Simbachawene awaonya polisi kubambikia watu kesi

Simbachawene awaonya polisi kubambikia watu kesi

Muktasari:

  • Waziri Simbachawene ameshauri mafunzo ya polisi kuongezwa kutoka miezi tisa hadi 12 ili kukabili changamoto ya ukosefu wa uadilifu miongoni mwa askari.

Moshi. Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene amelionya Jeshi la Polisi kwa tabia za baadhi ya askari wake kubambika watu kesi, huku pia akitaka mafunzo ya awali ya askari yaongezwe kutoka miezi tisa hadi 12 ili kupunguza changomoto ya ukosefu wa maadili kwa baadhi ya askari.

Akizungumza jana Julai 23 na wakufunzi pamoja na wanafunzi wa shule ya polisi Tanzania (TPS), Simbachawene amesema kumekuwepo na manung'uniko makubwa dhidi ya jeshi la polisi kutoka kwa raia ikiwemo watu kubambikiwa kesi, jambo linaloleta taharuki kwenye jamii.

"Kuna manung'uniko makubwa dhidi ya Jeshi la polisi ,kuna kuonea watu kesi za kubambikiza, hata kwenye uaadilifu katika kumkamata mtu kwa mujibu wa sheria unakuta mtu ambaye hana nia ya kukufanyia fujo wewe unataka kumletea ukamanda wako, sio kila mahali ni vita,"amesema Simbachawene

Amewataka kujitahidi kuwa waadilifu  na kujiepusha na tabia za ulevi
“Jambo ambalo linawaangusha huko mtaani mnakoishi ni tabia zenu ikiwemo pia na ulevi. Ngao mlizovaa ni kwenda kumwakilisha Rais kwenye maeneo mnayosimamia lakini unakuta ni mlevi na mnafanya maamuzi ya ovyo mkifanya hivyo hamtafika mbali."

"Kidogo tunachangamoto katika uadilifu ,wakati mwingine kazi ya polisi inataka kuonekana kama ni kazi ya watu ambao hawamjui Mungu ,kumbakiziza kesi mwenzako wewe ni sawa na muuaji, katika changamoto kubwa katika maisha ni kuuguliwa na kesi kufa sio tatizo," amesema Simbachawene

Kuhusu mafunzo, amesema: “Kuna haja ya kuwekeza katika shule hii ili iweze kutoa mafunzo mazuri ,na nafikiria hata training (mafunzo) yetu ya askari wapya ya miezi tisa naona ni ndogo tufanye miezi 12 watu wapate mafunzo ya kueleweka," amesema Simbachawene

Amesema Wizara hiyo ina kazi kubwa ya kuhakikisha inaandaa askari wenye uadillifu na waliofundishwa vizuri maadili ya kazi.

Naye Mkuu wa shule ya polisi Tanzania (TPS), Ramadhan Mungi amesema kuwa shule hiyo imejipanga kupandisha kiwango bora cha mafunzo yanayotolewa na shule hiyo ili yaweze kujenga weledi na maadili ya Kazi ya polisi.

Aidha alisema wako mbioni kukamilisha stashahada ya uhalifu wa kimtandao na upelelezi wa kisasa (cyber security and digital forensic) kwa kushirikiana na chuo kikuu cha Dodoma.

"Hii itapandisha hadhi hadi ya Jeshi letu ,Wizara pamoja na Taifa kwa ujumla na kuna uwezakano kozi hii kuanza mwaka huu kila kitu kimekamilika," amesema Mungi