Sheikh Poli atahadharisha kuhusu corona

New Content Item (4)
Sheikh Poli atahadharisha kuhusu corona

Muktasari:

  • Waislamu wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa homa ya mapafu (COVID-19).

Dar es Salaam. Waumini wa dini ya Kiislamu wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi virusi vya corona.

Wito huo umetolewa leo Alhamisi Mei 13,2021 na Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Aswar Sunna, Sheikh Juma Poli wakati wa swala ya Idd El Firtri iliyofanyika katika msikiti wa Answaar uliopo Kinondoni, Dar es Salaam.

Amesema kufuatia ugonjwa huo hatari taarifa za nchini India zinaeleza kuwa idadi kubwa ya watu wameendelea kupoteza maisha.

“Nasaha za viongozi wetu kutushauri tuendelee kuchukua tahadhari kwa kunawa mikono na maji yanayotiririka pamoja na kuziba pua na mdomo.

“Tumeona viongozi wetu wanachukua tahadhari na sisi hatuna budi kuendelea kufuata maelekezo ya watalamu wa afya na hata mashekh wetu wameendelea kusisitiza hilo,”amesema Sheikh Poli..

Akizungumzia hitimisho la mwezi mtukufu wa Ramadhani,  Sheikh Poli amesema kwa muislamu anapofanya jema moja basi hulipwa mara kumi .

“Binadamu anaweza kuteteleza kwa njia yoyote ya kibinadamu, lakini baada ya mfungo huu Mungu huleta furaha. Tumefunga siku 30 sio rahisi kumaliza salama, watu wakiwa kwenye mfungo hukutana na vitu mbalimbali nakutokana na mchanganyiko sio rahisi kumaliza salama,” amesema na kuongeza:

“Kwa Muislamu anapofunga Ramadhani anakuwa amtekeleza mfungo kamili kwa kuwa ni nguzo moja wapo muhimu.”