Sh2.5 bilioni zatumika kuwanoa watumishi 7, 609 wa madini

Muktasari:

  • Serikali imetumia kiasi cha Sh2.5 bilioni mwaka 2021 kutoa mafunzo kwa Watanzania walioko katika sekta ya madini nchini ili kuwajengea uwezo wa utendaji kazi hususani zile zinazofanywa na wageni.

Mwanza. Serikali imetumia kiasi cha Sh2.5 bilioni mwaka 2021 kutoa mafunzo kwa Watanzania walioko katika sekta ya madini nchini ili kuwajengea uwezo wa utendaji kazi hususani zile zinazofanywa na wageni.

Taarifa hiyo imetolewa leo Mei 20, 2022 na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula kwenye jukwaa la kwanza la utekelezaji wa ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini linalofanyika jijini Mwanza ambapo amesema mafunzo hayo yametolewa kwa watanzania 7, 609 walioko katika sekta hiyo.

Profesa Kikula amesema mafunzo hayo ni mwendelezo wa mkakati wa kuwajengea uwezo watanzania ambao hawana uzoefu katika sekta hiyo kutokana na uwepo wa Teknolojia mpya nchini.

"Kumekuwa na utaratibu wa kuwa na mpango wa urithishwaji kwa watanzania kwa nafasi zinazoshikiliwa na raia wa nchi nyingine. Hii itaongeza idadi ya watanzania wanaoshikilia nafasi za uongozi katika kampuni za madini nchini," amesema Profesa Kikula.

Katika hatua nyingine, Profesa Kikula amesema ajira za watanzania katika migodi mikubwa na kati nchini zimeongezeka kutoka 6, 668 mwaka 2018 sawa na asilimia 95 hadi 14, 308 mwaka 2021 sawa na asilimia 97 ya ajira zote.

"Ongezeko hili la ajira kwa watanzania limechochewa na usimamizi wa ushirikishwaji wa watanzania ambapo watanzania wanapewa kipaumbele katika fursa za ajira zote nchini," amesema.

Amewataka watanzania walioajiriwa katika kampuni hizo kutumia fursa hiyo kuhakikisha wanaendeleza uhawilishwaji wa Teknolojia (Transfer of Technology) na utafiti wa maendeleo ili kuongeza uzalishaji wa wataalam wa madini ambao ni wazawa.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico), Dk Venance Mwasse amesema jukwaa hilo linatoa fursa kwa watanzania kujua fursa zilizoko katika sekta ya madini nchini.

"Hapa kuna taasisi za fedha mbalimbali ambao tunatarajia zitawafungua watoa huduma katika sekta ya madini juu ya fursa ya mikopo ya isiyo na riba na ile ya riba nafuu inayopatikana katika taasisi hizo na namna ya kuitumia kuongeza tija na uzalishaji katika kampuni zao," amesema Dk Mwasse

Naye Mshiriki katika jukwaa hilo, Hamis Juma amesema mbali na kutambua fursa zilizoko katika sekta hiyo, jukwaa hilo linatoa fursa ya kutengeneza mtandao wa mashirikiano baina ya kampuni ya madini nchini.

Jukwaa hilo limeudhuriwa na mamia ya watoa huduma katika kampuni kubwa na kati za madini nchini huku likiambatana na maonyesho ambapo Taasisi za serikali na wadau wa madini wanaonyesha shughuli zao katika viwanja vya Rock City Mall jijini Mwanza.