Shughuli, televisheni zinavyositisha kulala

Muktasari:

  • “Siku hizi watu hawapati usingizi wa kutosha. Suala la kulala halipo kwenye vipaumbele vyao, wanaamini wana mambo mengi ya kufanya kwa familia au hata shughuli ya kuwaingizia kipato, hawaelewi jinsi usingizi wa kutosha ulivyo muhimu.”

“Siku hizi watu hawapati usingizi wa kutosha. Suala la kulala halipo kwenye vipaumbele vyao, wanaamini wana mambo mengi ya kufanya kwa familia au hata shughuli ya kuwaingizia kipato, hawaelewi jinsi usingizi wa kutosha ulivyo muhimu.”

Kauli hiyo inaelezwa na mtaalamu wa saikolojia wa Marekani, Dk Michelle Drerup, alipohojiwa na Jarida la Afya la Health Essential.

Dk Drerup anasema hata kama ukijitahidi kiasi gani kuzingatia mlo kamili na kufanya mazoezi, huwezi kuwa na afya nzuri kama hutapata muda wa kutosha wa kulala.

“Siku zote tunapendekeza lishe bora na mazoezi kwa kila mtu, lakini kwa misingi hiyo hiyo tunapendekeza kulala vizuri. Usingizi ni muhimu kwa afya zetu. Kwanza kabisa tunahitaji kufanya usingizi kuwa kipaumbele,” anasema mtaalamu huyo.

Kauli ya Drerup inaakisi maisha ya Watanzania wengi, hasa vijana ambao kulala sio kipaumbele na wako tayari kutumia muda wa usiku kwa ajili ya starehe, shughuli za kiuchumi au anasa nyingine kuliko kupumzika.

Seleman Kassim, ambaye ni dereva wa daladala anasema kwa siku analala wastani wa saa tatu hadi nne, anaamka alfajiri ya saa 10 kwa ajili ya kuanza majukumu yake ya siku ambayo mara nyingi anayahitimisha saa sita usiku.

“Hilo suala la kulala nafikiri linaendana na shughuli ya mtu, mimi nakaa Kawe lazima saa 10 alfajiri niwe barabarani kufuata gari Tegeta, nitafanya kazi kutwa nzima namaliza saa tano nirudishe gari kwa bosi halafu nianze safari ya kurudi nyumbani. Hapo hadi nilale inaweza kufika saa saba ndio unapata muda wa kujiegesha kidogo ukisubiri kukuche udamke tena,” anasema Kassim.

Ukiacha na Kassim anayelazimika kulala muda mfupi kutokana na shughuli anayofanya, wapo ambao hawapati muda wa kutosha wa kulala kwa sababu ya kutoa kipaumbele kwenye mambo mengine ambayo wanaona wana tija kwao.

Mariam Seif anasema huwa hapati muda wa kutosha wa kulala kutokana na vipindi vya televisheni anavyolazimika kuvifuatilia usiku akirudi nyumbani.

“Mimi narudi nyumbani kwenye saa tatu hivi, lakini kuna tamthiliya nazipenda huwa zinaanza saa moja hivyo nalazimika kuangalia marudio. Ili nizione zote naweza kujikuta naingia kulala saa saba au saa nane. Mwanzoni nilikuwa naumwa kichwa, lakini siku hizi nimeshazoea lazima kila siku niangalie.”

Christina Mbugi, mkazi wa Mbagala anasema kuna changamoto, hasa kwa familia maskini kuwa na ratiba ya kulala kama inavyopendekezwa kitaalamu, huku akiainisha kipato kuwa ni kichocheo kikubwa cha kutofikia malengo hayo.

“Kwa familia bora ni suala linalowezekana, hawa wana ratiba za kulala, hasa kwa watoto wao. Kwa watu wasio na kipato cha uhakika, hilo ni jambo gumu kulitekeleza. Siyo jambo la kushangaza kukutana na mtoto anafanya biashara hadi usiku mwingi, watoto kama hawa hawapati muda wa kutosha,” anasema Christina.

“Sio mijini tu, hata vijijini kuna changamoto hii zaidi, kwa kuwa licha ya kutokuwa na uhakika wa mazingira bora ya kulala, lipo suala la ukubwa wa familia.

“Familia hizo vijijini unaweza ukakuta watoto zaidi ya watatu wanalala kitanda kimoja, hapo bado usiku kucha mtu anafukuza mbu. Hata kama aliingia chumbani saa tatu usiku, unakuta muda aliolala ni mfupi,” anasema Christina.

Muda gani sahihi wa kulala

Ripoti ya Taasisi ya National Sleep Foundation ya Washington Marekani, imetoa mwongozo wa kulala kulingana na makundi ya umri, huku muda mfupi wa kulala ukiwa ni saa saba kwa watu wenye umri kuanzia miaka 65 na kuendelea.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu wenye umri kuanzia miaka 65 wanatakiwa kulala kati ya saa saba na nane, watu wazima (26 hadi 64) wanapaswa kulala kwa saa saba hadi tisa kwa siku kama ilivyo kwa wenye umri kati ya miaka 18 na 25.

Vijana walio kwenye rika balehe ambao ni kati ya miaka 14 hadi 17 wanatakiwa kulala kwa kati ya saa nane hadi 10, huku watoto wenye miaka sita hadi 13 wanapaswa kulala kwa saa tisa hadi 11.

Kwa watoto wenye miaka kati ya mitatu hadi mitano wanatakiwa kulala kwa saa 10 hadi 13, wenye mwaka mmoja na miaka miwili wanapaswa kulala kwa saa 11 hadi 14 wakati wenye miezi minne hadi 11 muda sahihi wa wao kulala kwa siku ni kati ya saa 12 hadi 15.

Watoto wachanga wenye umri kati ya siku moja hadi miezi mitatu hawa wanahitaji kupata muda mwingi zaidi wa kulala na inashauriwa mtoto mwenye umri huu alale kati ya saa 14 hadi 17.


Madhara ya kutolala

Daktari bingwa wa mfumo wa vichocheo, Profesa Andrew Swai anasema kutopata muda wa kutosha wa kulala kunachangia kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCDs) ikiwamo kisukari.

Anasema kuna ongezeko la vijana kuangukia kwenye kundi la magonjwa yasiyoambukiza, mfano kisukari ikichangiwa na kutopata muda wa kutosha wa kupumzisha mwili kwa maana ya kulala.

“Vijana wengi wa sasa kukosa muda mzuri wa kulala na kupumzika, akitolea mfano tabia ya vijana ya kukesha kwenye kumbi za starehe, kukesha kwenye simu na kompyuta au watoto kuangalia televisheni hadi usiku mwingi,” anasema Profesa Swai.

“Homoni nyingi zinazohusika na ujenzi wa mwili huwa zinatolewa usiku wakati umepumzika, kisayansi usiku ni kama tunaenda garage; sasa vijana wengi badala ya kupumzika usiku muda huo ndio wanahangaika huku na kule. Usipopumzika vya kutosha kisukari, presha, saratani lazima vitakunyemelea”.

Ukosefu wa usingizi kwa muda mrefu pia unaweza kuathiri mwonekano, inaweza kwenda mbele zaidi na kuifanya ngozi kupoteza mvuto wa asili, kupata makunyanzi na hata kuwa na weusi chini ya macho.

Akizungumzia hali hiyo, daktari bingwa wa magonjwa ya akili wa Wizara ya Afya, Erasmus Mndeme anasema licha ya kuwa watu wengi wanashindwa kufuata miongozo ya kiafya, ikiwemo kulala kwa saa nane kuna namna ambayo mwili wenyewe utaonyesha unahitaji mapumziko.

“Hakuna anayeweza kupambana na usingizi, ndiyo maana hata hao wanaopata muda mfupi wa kulala kuna muda tu watasinzia hata kama ni njiani, mwili ulivyoumbwa kuna namna yake ya kujipumzisha, hivyo hata ukiulazimisha utaona unashindwa kufanya kazi yake kwa ufanisi hadi upumzike.

“Inaweza isionekane athari kubwa, ila ukweli ni kwamba, ubongo unachoka na hilo likitokea hata uwezo wa kufanya kazi unapungua. Huwezi kufanya kazi kwa ufanisi kama mwili una uchovu na ubongo haufanyi kazi vizuri, hivyo basi lazima mambo au shughuli unayofanya itakuwa chini ya viwango,” anasema Dk Mndeme.

“Kukosa usingizi wa kutosha pia kunaweza kukapunguza uwezo wa kufikiri, kumbukumbu na kuchakata taarifa kwa maana ya kwamba ubongo unakuwa haufanyi kazi vizuri,” anasema Dk Drerup, kupitia Jarida la Afya la Health Essential.

“Kwa wanaoendesha vyanzo vya moto uchovu unaotokana na kukosa usingizi unaweza kuwa chanzo cha uendeshaji mbovu wa vyombo hivyo na hata kusababisha ajali zinazogharimu maisha ya watu wengine.”