Shangwe askari 34,000 wakipandishwa vyeo

Shangwe askari 34,000 wakipandishwa vyeo

Muktasari:

  • Wizara ya Mambo ya Ndani imetekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuwapandisha vyeo maofisa, wakaguzi na askari 34,106 wanaotoka majeshi ya polisi, magereza, uhamiaji pamoja zimamoto na uokoaji.

Dar es Salaam. Wizara ya Mambo ya Ndani imetekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuwapandisha vyeo maofisa, wakaguzi na askari 34,106 wanaotoka majeshi ya polisi, magereza, uhamiaji pamoja zimamoto na uokoaji.

Uamuzi huo ulitangazwa na Waziri wa wizara hiyo, George Simbachawene wakati akizungumza na waandishi wa habari Dodoma jana, huku akieleza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la mkuu wa nchi.

“Nawapongeza maofisa, wakaguzi na askari wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama waliopandishwa vyeo. Wamepandishwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi,” alisema Simbachawene.

Alisema askari 34,106 walistahili kupandishwa vyeo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/19, 2019/20 na 2020/21.

Akifafanua, alisema askari 26,464 wa jeshi la polisi wamepandishwa vyeo, “kati yao warakibu waandamizi wa polisi 110 wamepandishwa cheo cha makamishna wasaidizi. Warakibu wa polisi 110 wamepandishwa cheo cha warakibu waandamizi wa polisi.

“Warakibu wasaidizi wa polisi 241 wamepandishwa cheo cha kuwa warakibu wa polisi. Wakaguzi wa polisi 745 wamepandishwa cheo cha warakibu wasaidizi wa polisi, huku wakaguzi wasaidizi 890 wamepandishwa cheo cha wakaguzi wa polisi,” alisema Simbachawene.

Pia, alisema jumla ya askari R & F 4,148 wamepandishwa vyeo kuwa wakaguzi wasaidizi wa polisi. Pia askari R & F 20,220 wamepandishwa vyeo kutoka polisi konstebo kwenda koplo 13,751, na kutoka koplo kwenda sajini 5,619.

Waziri Simbachawene alisema kutoka sajini kwenda stafu sajini ni 800 na kutoka sajini kwenda meja ni askari 50, huku jeshi la magereza likiwapandisha vyeo jumla ya maofisa wakaguzi na askari 6,310.

Alisema kati ya hao, warakibu waandamizi wa magereza saba wamepandishwa cheo kuwa makamishna wasaidizi wa magereza na warakibu wa magereza 14 wamepandishwa cheo kuwa warakibu waandamizi wa magereza.

“Wakaguzi wa magereza 75 wamepandishwa cheo kuwa warakibu wasaidizi wa magereza. Wakaguzi wasaidizi wa magereza 69 wamepandishwa kuwa wakaguzi wa magereza, huku askari magereza 938 wenye ngazi R&F wamepandishwa kuwa wakaguzi wasaidizi wa magereza,” alisema Simbachawene.