SIMULIZI: Mwanajeshi aliyejiua juu ya kaburi la mkewe Dar es Salaam

SIMULIZI: Mwanajeshi aliyejiua juu ya kaburi la mkewe Dar es Salaam

Muktasari:

Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Reginald Ruta amekutwa amekufa huku mwili wake ukiwa juu ya kaburi la mkewe, Godebertha aliyezikwa katika makaburi ya Mekyuri Kipawa jeshini mkoani Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Reginald Ruta amekutwa amekufa huku mwili wake ukiwa juu ya kaburi la mkewe, Godebertha aliyezikwa katika makaburi ya Mekyuri Kipawa jeshini mkoani Dar es Salaam.

Juni 7, mwaka huu mwili wa askari huyo aliyezikwa katika makaburi hayo jana, ulikutwa katika kaburi la mkewe aliyefariki dunia Alhamisi iliyopita baada ya kuugua ghafla.

Kifo cha askari huyo wa kambi ya Msata mkoani Pwani kimeacha simanzi kwa ndugu, jamaa na marafiki, kwa kuwa kilitokea siku tatu tangu mkewe afariki.

Akisoma risala kwenye ibada ya kuaga mwili wa askari huyo, iliyofanyika nyumbani kwake mtaa wa Karakata Kipawa, diwani wa Karakata, Idary Karugendo alisema marehemu ameacha watoto wanne na wajukuu watano waliokuwa wanamtegemea.

“Mzee Ruta alikuwa tegemeo kwenye familia yake kama baba, hasa baada ya kifo cha mke wake kutokea siku chache zilizopita,” alisema Karugendo.

Akizungumza katika ibada hiyo, Katekista wa Kanisa Katoliki la Bikira Maria Kipawa, Silivester Sadick alisema kifo hicho ni funzo kubwa kwa watu wote na kinaonyesha wazi hakuna binadamu mkubwa mbele ya Mungu.

“Juzi tulikuwa hapa hapa, tena nawaongoza kwenye ibada ya kumuaga mke wake, hakuna aliyekuwa anajua nani anafuata lakini leo mzee Ruta anafuata, ni funzo kubwa ndio maana nawakumbusha kuzidi kumuomba Mungu wakati wote,” alisema.

Alisema kifo kinaharibu mipango yote ambayo binadamu anakuwa amejipangia kuitekeleza na ndiyo maana watu husema kifo hakina huruma, lakini ukishakufa unakwenda kwa Mwenyezi Mungu.

“Maisha ya hapa duniani yanapita, juzi tulizungumza hatujui nani anafuata, lakini mume ameenda, kama maisha yetu yako namna hii binadamu ni nani mbele ya Mungu.

Familia ipo kwenye wakati mgumu, kama ingekuwa ni mimi leo ingekuwaje, kikubwa tujitengenezee njia ya kufika mbinguni mapema na naiomba familia kuzidi kufanya maombi na kusimama katika imani kwa Mungu kwani hawezi kuwaacha,” alisema.

Kifo kilivyotokea

Kwa mujibu wa jirani mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake, alidai kuwa walikuwa wote na Ruta siku ya Jumamosi ambayo yalifanyika mazishi ya mkewe aliyefariki ghafla wakati akijiandaa kwenda kazini.

Alisema baada ya mazishi Jumatatu iliyopita, vijana waliokuwa wanachunga mbuzi waliukuta mwili wake juu ya kaburi hilo.

Chanzo hicho kilieleza kwamba watoto hao baada ya kuona mwili huo wakaenda kutoa taarifa jeshini kwa sababu eneo hilo linamilikiwa na Jeshi na walipofika pale wakampekua hawakuona chochote zaidi ya kitambulisho chake.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa baada ya mazishi ya mkewe, Jumapili iliyopita Ruta alifanya vikao vya mara kwa mara na watoto wake wanne na kuwaeleza mali alizonazo na sehemu zilipo.

“Baada ya kufanya vikao virefu na watoto wake huku akiwachekesha muda wote, aliwaambia kuwa atakwenda kununua marumaru kwa ajili ya kujengea kaburi la mkewe na aliwaeleza kuwa akishafanya manunuzi atawaeleza,” zinaeleza taarifa hizo.

Habari zaidi zinaeleza kuwa alimuomba mwanaye mmoja ampe Sh50,000 kwa ajili ya kununua marumaru hizo na alipopewa fedha hizo aliondoka nyumbani hakurejea tena.

Polisi wanena

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi Ilala, Janeth Magomi alikiri kupokea taarifa ya kifo na kudai ililetwa na wanajeshi wenzake kutoka kituo cha Polisi Stakishari.

“Kwamba kuna mwenzao wamemkuta amefariki juu ya kaburi la mkewe, wakati wanatoa taarifa hiyo tayari mwili ulishachukuliwa na kupelekwa hospitali ya Lugalo,” alisema Janeth.