Sh70 bilioni kumaliza kero ya maji Musoma, Butiama

Muktasari:
Mradi wa maji wa Mugango-Kiabakari-Butiama unaotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh70.5 bilioni umefika asilimia 91 za utekelezaji wake ambao unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Septemba 2023.
Butiama. Wakazi wa Wilaya ya Musoma na Butiama mkoani Mara wanatarajia kunufaika na mradi wa maji wa Mugango-Kiabakari- Butiama wenye thamani ya Sh70.5 bilioni unaotarajia kukamilika mwishoni mwa Septemba, 2023.
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ya Butiama aliyefanya ziara kukagua mradi huo Septemba 6,2023, Mhandisi Mshauri wa Mradi, Chrispin Mwashala amesema Serikali imelipa asilimia 65.6 za malipo yote na kazi kubwa iliyobaki ni pamoja na ufungaji wa pampu kwaajili ya kusukuma maji kwenye mradi huo uliofikia asilimia 91.
“Tayari tumeagiza pampu kubwa sita kutoka nchini Uturuki na zipo njiani zinakuja zitawasili hapa muda wowote, zikifika tu kazi ya ufungaji itaanza kisha tutaanza majaribio ya kusukuma maji kwenda kwenye matenki tayari kwaajili ya kutumiwa na wanufaika,”amesema
Amesema mradi huo ulioanza kutekelezwa Desemba, 2020 ulitarajiwa kukamilika Desemba, 2022 lakini haukukamilkka kutokana na changamoto kadhaa ikiwemo ucheleweshaji wa malipo pamoja na uwepo wa ugonjwa wa covid 19 uliosababisha vifaa vingi vilivyokuwa vikiagizwa kutoka nje ya nchi kuchelewa kufika nchini.
Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya mradi, Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Moses Kaegele amesema mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Sh70.5 bilioni unatarajia kunufaisha wakazi wa vijiji 39 katika wilaya ya Butiama na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma vijijini.
“Zaidi ya wananchi 233,000 watanufaika na mradi huu ambao utakuwa suluhisho la kudumu juu ya changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama iliyodumu kwa muda mrefu katika maeneo hayo ikiwepo eneo la Butiama,”amesema
Amemtaka mkandarasi wa mradi huo kufanyakazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi huo unakamilika katika muda huo ulioongezwa kwa maelezo kuwa walengwa wameusuburi kwa muda mrefu sasa.
Mkazi wa kijiji cha Kamugegi Wilaya ya Butiama, Anna Magige amesema mradi huo utakuwa mkombozi kwa wanawake ambao wameteseka muda mrefu kwa changamoto ya ukosefu wa maji katika kijiji chao.
“Kama unavyoona hapa kwetu palivyo pakavu, hatuna maji yaani kila siku ni shida, wanawke tumeshindwa hata kujihusisha na shughuli za ujasiriamali kwasababu muda mwingi tunautumia kutafuta maji, naomba kasi ya mradi iongezeke,"amesema Esha Guguye mkazi wa Kamugegi.