Simulizi abiria waliosota saa 18 lori likifunga njia

Simulizi abiria waliosota saa 18 lori likifunga njia

Muktasari:

  • Mamia ya wasafiri na magari yanayotumia barabara ya Morogoro kwenda Dar es Salaam walikwama kwa zaidi ya saa 12 na kulazimika kulala kwenye magari kutokana na lori lililopata ajali kuziba njia.

Dar/Morogoro. Mamia ya wasafiri na magari yanayotumia barabara ya Morogoro kwenda Dar es Salaam walikwama kwa zaidi ya saa 12 na kulazimika kulala kwenye magari kutokana na lori lililopata ajali kuziba njia.

Lori hilo lililokuwa limesheheni magogo lilishindwa kupanda mlima hivyo kuserereka na kufunga barabara katika eneo la Mikese na kuziba njia ya magari yanayotoka Morogoro na Dar es Salaam.

Abiria waliokwama barabarani usiku mzima, wamesimulia mkasa huo huku wakitoa ushauri kwa mamlaka kujenga njia ya mchepuko itakayosaidia kuchepusha magari pindi kunapokuwa na mkwamo kama huo.

Ushauri mwingine wa kukabili foleni barabarani ulitolewa Julai 29 na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) – Bara, Abdulrahman Kinana aliyependekeza Serikali kujenga barabara nane kutoka Dar es Salaam hadi Tunduma mkoani Songwe kutokana na umuhimu wake kwenye uchumi wa Taifa.

Mwananchi juzi ilishuhudia baadhi ya malori yaliyobeba nyanya, ndizi, viazi mbatata, kabichi, mchele hata ng’ombe na mbuzi kwenda Dar es Salaam yakiwa yamekwama.

Mmoja wa wasafiri waliolala kwenye basi akitokea Dodoma kwenda Dar, Leonard Mhongole alisema walikwama barabarani kuanzia saa 12 jioni walipoukuta msongamano mkubwa wa magari eneo la Mikese na kuambiwa kuna ajali ya lori iliyotokea majira ya saa 10 jioni na kuziba njia.

“Tumelala kwenye basi, nimefika nyumbani leo (jana) saa tano kasoro asubuhi. Magari yalikuwa mengi na hakuna pa kupita. Huwezi kwenda mbele wala kurudi nyuma,” alisimulia.

Mhongole alishauri kuwapo magari ya kuondoa magari yanayoharibika barabarani (break down) ili yasaidie kuwavusha abiria kuendelea na safari pamoja na kujengwa kwa njia za mchepuko.

“Madereva nao wafuate sheria, wasitanue kunapotokea ajali, hilo ndilo lilisababisha tukachelewa zaidi kwa sababu ilibidi tupangwe upya, waruhusiwe waliokuwa wametanua ili kufungua njia,” alisema Mhongole.

Mmoja wa madereva aliyekuwa akitokea Dar es Salaam kwenda Kilosa mkoani Morogoro, Fadhil Midege alisema alifika Ubena saa 10 alfajiri, lakini kutokana na foleni ndefu alifika Mikese mzani saa 5 asubuhi.

“Foleni ilikuwa kubwa na hatukujua nini limetokea huko mbele,” alisema.


Tanroads, Polisi wafafanua

Kaimu Meneja wa Tanroads Mkoa wa Morogoro, Mussa Kaswahili alisema baada ya kupata taarifa walikwenda eneo la tukio wakiwa na winchi waliloliazima kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) ambalo halikuweza kulinyanyua lori lililokuwa na mzigo.

“Sisi tulichelewa kupata taarifa za ajali hii, hata hivyo hatuna winchi letu. Kwa kutumia winchi la Temesa, tulikesha eneo la tukio na mpaka saa nne asubuhi barabara ilikuwa imeshafunguka na magari yalikuwa yakiendelea na safari,” alisema Kaswahili.

Akieleza changamoto ya foleni, Kaswahili alisema ilitokea baada ya madereva kukosa uvumilivu hivyo kila mmoja kutaka kuwahi mbele, lakini Jeshi la Polisi liliwasimamia na kuwaruhusu kwa utaratibu mzuri.

Kutokana na foleni hiyo, alisema Tanroads ilisitisha upimaji magari kwenye mzani wa Mikese hadi ilipoisha na usafiri kurejea kama kawaida.

“Tuliona tusitishe huduma ya kupima magari kwa sababu hilo nalo lingechangia foleni na usumbufu kwa sababu Barabara ya Morogoro - Dar es Salaam ilikuwa haipitiki kabisa, huwezi kujua gari hili linaelekea wapi, yaani ilikuwa vurugu tupu,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Musilimu alisema lori hilo lilifunga barabara usiku wa kuamkia jana, bali walishindwa kuliondoa kwa kulivuta kutokana na uzito wa shehena ya magogo iliyobebwa.

“Lori lina mzito mkubwa wa magogo, tulitakiwa kuwa na winchi lenye uwezo mkubwa kunyanyua mzigo huu ili barabara ipitike,” alisema Musilimu.

Hamida Shariff na Juma Mtanda (Morogoro) na Peter Elias (Dar)