Simulizi ya mwanaume alivyonusurika kifo sababu ya ukatili

Muktasari:

  • Takwimu zilizotolewa na Serikali hivi karibuni zinaonyesha kuwapo kwa watoto 5,732 wanaoishi na kufanya kazi mitaani, kati yao wavulana wakiwa 4583 na wasichana 1149.

Takwimu zilizotolewa na Serikali hivi karibuni zinaonyesha kuwapo kwa watoto 5,732 wanaoishi na kufanya kazi mitaani, kati yao wavulana wakiwa 4583 na wasichana 1149.

Sambamba na hilo takwimu hizo zinaonyesha kuwa watoto hao wanaongoza kuwapo katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa asilimia 20, ukifuatiwa na Mkoa wa Dodoma huku watoto hao wengi wao wakiwa na wazazi, walezi, ndugu au jamaa.

Takwimu hizo zilitolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Doroth Gwajima kupitia kamati ya ulinzi wa wanawake na watoto (MTAKUWWA) Mkoa wa Dar e Salaaam.

Simulizi ya James

Gazeti hili limepata wasaa wa kufanya mahojiano na James Yustar, mmoja wa watoto aliyeishi mtaani baada ya kupitia ukatili uliomsababishia kunusurika kifo.

James (28) licha ya kuwa ana unafuu katika uzungumzaji, unahitajika kuwa makini kumsikiliza na kumuelewa kutokana na kigugumizi kikali alichonacho.

James alijikuta akiishi mtaani baada ya mtu aliyeachiwa mali za mama yake mlezi kuzitamani na kutumia watu wamuue ili aweze kuzirithi.

James anasema miaka 28 iliyopita maeneo ya Namanga jijini Arusha mara tu baada ya kuzaliwa, aliokotwa jalalani na mama aliyemtaja kwa jina la Yustar Ebrania.

Anasema mama huyo ambaye wakati huo alikuwa ni mtawa wa kanisa la Katoliki, alimuokota akiwa katupwa kwenye boksi.

“Asubuhi wakati watawa wanakwenda kanisani, jirani na kanisa lao kulikuwa na jalala, hivyo akaona mbwa wakiwa wanaburuza boksi na ghafla akaona wanavuta shuka lililokuwa limejaa damu,” anasema James.

Anaongeza: “Jambo lile lilimfanya kutaka kujua nini kipo ndani yake na alipokaribia alisikia sauti ya mtoto akilia jambo lililomfanya kuomba msaada kwa watu na kuripoti tukio hilo kituo cha polisi.”

Hata hivyo, polisi walichoamua ni kumuomba mtawa huyo kukaa na James mpaka ndugu zake watakapopatikana.

Kuanzia hapo akaanza kumlea na alipofikisha miaka mitano, mtawa Yustar aliliomba kanisa kuacha utawa ili amlee James.

“Baada ya mama (mtawa Yuster) kuacha utawa aliondoka kwenye nyumba za kanisa na kwenda kuanza maisha mapya ambapo alifungua miradi ya maduka ya dawa na kituo cha afya Moshi na Arusha.

Anasema katika safari hiyo mpya ya maisha, mtawa Yustar alizidi kumpenda jambo lililomfanya ajue yule ndio mama yake mzazi.

Hatimaye alimwandikisha shule ya Msingi Arusha International darasa la kwanza, lakini akiwa darasa la tatu mama yake huyo alipata ajali akiwa anatokea Moshi kwenda Arusha yalipokuwa makazi yake.

Katika ajli hiyo alivunjika mbavu jambo lililomfanya kwenda kupatiwa matibabu Afrika Kusini.

James anasema tangu mama huyo apate ajali, hakuwa tena sawa kwani alikuwa akipata magonjwa ya mara kwa mara.

Anasema katika maisha yake ilikuwa ni utaratibu wa mama yake kumfanyia sherehe yake ya kuzaliwa ambapo walikuwa wakitumia siku hiyo kwenda kuwaona watoto katika kituo cha kulelea watoto yatima na wanaoishi mazingira magumu.

“Siku moja katika sherehe yangu hiyo ya kuzaliwa ilikuwa tofauti, kwani wakati tukiwa njiani kurejea nyumbani nilimuona mama akilia sana hadi kushindwa kuendesha gari,” anasema James.

Kutokana na hilo alimpigia simu ‘uncle’ mjomba, aje atuchukue, huyu ni kaka yake ambaye kwa kiasi kikubwa alikuwa akisimamia miradi yake na ndiye alikuwa mkuu wa wafanyakazi na kumuamini hadi majukumu mengine ya nyumbani.

Kitendo kile kilinifanya nimsumbue mama karibu wiki nzima kutaka kujua ni nini kilichomliza na siku moja ndio akakaa chini na kunieleza yote yaliyotokea katika maisha yangu hadi kujikuta ananilea.


Maisha yake yalivyobadilika

James anasema: “Baada ya mama kunielezea maisha yangu hayo ya namna alivyoniokota, pia akanipa historia ya maisha yake kwamba naye aliokotwa na Wazungu kwenye shimo la choo mwaka 1954 akiwa kichanga.”

Anasema Wazungu hao waliokuwa wamisionari, walifika katika kijiji kimoja huko Arusha na kutaka kwenda kujisaidia.

Lakini walipopiga hodi kwenye hiyo nyumba hawakukuta mtu na walipokaribia chooni walisikia sauti ya mtoto ikilia. Wazungu hao walimlea kanisani na waliporudi Ulaya wakaondoka naye na kujikuta anasomea huko.

Ukatili ulipomuanzia

James anasema zikiwa zimepita wiki mbili Yuster aliitisha kikao cha wafanyakazi wote akiwamo mjomba. Katika kikao hicho aliwaeleza wafanyakazi hao kuwa siku atakapoondoka duniani basi mrithi wake ni James na kutaka waendelee kuzisimamia mali hizo na atakapofikisha miaka 18, basi wamkabidhi kisha kumkabidhi nyaraka mbele yao ambapo badaaye alimuonyesha sehemu za kuzificha.

“Tangu alipoweka wazi hilo kwa wafanyakazi, hata miezi mitatu haikuisha mama alifariki na kuanzia hapo maisha yangu yalianza kuyumba.

“Hapo ndio wakati mjomba alianza manyanyaso kwangu, akageuza nyumba yetu danguro kwa kuingiza kila aina ya wanawake na kwa kuwa mimi nililelewa katika maadili ya dini, nilikuwa nikimuasa kuwa anachofanya ni dhambi lakini niliishia kutukanwa,” anasema James.

Anaongeza: ‘‘Kama haitoshi, uncle aliua biashara zote za mama na kufukuza wafanyakazi wote na akaanza kunidai zile nyaraka za mali, alipoona nakataa alinitumia watu wakaniteka nikiwa shuleni na kunipeleka mbali porini kwa kunifunga kamba na kuniingizia matambaa na masponchi mdomoni.

Anasema watu hao walimtamkia waziwazi kwamba wametumwa na mjomba wake wamuue kwa sababu anataka mali.

Walimbeba na kumweka eneo la kilima lililotokana na kifusi kilichochimbwa madini maeneo ya Mererani na kisha kumucha hapo mpaka jioni ambapo walimuambia watarudi kumuua.

Jioni ilipofika, watu hao wakiwa wanarudi alikuwa akiwaona kwenye bonde chini kabla hawajamfikia alipo, ghafla radi ikapiga kubwa na kifusi kilichokuwa eneo lile kikawafukia na hapo ikawa mwisho wa maisha yao.

Anasema baada ya hapo alianza juhudi za kujiokoa akiwa anasota ili kuweza kutoka eneo lile, kitendo kilichomchukua wiki nzima mpaka pale alipookolewa na wasamaria wema akiwa hajitambui.

“Wasamaria hao ambao ni watu jamii ya Kimasai, walinitibu na dawa za kiasili, lakini wakati huo nilikuwa katika hali mbaya sana, nimevimba mwili mzima na kutokana na vitambaa na sponji walivyoniweka mdomoni, mashavu nayo yalivimba hadi upande mmoja kupasuka na kujikuta napitishia chakula hapo,” anasema James.

“Ulimi nao ulikuwa umeoza na nikawa natoa harufu kali mithili ya mzoga damu pamoja na usaha havikuniacha salama na ilinichukua siku tatu kuzinduka na baada ya hapo ndio sikuweza kuzungumza tena,” anasema James.

Anasema nilikaa na wamasai takribani miezi nane na kujikuta nina hamu ya kurudi nyumbani. Katika kunirudisha nyumbani niliondoka nao kwenda mnadani, baada ya kuuza ng’ombe zao walinipatia Sh70, 000 na uzuri nilikuwa napakumbuka nyumbani, nilipofika nilimkuta mlinzi na kunieleza kuwa nyumba hiyo ilishauzwa.

‘‘Nikamuelezea yaliyonikuta na kumuambia kuwa nina hela, ndipo akanipa wazo la kuanza kufanya biashara, tukawa tunauza naye sigara na karanga pale Namanga mpaka tulipoamua kudandia magari na kwenda jijini Dar es Salaam kutafuta maisha,

Anasema walipofika Dar es Salaam malazi yao yalianzia stendi ya Ubungo kabla ya kuhamia chini ya daraja la Ubungo na baadaye kwenye baraza za soko la Kariakoo.

“Kwa kuwa nilikuwa napenda kusoma nilimueleza Bruno kuwa nahitaji kurudi shule na alihakikisha narudi kwa kuanza kuninunulia sare za shule na begi.

Hata hivyo katika shule zote tulizokuwa tunaenda tulikwama tukitakiwa kwenda na mzazi,” anasema James.

Siku moja alifanikiwa kukutana na wanafunzi wa shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, waliokuwa wakilelewa katika kituo cha watoto wanaoishi mazingira magumu cha Dogodogo Centre, wakaahidi kumsaidia ambapo walimtambulisha kwa mwalimu.

“Tangu siku hiyo nikawa nasoma, mwalimu alikuwa ananipenda jinsi nilivyokuwa na bidii ya shule, nilionyesha pia nina uelewa kuzidi wangine. Rafiki yangu Bruno alifariki baada ya kugongwa na gari makutano ya barabara ya Lumumba na Uhuru,” anasema James.