Shirika latenga Sh170 milioni kupambana na ukatili wa jinsia Shinyanga

Shirika latenga Sh170 milioni kupambana na ukatili wa jinsia Shinyanga

Muktasari:

  • Wadau wa masuala ya jinsia wametakiwa kuongeza nguvu katika mapambano dhisi ya ukatili wa kijinsia mkoani Shinyanga.

Shinyanga. Mfuko wa Ruzuku wa wanawake Tanzania (WFT) imetoa ufadhili wa Sh170 milioni kwa mashirika saba yasiyo ya kiserikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia mkoani humo.

Akizungumza jana katika utoaji wa ufadhili huo jana Januari 13, mwakilishi wa mfuko wa (WFT) mkoani Shinyanga, Glory Mbia, ameyataja mashirika na taasisi zilizofaidika na ufadhili huo kuwa pamoja na dawati la jinsia, chama cha Waandishi wa habari mkoani Shinyanga, Radio Faraja, WEADO, Agape, Thubutu Afrika Intiatives, Rafiki SDO, Yawe, GCI, na Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

"Sisi binafsi tunatarajia kwenye utekelezaji wa mradi huu, kuleta mabadiliko chanya ndani ya jamii, na kupunguza ama kutokomeza kabisa matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto nakuhakikisha amani inakuwepo," amesema Mbia.

Akizungumzia hali ya ukatili wilayani Shinyanga, Mkuu wa Idara ya maendeleo ya jamii Halmashauri hiyo, Deus Mhoja amesema hali ya matukio ya ukatili wa kijinsia siyo mbaya ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

"Kwa sasa matukio yaliyopo ndani ya jamii ni ulawiti wa watoto, ubakaji, vipigo, mimba na ndoa za utotoni, ambayo ndiyo wanashirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kuyatokomeza, yakiwamo mashirika yasiyo ya kiserikali, na vyombo vya habari vimesaidia sana kupunguza ukatili wa kijinsia," amesema Mhoja.

Mgeni rasmi wa uzinduzi huo alikuwa Stewart Makali, ambaye ni Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, akimwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, amewataka wadau hao wakazitumie fedha za mradi huo kwa malengo yaliyokusudiwa, na kuibadilisha jamii kuachana na matukio ya ukatili.

Akizungumza kwa niaba ya waandishi wa habari mratibu ya waandishi wa habari mkoani Shinyanga, Estomini Henry  ameomba ushirikiano kutoka kwa viongozi wakati wa utekelezaji wa mradi huo, kuanzia ngazi ya kata na wasiwanyime taarifa wala kutopokea simu, ili kuhakikisha tatizo la ukatili linatoweka kabisa.