hizo zipo kwenye rekodi ya mahakama.

Hakimu Shahid alisema  ameziona nyaraka hizo na zipo kwenye rekodi ya mahakama.

Kutokana na hali hiyo, Simon aliiambia mahakama kuwa watatoa majibu kwa njia ya mdomo mahakamani hapo baada ya upande wa utetezi kuwasilisha hoja zao kwa maandishi na wako tayari kujibu muda wowote ikiwa mahakama itaruhusu.

Awali, Rugemarila alidai mahakamani kuwa aliandika barua kwa kamishna wa TRA kupitia mjumbe wa Takukuru aliyetembelea gerezani akielezea jinsi Benki ya Standard Chartered Hong Kong inavyokwepa kodi huku akieleza wanaostahili kujumuishwa kwenye kesi ni benki hiyo na si yeye.

Alidai aliandika notisi kwa tasisi tisa ikiwemo Usalama wa Taifa akitaka DPP awasilishe hati ya kuachiwa kwake na asipofanya hivyo yeye atawasilisha hoja ya kuiomba mahakama imuondoe katika kesi hiyo.

Katika hatua nyingine, upande wa mashtaka ulieleza  mahakama hiyo kuwa wanataka kujua kama Rugemarila ana uwakilishi wa wakili au anajitetea mwenyewe mahakamani.

Ni baada ya mshtakiwa huyo  kuwasilisha hoja mbalimbali mahakamani hapo, ikiwemo kujitetea badala ya mawakili wake kufanya kazi hiyo .

Alijibu hoja za upande wa mashtaka, Rugemalira alidai kuwa hajui tatizo la upande wa mashtaka ni nini kwa yeye kujitetea kwa sababu sheria ina  mruhusu kujitetea, hivyo aliiomba mahakama kutozingatia maelezo yaliyowasilisha  na upande wa mashtaka.

Waitwa mahakamani

Novemba 9, 2020 mahakama ilimetoa hati ya kuwaita mahakamani Seth na wenzake wawili ili waje wasikilize kesi yao ya uhujumu uchumi inayowakabili.

Mahakama hiyo ilifikia hatua hiyo kutokana kesi kusikilizwa kwa njia ya video tangu kuibuka kwa ugonjwa wa Covid 19 Machi 2020 hadi Novemba 2020

Kuingia kwa ugonjwa huo nchini kulisababisha kesi nyingi ambazo washtakiwa wake wapo mahabusu wenye kesi ambazo upelelezi wake haujakamilika na wenye mashtaka ambayo hayana dhamana kusikilizwa  kwa njia ya video.

Utaratibu huo umedumu hadi sasa ambapo washtakiwa wenyewe kesi za uhujumu uchumi zenye mashtaka ya kutakatisha fedha, pamoja na mashtaka mengine ambayo hayana dhamana, kesi zao husikilizwa kwa mtindo huo.

Uamuzi huo wa kuwapeleka mahakamani washtakiwa hao kutoka gerezani ulitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha ombi la kuwataka washtakiwa hao wapelekwe mahakamani hapo kwa ajili ya kusikiliza kesi yao.

Ombi hilo lilowasilishwa mahakamani hapo siku hiyo na wakili wa Serikali, Faraja Nguka wakati kesi hiyo ilipoitwa.

"Hakimu kesi iliitwa kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa hawa walitakiwa kuwepo leo (jana) mahakamani kwa sababu tulishatumahati ya kuwaita washtakiwa waliopo gerezani, sasa sijajua kwanini hawajaletwa" alidai Wakili Nguka.

Wakili Nguka baada ya kueleza hayo, Hakimu Shaidi alielekeza kuwa tarehe ijayo washtakiwa hao wanatakiwa wapelekwe mahakani hapo na kutoa hati ya kuwaita washtakiwa hao.

Rugemalira aomba kufutiwa kesi

Desemba 19, 2020  Rugemalira aliombamahakama imfutie kesi yake ifikapo Desemba 31, 2020 kama upande wa mashtaka hawatakamilisha upelelezi katika kesi inayomkabili.

Rugemalila alifikia hatua hiyo baada ya wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon kuieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kwamba anaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Tofauti na siku nyingine ambapo kesi hiyo husikilizwa kwa njia ya video, siku hiyo washtakiwa hao walipelekwa mahakamani hapo wakitokea gerezani.

Wakili Simon baada ya kueleza hayo ndio Rugemarila alipoieleza mahakama hiyo kuwa tarehe ijayo kama upande wa mashtaka hawataieleza mahakama hiyo upelelezi umekamilika, basi anaomba mahakama imwachie huru.

Mshtakiwa huyo alidai kuwa kesi hiyo ni ya muda mrefu na imefikisha miaka mitatu bila upelelezi kukamilika, hivyo anaiomba mahakama iifute kesi hiyo.

Akijibu hoja za mshtakiwa, Simon alidai utaratibu wa kufuata kesi hiyo ni jambo ambalo upande wa mashtaka hawawezi kulifanyia kazi.

Wakili Simon alidai mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, hivyo upelelezi utakapokuwa umekamilika ndipo watakuja kuieleza mahakama hiyo hatua zinazotakiwa kufuata.

" Hatuwezi kusema upelelezi bado katika maeneo gani, au upo katika hatua gani, ieleweke tu kwamba tutakapokamilisha upelelezi tutakuja kuieleza mahakama hii" alidai wakili Simon.

Mahakama yatoa siku 30

Februari 25, 2021 mahakama ilitoa siku 30 kwa Seth na Makandege kujadiliana na DPP

Iliamuru majadiliano  ya kukiri mashtaka yaliyowasilishwa na Seth na  Makandege yasikilizwe  ndani ya siku 30.

Ilifikia uamuzi huo baada ya Seth kuwasilisha mahakamani hapo maombi mawili ambayo ni kuletwa mahakamani kila kesi yake inapotajwa na kukutana DPP kwa ajili ya kufanya majadiliano ya kukiri mashtaka yake.

Hakimu Shaidi, baada ya kusikiliza hoja za pande zote alikubaliana na hoja za upande wa utetezi akisema kuwa DPP ana mamlaka ya kukubali au kukataa maombi hayo lakini pia halazimishwi kukubali.

"DPP halazimishwi kukubali, lakini pia lazima akubali au akatae na sio kukaa kimya, mahakama pia ina uwezo wa kuelekeza ndani ya siku 30 makubaliano hayo yafanyike na jibu litolewe, hivyo mahakama inaelekeza jambo hilo lifanyike ndani ya siku 30 kuanzia leo,”  alisema Hakimu.

Kuhusu washtakiwa kushindwa kupelekwa mahakamani, Shaidi alielekeza washtakiwa hao kupelekwa mahakamani kila tarehe ya kesi hiyo inapotajwa kwani sheria iko wazi

Kabla ya kuwasilishwa kwa maombi hayo, wakili wa Serikali Faraja Ngukah alidai kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa shauri hilo haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Ngukah baada kueleza hayo, Melchisedeck Lutema ambaye ni wakili wa Seth aliieleza mahakama hiyo kuwa licha ya kuandika barua hizo mbili kuomba kufanya majadiliano moja ya  Julai Mosi 2019 iliyopokewa Julai 23,2019 na ya pili ya Julai 20, ,2020 iliyopokewa Septemba 10,2020, lakini mpaka sasa zote hazijajibiwa.

"Kwa mujibu wa Kanuni mpya za Pre-bargain zilizotolewa na jaji mkuu, mwaka huu mahakama ina mamlaka ya kutoa muda kwa pande zote kujadiliana na kukamilisha majadiliano kwa muda usiozidi siku 30. Hivyo tu naomba mahakama itoe maelekezo hayo," alidai Lutema.

Alisema ni jukumu la DPP kujibu barua za wateja wao  kama hataki kuingia majadiliano aseme ili waendelee na hatua nyingine.

"Ofisi ya DPP imekaa kimya kwa kutojibu barua za wateja wetu za kukili makosa,” alidai.


Alidai mteja wake yupo tayari kufanya makubaliano na anatoa taarifa mahakamani kwa mujibu wa kanuni ya 3 ya kanuni mpya za makubaliano zilizotolewa na jaji Mkuu mwaka 2021 na chini ya kifungu cha 5 cha kanuni hizo.

Katika hatua nyingine wakili huyo alikumbushia barua aliyoandika mteja wake akilalamika kutoletwa mahakamani kwa muda wa miezi saba sasa ambapo hakimu aliamuru mshitakiwa huyo kuletwa mahakamani kila baada ya siku 14 kwani ni haki yake kisheria.

Wakati wakili Lutema akiwasilisha hoja hizo, wakili wa Makandege, Joseph Sungwa naye aliwasilisha maombi ya mteja wake ambayo yanafanana na yale yaliyowasilishwa na wakili wa Seth.

Akijibu hoja hizo, wakili Ngukah alikiri kwamba ni haki ya mshtakiwa kuletwa mahamanani kila baada ya siku 14 na anachokumbuka mara ya mwisho mshtakiwa  aliletwa Desemba 17, 2020 na kwamba walishindwa kufikishwa washtakiwa hao walishindwa kupelekwa mahakamani  kutokana na shida ya usafiri.

Kuhusu barua ya maombi ya kukiri makosa Ngukah alidai mawakili wafatilie suala hilo kwa DPP.

Hakimu Shaidi baada ya kusikiliza hoja za pande zote alitoa uamuzi na kuahirisha kesi hiyo hadi Machi 11, 2021, itakapotajwa.


Mbali na washtakiwa hao, mshtakiwa mwengine ni Mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) James Rugemalira.

Mashtaka yao kwa ufupi:

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 12 likiwemo la kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo Oktoba 18, 2011 na Machi 19 , 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ili kutenda kosa.