Siri Aggrey Mwanri kuwa Mwinjilisti

Wednesday April 07 2021
MWANAPICCCC

Aggrey Mwanri kuwa Mwinjilisti

By Daniel Mjema

Moshi. Mkuu wa Mkoa wa zamani wa Tabora, Aggrey Mwanri amegeukia uinjilisti akihudumu katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Wilaya ya Siha.

Mwanri aliyekuwa mkuu wa mkoa huo mwaka 2016 hadi 2020, mbunge wa Siha (2000-2015) na naibu waziri wa Tamisemi alijizolea umaarufu kutokana na kauli na matendo yaliyokuwa yakiwavunja mbavu wananchi hasa alipokuwa  mkoani Tabora.

“Injinia soma hiyo, ngapi hapo,” ni kati ya kauli zilizompa umaarufu zaidi alizokuwa akizitamka wakati akikagua miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo huku akiwabana watendaji wa Serikali na makandarasi waliokuwa na utendaji wa kusuasua.

Baada ya kuachana na ukuu wa mkoa sasa mwanasiasa huyo ni mwinjilisti wa karama akihudumu katika Usharika wa Ivaeni uliopo Siha na kuanzia Aprili 4, 2021 picha zake akiwa amevaa joho akihubiri kanisani zilianza kubamba katika mitandao ya kijamii.

Anaonekana akiendesha ibada katika mtaa wa kikanisa wa Wanrimungu Jumapili ya Pasaka na katika mtaa wa Kibong’oto Jumatatu ya Pasaka, na baadaye alipiga picha mbalimbali na waumini wa mitaa hiyo.

Akizungumza na Mwananchi Digital juzi Machi 5, 2021, Mwanri amesema alitunukiwa uinjilisti alipokuwa mkuu wa Mkoa wa Tabora kazi aliyoendelea nayo hata baada ya kustaafu.

Advertisement

“Nilipokuwa mkuu wa mkoa wa Tabora. Utakumbuka kwamba nilitoa huduma katika madhehebu mbalimbali ya dini lakini kanisa langu la Kilutheri pale Dayosisi ya Magharibi kati nako nilitoa huduma. Walipofika maaskofu waliokuwa wanahudumia eneo lile la Dayosisi ya Magharibi kati, walivutiwa na namna tulivyotoa huduma zile hadi tukapata dayosisi na baba Askofu wake ni Issack Laizer yeye ndio alikuwa Askofu wetu pale,” amesema.

Katika ufafanuzi wake amesisitiza, “tulipokwenda Tabora sisi tulikuta tuko eneo la misheni na lilikuwa linahudumiwa na maaskofu watatu. Maaskofu wale walipofurahishwa na jambo lile wakapendekeza kwa Kanisa nitunukiwe nafasi ya Uinjilisti katika kanisa.

“Jambo hili aliliridhia mkuu wa Kanisa Dk Fredrick Shoo (mkuu wa KKKT  na mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini)  na alipokuja akakubali kwamba anitunuku nafasi ile na wakati ule nilikuwa mkuu wa mkoa wa Tabora. Mimi nilipoona jambo lile limeletwa kwangu niliona kama ni kitu kinachoniletea ufunuo wa aina fulani katika maisha yangu, kwa hiyo nikalikubali jambo lile kwa heshima kubwa kwa ajili ya kulinda imani.”

Kwa mujibu wa Mwanri, baada ya kumaliza utumishi wake kwa nafasi ya mkuu wa mkoa wa Tabora aliendelea  kuhubiri Injili katika Wilaya ya Siha  Jumapili na Jumatatu ya Pasaka, aliombwa na kiongozi wa usharika wake kutoa huduma.

MWANARIPICC

Kuhusu kuacha siasa ama la amesema, “nafanya kile ambacho kinanijia na Mungu anakileta ambacho ni kusudi la Mungu ninakwenda nacho. Watu wana nafasi za aina mbalimbali na maisha yanakwenda.”

“Yawe ni ya kiuchumi, ustawi wa Jamii, kilimo au kumhubiri Mungu. Tunachokitafuta hapa duniani sisi ni kutekeleza kusudi la Mungu lililotuleta basi  si kingine.”

Advertisement