Shaka amfananisha Rais Samia kama kulwa na doto katika maendeleo

Muktasari:

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapindizi (CCM), Shaka Hamdu Shaka ameanza ziara ya siku tano Mkoa wa Tabora kukagua utekelezaji wa Ilani ya chama hicho 2020/25

Tabora. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapindizi (CCM), Shaka Hamdu Shaka amesema Rais Samia Suluhu Hassan katika suala la kusukuma na kuleta maendeleo ya nchi kama Kulwa na doto.

 Amesema hayo leo Jumanne, Agosti 16,2022 katika wilaya ya Kaliua baada ya kukagua ujenzi wa hospitali ya Kata ya Mwongozo katika kijiji ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya siku tano kukagua utekelezaji wa Ilani ya chama hicho 2020/25 mkoani Tabora.

Amesema hospital hiyo ujenzi wake ulisimama kwa muda wa miaka 10 toka 2012 hadi 2022, lakini ndani ya mwaka mmoja ambao Rais Samia yupo madarakani ujenzi wa mradi huo umekamilika baada ya kuidhinisha fedha za ukamilishwaji.

“Mama Samia halali kuhakikisha anawaletea Watanzania maendeleo kwa kuwa ndio kipaumbele chake cha msingi katika kuwatumikia Watanzania kwa kuwajengea vituo vya afya watu wapate huduma bora,” amesema Shaka

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Paulo Chacha amesema licha ya kukamilika ujenzi huo ili kiweze kuanza kazi hivyo wanaiomba Serikali kuwapelekea watumishi.

"Kituo hiki kitakuwa msaada kwa wakazi wa kata hii ya Mwongozo na wale wa vijiji vya Kata jirani na katika kuhakikisha tunapata watumishi tumeandika barua kwa Serikali kuomba watumishi wa serikali," amesema Chacha