Siku 1020 za Sabaya wilayani Hai

Lengai Ole Sabaya

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan jana Alhamisi Mei 13, 2021 alimsimamisha kazi mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazomkabili.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan jana Alhamisi Mei 13, 2021 alimsimamisha kazi mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazomkabili.

Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa ilieleza kuwa Sabaya amesimamishwa kazi kuanzia Mei 13. Sabaya aliteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Hai kuanzia Julai 28 mwaka 2018 na Hayati John Magufuli. Kwa uamuzi wa kiongozi mkuu huyo wa nchi maana yake ni kwamba Sabaya atakaa pembeni kusubiri uchunguzi dhidi yake akiwa ameshika wadhifa huo  kwa siku  1020.

Siku 1020 za Sabaya wilayani Hai

Wakati huo, Sabaya alikuwa maarufu kutokana na staili ya uongozi wa kibabe na kuendesha operesheni za kusaka watu aliowatuhumu kuvunja sheria za nchi.

Katika muda aliokaa madarakani, Sabaya amejijengea marafiki na maadui wengi kutokana na utendaji wake uliotafsiriwa kuwa ni wa kibabe. Sabaya alitumia vilivyo sheria ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inayompa mamlaka ya kuwaweka ndani watu kwa saa zisizozidi 48, kwa kuamuru kuwaweka mahabusu watumishi wa taasisi za Serikali hata raia wenye tuhuma.

Mfanyabiashara mashuhuri wa Moshi anayemiliki hoteli ya kitalii ya Weruweru River Lodge, Cuthbert Swai aliwahi kujitokeza hadharani kwenye kikao cha watendaji wa Serikali na wafanyabiashara kilichokuwa chini ya mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira na kumtuhumu Sabaya kwa kumwomba rushwa na kumfanyia fujo hotelini kwake.

Mkuu huyo wa wilaya anatuhumiwa kuvamia hoteli inayomilikiwa na mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe wakati wa uchaguzi mkuu mwaka jana akimtafuta Mbowe kwa malengo yasiyojulikana. Pia Sabaya anahusishwa na kushiriki kampeni dhidi ya Mbowe kwenye uchaguzi wa Jimbo la Hai mwaka 2020 kinyume na majukumu yake.

Mbowe alishindwa ubunge na kiti hicho kilichukuliwa na Saasisha Mafue wa CCM. Pamoja na malalamiko hayo dhidi yake, wapo wananchi na watumishi wa umma waliokuwa karibu na Sabaya ambaye walimuona kama mtetezi na mtatuzi wa kero zao.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amemteua Nsubili Joshua kuwa Karani wa Baraza la Mawaziri. Joshua alikuwa akikaimu nafasi hiyo kabla hajateuliwa jana. Rais Samia pia amemteua Ayub Makoye kuwa Naibu Karani wa Baraza la Mawaziri.

Makoye alikuwa akikaimu nafasi hiyo. “Katika hatua nyingine, Rais Samia amemteua Dk Stergomena Tax kuwa mwenyekiti wa bodi ya Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute). Dk Tax ni katibu mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC),” ilisema taarifa hiyo.

Lengai Ole Sabaya

Taarifa hiyo pia ilieleza Rais Samia amemteua Dk Laurian Ndumbaro kuwa makamu mwenyekiti wa Taasisi ya Uongozi. Dk Ndumbaro ni katibu mkuu katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Sambamba na uteuzi huo, Rais Samia amefanya uteuzi wa wajumbe wa bodi ya Taasisi ya Uongozi ambao ni Balozi Riitta Swan, Profesa Penina Mlama, Lina Soiri, David Walker, Suzan Mlawi, Dk Hamis Mwinyimvua na Profesa Samwel Wangwe. Uteuzi wa wajumbe hao ulianza jana, Mei 13.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amemteua Ishmael Andulile Kasekwa kuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB). Uteuzi wa Kasekwa umeanza Mei 10 akichukua nafasi ya Dk Rosebud V. Kurwijila ambaye amemaliza muda wake.