Shinikizo la damu chanzo kifo cha Ole Nasha

Ole Nasha kuzikwa kijijini kwake

Muktasari:

  • Serikali imesema  kifo cha Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, William Ole Nasha kimetokea baada ya kupata shinikizo la damu.



Dodoma. Serikali imesema  kifo cha Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, William Ole Nasha kimetokea baada ya kupata shinikizo la damu.

Katibu mkuu Wizara ya Uwekezaji Profesa Godius Kahyarara amesema ugonjwa huo alikuwa nao tangu mwaka 2014.

Historia imemtaja Ole Nasha kuwa katika utumishi wake bungeni kwa miaka sita, alifanikiwa kutoa hoja 16, maswali ya msingi 166 na nyongeza 318.

Ole Nasha alifariki dunia Septemba 27, 2021 akiwa nyumbani kwake mtaa wa Medeli jijini Dodoma na mwili wake unatarajia kusafirishwa kesho Ijumaa Oktoba Mosi, 2021  kwenda Ngorongoro na  mazishi yatafanyika Jumamosi Oktoba 2, 2021.

Katika taarifa yake Profesa Kahyarara amesema kifo cha Ole Nasha kilikuwa cha ghafla kwani walifanya naye vikao katika mradi wa Bagamoyo.

"Tulikaa vikao vya pamoja katika mradi wa Bagamoyo, baada ya hapo mwenzetu aliamua kupitia Arusha na siku aliporudi ghafla umauti ulimkuta," amesema Kahyarara.

Amesema hadi mauti unamkuta alikuwa ni mtu aliyekuwa kiunganishi kikubwa kwa watumishi katika maeneo aliyopitia kwa utumishi wake.

Kwa upande wake naibu Waziri wa Mifugo Abdalah Ulega amezungumzia Ole Nasha kuwa aliacha alama kwa naibu Mawaziri wenzake na hata Wizara ya Mifugo aliyohudumu.

Ulega amemtaja Ole Nasha katika kipindi cha uhai wake kuwa alikuwa mtu mcheshi na mwenye kupenda utani hasa kwa wapenzi wa timu ya Yanga yeye akiwa mshabiki wa Simba.


Imeandikwa na

Habel Chidawali na Amedeus Moshi, Mwananchi