Shuhuda ataja transfoma, moto kiwanda cha Jambo

Kiwanda cha Jambo ii cha utengenezaji wa bidhaa za plastiki  kilichopo eneo la Vingunguti likiteketea kwa moto

Dar es Salaam. Wakati wafanyakazi wa Kiwanda cha Jambo wakisikilizia hatima yao baada ya sehemu ya kiwanda hicho kuungua moto, shuhuda wa kwanza wa tukio hilo, Leila Bhanji amesema alikuta transfoma iliyo pembezoni mwa jengo, moto ulikoanzia likiwa limelipuka.

"Niliona moshi, nilipofika eneo la tukio nikakuta moto umeanza lakini haujashika kasi sana na transfoma likiwa limelipuka," amesema Leila Bhanji ambaye ndiye alipiga simu kwa watu wa zimamoto jana.

Hata hivyo Ofisa Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho kinachotengeneza vitu vya plastiki, hakutaka kuzungumza chochote akisisitiza mkurugenzi ndiye atazungumza.

"Siwezi kuzungumza, director hali yake si nzuri ana presha, akiwa sawa atazungumzia jambo hili," alisema Mtendaji huyo mwenye asili ya India kwa kifupi na kuondoka eneo la tukio.

Mmoja wa wasaidizi wa mkurugenzi ambaye alikuwa akiratibu shughuli za uokozi pia mwenye asili ya India alisema moto huo ulianzia production na stoo.

"Mashine zote zimeteketea, hakuna uzalishaji unaofanyika, kuhusu hatima ya wafanyakazi pia sijui, tuko kwenye presha ya kuzima kabisa moto wote, hadi baadaye ndipo tutajua mambo mengi," amesema.

Baadhi ya wafanyakazi wachache leo walikuwa wakihamisha baadhi ya vitu vilivyonusurika na mito kupeleka eneo jingine, huku baadhi wakihaha bila kujua hatima yao baada ya tukio hilo.

Msimamizi wa kiwanda hicho, Ismail Kondo alisema vitu vilivyokuwa stoo ni viti, madiaba na vikombe ambavyo idadi yake bado haijafahamika.

"Moto ulipoanza, tulipata taharuki, baadae wafanyakazi wakaambiwa warudi nyumbani, wengi hatukuweza kuondoka, tupo tunasikilizia kujua nini kinaendelea, ila imetuumiza sana,"

Hadi leo saa 6 mchana, moto huo ulioanza jana kati ya saa 4 na saa 5 asubuhi ulikuwa umedhibitiwa kwa asilimia kubwa.

Mmoja wa askari aliyeomba hifadhi ya jina kutokana na itifaki alisema sehemu ya ukuta wa jengo la stoo ulibomoka na kuangukia kifusi cha vitu vilivyoungua hivyo kuendelea kusababisha moshi na moto kuasi kuendelea.

"Tunatakiwa kutoa hichi kifusi cha juu hili kudhibiti moto uliopo chini ambao umefunikwa na kifusi," amesema.

Zaidi ya magari manane ya zimamoto ya vitengo tofauti jana na leo yameshirikiana kuuzima moto huo  ulioanzia kwenye stoo ya kampuni hiyo ingawa hadi sasa chanzo chake hakijajulikana.