Shirika lahamasisha usafi wasichana wakati wa hedhi

Muktasari:

  • Wakati Dunia ikiadhimisha siku ya maji, ikiwa na kauli mbiu ya ‘Harakisha upatikanaji wa maji kupambana na mabadiliko ya tabia nchi,’ shirika la WaterAid limesisitiza upatikanaji wa maji na usafi ili kuwawezesha wasichana kwenda shule.

Dar es Salaam. Katika kuadhimisha siku ya maji duniani yenye kauli mbiu ya ‘Harakisha upatikanaji wa maji kupambana na mabadiliko ya tabia nchi,’ shirika la WaterAid limesisitiza upatikanaji wa maji na usafi ili kuwawezesha wasichana kwenda shule.

Inakadiriwa kuwa, asilimia 2 tu ya wanawake nchini hawa walio mijini ndiyo hutumia taulo za kike za kutupa baada ya matumizi wakati wa hedhi, huku wasichana wengi hasa vijijini wakitumia vitambaa au pamba kujitunza wakati huo.

Inakadiriwa kuwa asilimia 34 ya wasichana nchini hushindwa kwenda shule kati ya siku nne hadi tano wanapokuwa katika hedhi, kwa kuhofiwa aibu ya kudhalilishwa wanapokuwa kwenye siku zao, huku wengine wakishindwa kabisa kuendelea na masomo.

Akizungumza kupitia taarifa iliyotolewa na Water Aid Tanzania, Mkurugenzi wa shirika hilo, Anna Mzinga amesema kutopatikana kwa vifaa vya usafi wa mazingira kumekuwa sababu ya wasichana wengi kuwa watoro shuleni.

“Asilimia 34 ya wasichana wameshindwa kwenda shule wakati wa hedhi kwa kukosa vyumba vya kubadilishia nguo, huku asilimia 26 wakidai kukosa vyoo bora na safi,” amesema.

Amesema shirika hilo lina mpango wa mkakati wa miaka mitano kuanzia mwaka 2023-28 ifikapo Mei mwaka huu ukilenga kupambana na ukosefu wa maji na kuhakikisha upatikanaji wa mazingira safi.

“Tutaendelea kushirikiana na wadau kuhamsisha upatikanaji wa sera na bajeti itakayowezesha kuwepo kwa usafi, upatikanaji, utakaohusisha jinsia na jamii na upatikanaji wa maji endelevu,” alisema Mzinga. 

Amesema upatikanaji wa maji na usafi wa mazingira na rasilimali zake utaimarisha afya ya watoto, familia na jamii na kuleta uchumi imara na fursa za mafanikio.

“Upatikanaji wa maji na usafi wa mazingira unahitajika kwa ajili ya kuimarisha afya na maisha bora yatakayowezesha na ukuaji wan chi wenye tija,” alisema.