Shigongo anza utekelezaji kuwasaidia wanafunzi Buchosa

Muktasari:

  • Mbunge wa Buchosa (CCM), Erick Shigongo ameanza kampeni ya kusaidia watoto wanaotoka kwenye familia zisizo na uwezo wa kuwapatia vifaa vya shule.


Buchosa. Mbunge wa Buchosa (CCM), Erick Shigongo ameanza kampeni ya kusaidia watoto wanaotoka kwenye familia zisizo na uwezo wa kuwapatia vifaa vya shule.

Vifaa hivyo ni sare na madaftari kwa ajili ya wanafunzi wa  darasa la kwanza kwa  shule 99 za jimbo hilo.

Hadi sasa ameshatoa sare 207   na madaftari  6014 kwa watoto wa kata tisa  kati ya kata 21 zinazounda  za jimbo hilo.

Shigongo amesema jambo hilo ni kati ya ahadi alizozitoa wakati wa kampeni wakati akiomba wananchi wamchague awe mbunge.

"Nitatoa kwa shule zote na kampeni hii ni endelevu lazima watoto waendee shule elimu ni mtaji ,elimu ni maisha," amesema Shigongo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Buchosa,  Idama Kibanzi amesema huu ni mwanzo mzuri kwa mbunge huyo ikiwa ni miezi mitatu tu tangu alipochaguliwa.

Mmoja wa wakazi wa Buchosa, Happiness Juma amesema, “tunashukuru kwa kampeni hii ambayo imesaidia kuwainua watoto wanaotoka kwenye familia masikini.”