Sh23 bilioni kukopesha wajasiriamali

Muktasari:

Wakati utaratibu wa kuwapanga wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali nchini Tanzania ukiendelea kufanyika, taasisi za fedha za ndani na za kimataifa zimeendelea kuweka mazingira mazuri ya kuwawezesha wajasiriamali hao hasa wanawake kukuza biashara na kupiga hatua.

Dar es Salaam. Mikakati ya Serikali na taasisi za fedha nchini kuendelea jitihada za kuwawezesha wajasiriamali nchini, imezidi kushika kasi baada ya benki ya CRDB kuingia makubaliano ya mkopo wa jumla ya Dola za Marekani milioni 60 (Sh138 bilioni) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Hatua hiyo inalenga kuwawezesha wajasiriamali nchini hususan wanawake na kwenye makubaliano hayo na AfDB, CRDB itaelekeza kiasi cha Dola za Marekani milioni 50 (Sh115 bilioni) katika kuimarisha mtaji wake pamoja na kusaidia mpango wa upanuzi wa kikanda za benki hiyo. 

Sehemu iliyobaki ya mkopo huo ambayo ni Dola za Marekani milioni 10 (Sh23 bilioni), itaelekezwa kwenda kusaidia upatikanaji wa fedha kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini Tanzania.

Mkataba huo pia unajumuisha msaada wa kiufundi na mafunzo wenye thamani ya dola za Marekani 175,000 (Sh405 milioni) ili kuimarisha uwezo wa benki hiyo kusaidia wajasiriamali wanawake nchini ili waweze kukopesheka zaidi na kuanzisha miradi ya maendeleo.

Aidha, Mfuko wa Dhamana ya Afrika (AGF) umeboresha mpango wake wa dhamana kwa wa Sh115 bilioni kwa benki hiyo kwa ajili ya wajasiriamali nchini.

Mpango huo unajumuisha sehemu ya dhamana ya AFAWA ya Ukuaji ili kupunguza hatari ya soko kwa wanawake wajasiriamali na kusaidia zaidi ukuaji wao. Mkataba huo umesainiwa leo Jumatano, Julai 27, 2022 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Afrika Mashariki, Nnenna Nwabufo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Dhamana Afrika, Jules Ngankam na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela.

Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, Ngankam amesema mpango huo unakwenda kuwaimarisha shughuli za wajasiriamali katika sekta mbalimbali nchini Tanzania. Amesema ushirikiano wa muda mrefu na benki hiyo, umekuwa chachu ya kufikiwa kwa mafanikio hayo.

"Ni imani yangu kuwa ushirikiano huu wa pande tatu baina ya CRDB, AfDB, na AGF, utakuwa na matokeo chanya zaidi hususan katuka kuziba pengo la ufadhili kwa biashara za wanawake," amesema.

Naye Nwabufo amesema wajasiriamali sasa watapata fursa za uhakika za kuboresha biashara kwa kupata fedha na kwamba, itaongeza juhudi za Tanzania kuziba pengo la upatikanaji wa fedha kwa wajasiriamali wanawake ambalo linakadiriwa kufikia dola bilioni 1.6.

Kwa upande wake, Nsekela amesema kuwa mkopo huo utaendelea kuifanya benki hiyo kuwa kimbilio la wafanyabiashara wakubwa, wa kati na wadogo ambao ni kundi kubwa linalohitaji kuwezeshwa kusonga mbele.