Shahidi adai hajui kina Zumaridi wanashtakiwa kwa kosa gani

What you need to know:

Kwenye hati ya mashtaka ya kesi hiyo, Zumaridi na wenzake 83 wanakabiliwa na mashtaka manne ikiwemo kufanya kusanyiko lisilo na kibali kinyume na kifungu cha 74 (1) na 75 cha kanuni ya adhabu na kumjeruhi Sajenti Evodius kwa kumshambulia kwa kutumia ngumi, mateke na mawe sehemu mbalimbali za mwili wake.

Mwanza. Katika hali isiyo ya kawaida shahidi wa tatu katika kesi ya Jinai namba 12/2022 inayomkabili Diana Bundala maarufu "Mfalme Zumaridi" na wenzake 83 ambaye ni Askari wa Jeshi la Polisi mwenye namba, G1727 Koplo Patrick ameieleza mahakama hajui washtakiwa hao wanashtakiwa kwa kosa gani.

 Kwenye hati ya mashtaka ya kesi hiyo, Zumaridi na wenzake 83 wanakabiliwa na mashtaka manne ambayo ni kufanya kusanyiko lisilo na kibali kinyume na kifungu cha 74 (1) na 75 cha kanuni ya adhabu na kumjeruhi Sajenti Evodius kwa kumshambulia kwa kutumia ngumi, mateke na mawe sehemu mbalimbali za mwili wake.

Mashtaka mengine ni kumjeruhi Kopro, Patrick Mguuni na kumjeruhi Inspekta, Temi kwa kutumia ngumi, mateke na mawe sehemu mbalimbali za mwili wao walipokwenda kuwakamata washtakiwa hao nyumbani kwa Zumaridi katika mtaa wa Buguku eneo la Buhongwa jijini Mwanza.

"Shtaka la pili, tatu na nne ni kusababisha majeraha kwa maofisa watatu wa polisi kinyume na kifungu namba 241 sura ya 16 cha Kanuni ya Adhabu kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2016," Dorcas Akyoo ambaye ni Wakili wa Serikali Mwandamizi aliieleza mahakama hiyo.

Baada ya Akyoo kumuongoza shahidi kutoa ushahidi wake, Hakimu Mushi ameagiza jopo la mawakili wa utetezi linaloundwa na Wakili Steven Kitale, Linus Amri, Merichzedeck Gunda na Silas John kuanza kumuuliza shahidi huyo maswali kuhusiana na ushahidi aliotoa mahakamani hapo.

Akianza kuuliza swali kwa shahidi huyo, wakili wa utetezi, Steven Kitale amemuuliza Koplo Patrick iwapo anajua mashtaka aliyokuja kuyatolea ushahidi kuhusu Mfalme Zumaridi na wenzake 83 na kupelekea washtakiwa na mashuhuda wa kesi hiyo, shahidi huyo ameeleza kwamba hafahamu wanashtakiwa kwa kosa gani.

Shahidi huyo alipoulizwa na Kitale iwapo alikuwa anafahamu kwamba Mfalme Zumaridi na wenzake wanakabiliwa na kosa la kufanya kusanyiko lisilo na kibali ameieleza mahakama kwamba hakuwa na taarifa hiyo badala yake alijua wanawakamata kwa kujeruhi maofisa wa jeshi la polisi.

Pia, shahidi huyo ameieleza mahakama hiyo kwamba Mkuu wa msafara wa askari wa Polisi ambaye ni Mkuu wa Upelelezi wilaya ya Nyamagana, Inspekta Temi ndiyo alitoa agizo la kuvunja mageti ya nyumbani kwa Zumaridi baada ya kutoa mageti hayo yafunguliwe bila mafanikio.

Kitale alipomuuliza shahidi huyo iwapo alishambuliwa kwa ngumi, mateke na mawe, shahidi ameieleza mahakama kwamba hakupigwa mateke na ngumi badala yake akipigwa jiwe na mshtakiwa namba 33, Mershaki Son of Joseph huku jina halisi la mshtakiwa likiwa ni Meshack Joseph.

Shahidi huyo alipoulizwa iwapo kuna uharibifu wowote uliotokea kwenye gari baada ya kushambuliwa na washtakiwa ameieleza mahakama kwamba magari ya polisi hayakupata madhara yoyote.

Kesi hiyo imeitwa leo Jumanne, kwa ajili ya kuendelea na usikilizaji wa ushahidi wa upande wa Jamhuri chini ya Hakimu Mkazi, Clescensia Mushi.

Sehemu nyingine na maswali na majibu kati ya wakili wa Utetezi, Steven Kitale na Shahidi huyo, Koplo Patrick ilikuwa hivi;


Kitale: Shahidi naomba kufahamu elimu yako?


Shahidi: Kidato cha nne


Kitale: Unamfahamu Sajenti Evodius?


Shahidi: Namfahamu


Kitale: Shahidi kati yako wewe na yeye nani alianza kufika kituo cha Polisi?


Shahidi; Sikumbuki


Kitale: Shahidi unafahamu washtakiwa wanashtakiwa kwa makosa yapi?


Shahidi: Sifahamu


Kitale: Wakati mnapewa maelekezo ya kwenda kwa Mfalme Zumaridi, ni kweli kwamba kulikuwa hakuna maelekezo ya mkusanyiko usiyo halali?


Shahidi: Hakukuwa na maelekezo ya mkusanyiko usiyo halali


Kitale: Ni kweli kazi uliyotumwa kule na wenzako ilikuwa ni ukamataji?


Shahidi: Ni kweli


Kitale: Ni kweli kwamba taarifa za kuwakamata zilikuwa taarifa za kuambiwa na hukuwa na uhakika nazo?


Shahidi: Ndiyo


Kitale: Katika ushahidi wako hapa mahakamani, hujaonyesha sehemu yoyote ulipopata jeraha lolote linalohusiana na kupigwa kwa matekez ngumi na mawe katika sehemu mbalimbali za mwili wako?


Shahidi: Ni kweli


Kitale: Katika hawa watuhumiwa walioko mahakamani hakuna mtuhumiwa uliyeonyesha alikupiga kwa ngumi, na mateke?


Shahidi: Ni kweli


Kitale: Ni kweli hakuna mshtakiwa anayeendana na majina hayo uliyosoma (yaliyo kwenye hati ya mshtaka) kwamba alikupiga kwa mawe?


Shahidi: Si kweli


Kitale: Kuna uharibifu uliofanyika kwenye magari ya polisi?


Shahidi:  Hapana


Kitale: Umeeleza kwamba ulipewa PF3, uliongozana na nani kwenda hospitalini


Shahidi: Nilikuwa peke yangu


Kitale: Ulipewa taarifa ya vipimo?


Shahidi: Sikupewa


Kitale: Daktari alikwambiaje?


Shahidi: Aliniambia mguu umeteguka, na kusababisha uvimbe


Kitale: Shahidi hayo Daktari aliyokwambia ndiyo aliyoandika humu?


Shahidi: Sikuweka kuona kwa sababu PF3 alibaki nayo ila alinipa dawa ya kuchua na maumivu


Kitale: Ulianza kwenda hospitali au kwenda hospitali?


Shahidi: Nilianza kuandika maelezo kabla ya kwenda hospitalini


Kitale: Shahidi wewe kwa kujiangalia huo mguu ulikuwa na uwezo wa kutembea vizuri?


Shahidi: Nilikuwa nachechemea


Kitale: Nani aliendesha gari lako kutoka eneo la tukio hadi Kituoni


Shahidi: Aliendesha mwenzangu Koplo Mabala


Kitale: Ni vitu gani ulivyoona vilikuwa vimepekuliwa na kukamatwa kwa Zumaridi


Shahidi: Sifahamu kwa sababu mimi nilibaki kwenye gari


Kitale: Shahidi unafahamu Mfalme Zumaridi alikamatiwa wapi?


Shahidi: Sikumbuki, nilimuona wakati anapakiwa kwenye gari


Kitale: Kuna utofauti kati ya jiwe na mawe?


Shahidi: Sifahamu


Kitale: Sasa wewe kwenye sehemu zako za mwili ulipigwa na nini jiwe au mawe?


Shahidi: Jiwe


Kitale: Na siyo mawe?


Shahidi: Ndiyo


Kitale: Ni mwafrika gani mwingine uliyemuona amepata madhara kwenye hilo tukio?


Shahidi: Sajenti Evodius


Kitale: Ulimuona aliyemuwekea hayo majeraha?


Shahidi: Sikumuona


Kitale: Ulifahamu silaha iliyomjeruhi?


Shahidi: Sifahamu


Kitale: Siku hiyo ulikuwa na Inspekta Temi?


Shahidi: Ndiyo


Kitale: Umeeleza kwamba kiongozi wa msafara alipaza sauti, tutajie maneno aliyoyapaza?


Shahidi: Sikuweza kusikia kwa sababu gari yangu ilikuwa ya tatu nyuma


Kitale: Sina swali jingine


MWISHO.

This page might use cookies if your analytics vendor requires them.