Sh507 milioni kupeleka maji Chunya

Mkuu wa wilaya ya Chunya akizungumza na wananchi wa kata ya Sangambi

Muktasari:

  • Adha ya maji kwa wakazi wa kata ya Sangambi wilayani Chunya mkoani Mbeya inakwenda kutatuliwa baada ya kuanza ujenzi wa mradi wa maji wenye thamani ya Sh507 milioni.

Chunya. Adha ya maji kwa wakazi wa kata ya Sangambi wilayani Chunya mkoani Mbeya inakwenda kutatuliwa baada ya kuanza ujenzi wa mradi wa maji wenye thamani ya Sh507 milioni.

Mradi huo unatarajiwa kutatua changamoto ya ukosefu wa maji inayowakabili wananchi wa kata hiyo kwa muda mrefu.

Wakizungumza wakati wa makabidhiano ya kuanza mradi huo kati ya Serikali na kampuni ya Leostart company Ltd ambayo ndio imepewa tenda ya kujengwa na kusambaza maji katika kata hiyo, wamesema mradi huo utamaliza adha wanayokumbana nayo.

Mkazi wa Sangambi, Rahabu Samsoni amesema mradi huo utakapokamilika utapunguza magonjwa ya mlipuko yanayosababishwa na matumizi ya maji yasiyo safi na salama.

Injinia wa maji Ruwasa wilaya ya Chunya, Ismail Ismail amesema mradi huo unatarajia kukamilika Juni 30, 2022 ambapo mkakati wa kuhakikisha mwananchi anapata maji safi na salama.

Mbunge wa Jimbo la Lupa, Masache Kasaka akizungumza na wananchi wa kata hiyo aliwasisitiza wananchi kushirikiana vyema na wakandarasi wanaojenga mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati.

Amesema hawezi kuvumilia kuona watu wanahujumu miundombinu ya maji kama ilivyo kwa baadhi ya miradi na kuwarudisha nyuma juhudi za Serikali ambapo amewaasa wananchi kuwa walinzi wa mradi huo.

Diwani wa kata ya Sangambi, Junjulu Mhewa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kupunguza changamoto ya maji katika kata yake.

Aidha Mkuu wa wilaya ya Chunya, Mayeka Mayeka amewasihi wananchi kuhakikisha wanashirikiana vyema na mkandarasi ili mradi huo ukamilike kwa wakati na wao waendelee kunufaika.