Simulizi alivyokimbia ndoa hadi kuwa kinyozi

Simulizi alivyokimbia ndoa hadi kuwa kinyozi

Muktasari:

  • “Wao waliongea tu lakini sisi tulichukulia suala hilo kwa uzito na kuanza kulifanyia kazi.”anasema.

Dar es Salaam. Mara nyingi tumezoea kuona wanaume wakifanya kazi katika saluni za kike na kumudu shughuli zote zinazofanywa na wanawake, ikiwemo utengenezaji wa nywele.

 Lakini ni ngumu kuwakuta wanawake wakifanya shughuli zote katika saluni za kiume, ikiwemo kunyoa nywele kwa ustadi kulingana na matakwa ya mteja.

Lakini Mwananidi Idd ni miongoni mwa wanaojivunia kuwa vinyozi na sasa anamiliki saluni yake mwenyewe ambayo Oktoba mwaka huu inatimiza miaka mitatu, huku ikifikisha thamani ya takribani Sh100 milioni.

Akiwa mtu aliyesoma hadi darasa la saba na aliyekimbia ndoa za utotoni baada ya kuolewa kwa zaidi ya mwaka mmoja, kabla ya kujua kunyoa alikuwa ni miongoni mwa wasichana wanaoosha watu walionyolewa.

Wakati akifanya kazi hiyo katika moja ya saluni maarufu ndani ya jiji hili aliamua kufanya kazi hiyo kwa moyo na kuwa tayari kujifunza ujuzi mpya kila alipopata nafasi.

Alikuwa akifanya hivyo kwa sababu ya malengo aliyokuwa nayo ya kujiimarisha kiuchumi, lakini hakuwaza kuwa kinyozi.

“Ilitokea tu kuanzia saa 1 jioni, vinyozi wengine walikuwa wanaondoka na anabaki mmoja tu ambaye kwa sasa ndio mmiliki mwenzangu anaitwa Mohammed, unakuta amezidiwa na wateja, jambo ambalo lilikuwa likimfanya kuniambia kama ungekuwa unajua kunyoa ungenisaidia,” anasema Mwanaidi.

Anasema hilo lilikuwa likijenga kitu ndani yake na kumfanya kuzingatia zaidi kile kinachofanywa na vinyozi ili kujifunza.

“Kuna wakati alikuwa akiniambia huyu anataka kunyoa kipara tu si unaweza, na mimi nakubali kuwa naweza kwa sababu mara zote nilikuwa nikiwaangalia namna wanavyofanya hivyo nikijaribu nafanikiwa kunyoa,” anasema Mwanaidi.

Anasema haikuchukua muda mrefu yeye kufahamu aina tofauti za unyoaji kibunifu, kabla ya mwaka 2017 kuamua kwenda kujifunza masuala ya urembo yanayojumuisha pedicure, manicure, massage na matibabu ya ngozi aina zote.

Walifunguaje saluni

Anasema haikuwa jambo rahisi kufika alipo sasa, kwani kabla ya kufungua ofisi hiyo amefanya kazi saluni tofauti, katika kipindi hicho walikuwa wakinunua kifaa kimoja kimoja kila walipopata pesa na kukitunza.

“Hata tulipohamia hapa tulikuwa na eneo dogo sana tofauti na sasa ambapo kuna maeneo tofauti, ikiwemo daraja la kawaida, la pili na VIP ambako watu hupatiwa huduma tofauti,” anasema Mwanaidi.

Anasema wakati wakihama katika saluni tofauti wateja wao walikuwa wakiwafuata kila wanapokwenda, jambo ambalo liliwafanya kuchoka na kuwataka wafungue eneo lao wenyewe la biashara ili wasiwapoteze.

“Wao waliongea tu lakini sisi tulichukulia suala hilo kwa uzito na kuanza kulifanyia kazi,” anasema.

Rahisi kiasi gani?

Anasema ikiwa mtu anapenda na kuamini anachokifanya kuwa kitaweza kumtoa ni rahisi kutimiza malengo yake, lakini mara nyingi wasichana wanaofanya kazi saluni wamekuwa hawadumu hata kwa miezi miwili.

“Wadada wengi wa saluni wamekuwa hawadumu hata miezi miwili kwa sababu huenda hawapendi wanachokifanya, lakini wangekuwa wanaamini kuwa wanachokifanya kitawasaidia wangekuwa wanatulia,” anasema Mwanaidi.


Jamii inamuonaje kinyozi mwanamke?

Anasema katika saluni yake wapo vinyozi wawili wa kike ambao wanafanya kazi vizuri, huku akibainisha kuwa utendaji kazi wao wakati mwingine huzidi hata wavulana.

“Hata mteja anapokuja kwa mara ya kwanza na kukuta kinyozi ni mwanamke huwa na mshangao na kutamani kuhudumiwa nao, hili humfanya atamani kurudi mara kwa mara na hawa wana wateja wengi kuliko wanaume,” anasema Mwanaidi.

Mbali na vinyozi, saluni hiyo ina wafanyakazi 25 ambao wapo vitengo mbalimbali, ikiwemo vinyozi, waoshaji, wataalamu wa masula ya urembo.

Akiwa ni mama wa watoto wawili, amekuwa mara nyingi mtu wa mwisho ambaye hufunga saluni hiyo saa 4 hadi 5 usiku, ikiwa ni baada ya kutoka nyumbani kwake saa 2 asubuhi.


Kwa nini alikimbia ndoa?

Akiwa mzaliwa wa Kondoa jijini Dodoma, anasema baada ya kuolewa alikaa katika ndoa kwa zaidi ya mwaka, lakini kutokana na kuona hana uwezo wa kuhudumia ndoa aliamua kutoroka.

Anasema hata siku aliyoamua kuondoka eneo hilo alipanda malori yanayobeba mizigo yaliyokuwa yakiondoka saa 10 alfajiri.


Changamoto

Uwepo wa virusi vya Uviko-19 umeathiri pia biashara yao, kwani baadhi ya wateja waliokuwa wakifika katika ofisi yao kufuata huduma sasa hawaendi

“Hili pia lipo kwa baadhi ya wateja ambao tulikuwa tunawafuata nyumbani kunyoa, hawataki sisi twende na ofisini hawaji, hivyo kwa kiasi tumepoteza wateja,” anasema Mwanaidi.

Anasema wakati mwingine pia amekuwa akikutana na changamoto mbalimbali, ikiwemo maneno ya kukera kutoka kwa wanaume.

“Wakati mwingine unawaza kwa nini huyu ameniambia hivi, unajizuia kumjibu kwa sababu ni mteja wako na ukimjibu vibaya utampoteza,” anasema Mwanaidi.

Lakini uwepo wa changamoto hizo haijawa kikwazo kwao, kwani moja ya malengo ni kuwa na saluni inayotembea (mobile barbershop) itakayokuwa ikitoa huduma zote ndani ya gari, ikiwemo kunyoa na kuosha.

“Pia malengo yetu mengine ni kuwa na nyumba yetu yenyewe pamoja na chuo ambacho kitakuwa kikitoa mafunzo ya kunyoa, hususan kwa wadada, pia kuwafundisha namna ya kuthamini kazi wanazofanya,” anasema Mwanaidi.