Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sh300 milioni zawasubiri wanahisa wasiojulikana wapate gawio

Baadhi ya Wanachama wa TCCIA Mkoani Pwani wakihakiki taarifa zao wakati wa Mkutano wao Mkuu wa mwaka uliofanyika Mjini Kibaha. Picha na Sanjito Msafiri

Kibaha. Zaidi ya Sh300 milioni zilizotakiwa kulipwa kwa wanachama wa Chemba ya Wafanyabiashara Mkoa wa Pwani (TCCIA) hazijawafikia walengwa kwakuwa wengi wao hawajulikani walipo.

Wanachama hao ni wale waliojiunga na TCCIA Investment yenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam zaidi ya miaka 10 iliyopita kwa kununua na kuwekeza hisa kwenye taasisi hiyo.

Hayo yamebainishwa jana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa (TCCIA), Peter Kifunguomali wakati wa Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika Kibaha mkoani Pwani.

“Miongoni mwao taarifa zao hazipatikani sawasawa wala mawasiliano yao, hivyo tunatumia wasaa huu kuwaomba wale waliokuwa wanachama na walinunua hisa waje na taarifa zao kamili ili wapate gawio,” amesema.

Amesema kuwa kutokana na umakini wa utendaji kazi wa taasisi hiyo hakuna  mwanachama anayepoteza haki yake na hata kama imetokea bahati mbaya amefariki ndugu wanapaswa kufuata taratibu za kisheria ili kuchukua hisa za marehemu.

Wakizungumza kwenye mkutano huo baadhi ya wanachama wa chama hicho wamesema kuwa kuwekeza hisa kuna faida na pia kunamuondolea mwanachama msongo wa mawazo huku pesa zake zikiwa salama.

“Nilijiunga miaka zaidi ya 10 na nikanua hisa nimeshafaidika kwa mambo mbalimbali na pesa zangu ziko salama hivyo nawaasa wengine hasa wanawake wasijiingize kwenye michezo ya mitaani ya kupeana fedha bali wajiunge huku na wanunue hisa,” amesema Glada Gia.

Makamu Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara Kilimo na wenye Viwanda (TCCIA) Mkoa wa Pwani, Fadhiri Gonzi amesema kuwa mkoa huo una zaidi ya wanachama 200 lakini wengi wao wamekuwa hawajitokezi ili kupata gawio na kwamba wameendelea kuwatafuta kwa njia mbalimbali ili kupata haki zao.