Simanjiro watakiwa kumaliza migogoro si kukimbilia mahakamani

Muktasari:

Jamii wilayani Kiteto Mkoa wa Manyara ineshauriwa  kutatua migogoro mbalimbali kabla ya kesi kufika mahakamani.Kiteto. Jamii wilayani Kiteto Mkoa wa Manyara ineshauriwa  kutatua migogoro mbalimbali kabla ya kesi kufika mahakamani.

Akizungumza na wafungwa na mahabusu katika gereza la Kiteto leo Jumapili Januari 22, 2023 katika wiki ya sheria hakimu wa mahakama ya wilaya, Mosi Sassy alitaja kauli mbiu ya mwaka 2023 ni umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi katika kukuza uchumi endelevu, wajibu wa mahakama na wadau.

"Kauli mbiu hii imekuja wakati mwafaka kwa kuwa Kiteto ina changamoto ikiwemo migogoro ya ardhi, ndoa na talaka, hivyo kama pande hizo zitatumia mlango wa usuluhishi zitaondokana na gharama za kufuatilia kesi sambamba na kutumia muda mwingi kudai haki," amesema Sassy.

Wakili Ibrahimu Masawe aliwaeleza wafungwa na mahabusu hao kutumia wiki ya sheria kujifunza sheria pale wanapofika wanasheria kuongea nao

Akizungumzia migogoro ya ardhi Kiteto mwendesha mashtaka wa Serikali,  Salimu Issa amesema wananchi wa Kiteto wakiamua kutumia njia ya usuluhishi wa migogoro kama  kauli mbiu ilivyo wataondokana na gharama kubwa wanazotumia kufuatilia kesi zao mahakamani.

"Ukifuatilia kwa ukaribu kesi nyingi Kiteto ni migogoro ya ardhi, sasa hapa pande hizi zingekuwa na uelewa wa usuluhishi wangeondokana na adha wanazopata kila kukicha," amesema.