Siri nzito nyuma uteuzi wa Samia

Siri nzito nyuma uteuzi wa Samia

Muktasari:

  • Panga pangua iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa makatibu wakuu na wakuu wa taasisi nyeti nchini, imeelezwa na wadau kuwa ni mwelekeo mpya unaozingatia zaidi weledi na uzoefu kazini.


Dar es Salaam. Panga pangua iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa makatibu wakuu na wakuu wa taasisi nyeti nchini, imeelezwa na wadau kuwa ni mwelekeo mpya unaozingatia zaidi weledi na uzoefu kazini.

Pangua pangua hiyo imekuja kufuatia kauli yake aliyoitoa Aprili Mosi wakati anawaapisha mawaziri na manaibu Waziri Ikulu ya Chamwio mkoani Dodoma, akisema wengine atakutana nao kwenye kiapo baada ya Pasaka yaani leo Jumanne.

Pia pangua pangua imekuja ikiwa ni wiki moja tangu Rais Samia alipopokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), ambapo alizitaka taasisi hizo kushirikiana na Gavana wa Benki Kuu (BoT), kufuatilia fedha zote zilizotoka kuanzia Januari hadi Machi, mwaka huu kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Samia alisema kuna ubadhirifu mkubwa wa mabilioni ya fedha na kumtaka Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo, haraka kuimulika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), huku mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Deusdedit Kakoko, akisimamishwa kazi kupisha uchunguzi.

Pia aliitaja Wizara ya Ofisi ya Rais, Tamisemi akisema imetawaliwa na upotevu wa fedha.

Akizungumzia uteuzi huo wa juzi, mchambuzi wa masuala ya siasa Bubelwa Kaiza alisema mabadiliko hayo yanaashiria mwelekeo mpya wa Rais Samia aliosema unajali zaidi weledi.

“Awali watu walioteuliwa kwenye wizara nyeti waliokuwa ni wale Rais aliwajua zaidi na aliowaamini, lakini Rais Samia anaangalia zaidi weledi,” alisema Bubelwa.

Juzi Aprili 4, 2021, Rais Samia alitekeleza alichokisema kwa kupangua makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu wa wizara na wakurugenzi wa taasisi nyeti za Serikali.

Katika uteuzi huo, Rais Samia amemteua Emmanuel Tutuba kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, akisaidiwa na manaibu Katibu watatu ambao ni Adolf Ndunguru, Amina Shaaban na Khatib Kazungu.

Tutuba, ambaye kabla ya hapo alikuwa Katibu Tawala wa mkoa wa Mwanza kuanzia Januari 31, 2020, amechukua nafasi iliyoachwa na Dotto James aliyehamishiwa Wizara ya Viwanda na Biashara.

Uteuzi wa Tutuba kwenye nafasi hiyo umetajwa kuzingatia zaidi weledi, huku awali hakuwa akifahamika sana kama kama ilivyo kwa wengine.

Mbali na makatibu, Rais Samia pia amemteua Alphayo Kidata kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).


Kauli za wachambuzi

Akizungumzia uteuzi huo, mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Abel Kinyondo alisema mabadiliko yalikuwa ni ya lazima kwa kuwa Rais ni mpya.

“Hakuna kitu kinachofanyika katika uendeshaji wa Serikali bila kuwa na fedha, kwa hiyo sehemu ya kwanza kuguswa lazima iwe wizara ya fedha na taasisi zake.

“Kama utakumbuka Rais Samia amesema hivi karibuni kuwa, TRA walikuwa wanatumia nguvu kukusanya kodi badala ya akili na maarifa huku Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alimtaka Waziri mpya wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba kukusanya Sh2 trilioni kwa mwezi. Kwa hiyo pale wizarani wanatafuta watu wa uhakika,” alisema Kinyondo.

Maoni hayo yaliungwa mkono na Profesa Samuel Wangwe, akisema uteuzi wa Tutuba kwenye nafasi hiyo wizarani hapo una malengo makubwa.

‘Yule mtu wa fedha ana uzoefu, alikuwa pale kwa muda mrefu, akaenda kuwa RAS, kwa hiyo ana uzoefu wa fedha na mambo ya mikoani,” alisema Profesa Wangwe.

Pia amegusia uteuzi wa Profesa Godius Kahyarara aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), akisema ni mtaalamu katika eneo hilo.

“Profesa Kahyarara ni mchumi na ana uzoefu katika uwekezaji, maana hata pale NSSF walikuwa wanafanya uwekezaji ili kuzidi kulipa uhai shirika.

“Inaonyesha wameona kwamba uzoefu wake huko nyuma hata kama aliondoka kwa namna ile, lakini wamechunguza wameona yuko safi,” alisema Profesa Wangwe aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) wakati Profesa Kahyarara akiwa mkurugenzi.

Kuhusu Kamishna Mkuu wa TRA, Profesa Wangwe alisema, licha ya kuondolewa kwake katika mamlaka hiyo awali, inaonyesha amechunguzwa na kukutwa kuwa yuko safi.

“Naona baada ya uchunguzi wameona mambo yako safi. Ninavyomfahamu ni mtu ambaye atafanya kazi vizuri.

“Mimi naona ni uteuzi mzuri, si alisema jicho lake linaona mbali, naona ni kweli. Naamini kwamba anatumia mifumo kumshauri na anashaurika,” alisema.

Kwa upande wa Wizara ya Habari, Dk Hassan Abbas amebaki kwenye nafasi hiyo huku nafasi yake ya Msemaji Mkuu wa Serikali akiteuliwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa.

Kwa upande wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ameteuliwa, Dk Jabir Kuwe anayechukua nafasi ya James Kilaba.

Akizungumzia mabadiliko hayo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari (MCT), Kajubi Mukajanga alisema uteuzi huo unaweza usiwe na matokeo makubwa kama hakutakuwa na mabadiliko ya mifumo na sheria.

“Tuna matatizo makubwa ya mfumo na sheria, kwa hiyo tunatarajia hayo mabadiliko yatakwenda sambamba na mabadiliko ya mifumo na sheria. Unajua MCT tumeshakwenda mahakamani kupinga kanuni na taratibu zinazosimamia maudhui ya mitandao, Sheria ya Huduma za Habari.

“Sisi kama wadau tuko tayari kushirikiana na Serikali, mapendekezo tumeshayapeleka mara nyingi. Tuko tayari kujadiliana na viongozi walioteuliwa kuhusu sheria hizo,” alisema Kajubi.

Akifafanua zaidi, mchambuzi wa siasa Bubelwa Kaiza alitoa mfano wa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Dk Laurian Ndumbaro akisema amedumu katika wizara hiyo kutokana na uzoefu na weledi.

“Hata kurudishwa kwa Profesa Kahyarara ni kutokana na weledi wake. Vilevile Dk Mataragio aliyekuwa ameondolewa katika Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) pia wameangalia weledi ndiyo maana amerudishwa,” alisema.

Mwingine ni Katibu Mkuu Maliasili na Utalii, Allan Kijazi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara wa Maliasili na Utalii akichukua nafasi ya Dk Aloyce Nzuki baada ya kuteuliwa na Rais Magufuli kushika nafasi hiyo Julai 17, 2020 akitakiwa kuendelea kuwa Kamishina wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi la Taifa (Tanapa).

Vilevile kuna Naibu Katibu Mkuu mteule wa Tamisemi anayeshughulika na afya, Grace Maghembe ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya nafasi aliyoipata baada ya kupandishwa kutoka kuwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Mwingine ambaye nyota yake ya kuaminiwa imezidi kutakata ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Gerson Msigwa ambaye ameteuliwa kutoka nafasi ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu.

Pia, Msigwa ndiye atakuwa Msemaji Mkuu wa Serikali jukumu ambalo awali lilikuwa kwa Dk Abbas.

Mabadiliko Tamisemi

Rais Samia alishatoa angalizo kwa aliyekuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo ambaye sasa ni Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Muungano na Mazingira) akimtaka kushughulikia upotevu wa fedha, la sivyo watatafuta njia ya kumsaidia.

Aprili Mosi baada ya kutangaza mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, Waziri Jafo alihamishiwa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), huku Waziri Ummy Mwalimu akihamishiwa Tamisemi.

Akisisitiza kuhusu ukusanyaji wa mapato, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliwasisitiza mawaziri akiwamo Ummy Mwalimu kujizatiti katika ukusanyaji wa mapato.

Katika mabadiliko ya makatibu wakuu, wizara hiyo haikusalimika, kwani aliyekuwa Katibu Mkuu, Joseph Nyamhanga ameenguliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Profesa Riziki Shemdoe aliyekuwa Viwanda na Biashara.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Paul Lusuile alisema mabadiliko katika Ofisi ya Rais (Tamisemi) yamelenga kuiboresha wizara hiyo.

“Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni kubwa sana, kwa sababu inagusa maisha ya watu moja kwa moja na inagusa sekta muhimu kama vile afya, elimu ambako wapiga kura wengi wapo.

“Mabadiliko haya ni muhimu kuwahamasisha watu kufanya kazi kwa bidii kwa kufuata sheria za utumishi na miiko. Pia yanawakumbusha watumishi kwamba utumishi siyo kazi ya kudumu, mtu yeyote anaweza kupandishwa au kushushwa,” alisema Luisuile.

Mabadiliko yalivyowagusa wananchi

Baadhi ya watu kutoka sehemu mbalimbali nchini, wamempongeza Rais Samia kwa mabadiliko aliyofanya katika nafasi ya makatibu wakuu wa wizara, manaibu katibu wakuu na wakuu wa taasisi na idara za Serikali.

Mkazi wa Temeke jijini Dar es Salaam, Abdilahi Ismail alisema kuwa Rais Samia ni mtu wa vitendo zaidi katika utendaji.

“Unajua Rais Samia wakati anaingia madarakani kama unakumbuka wakati anapokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), alitaja maeneo ya matatizo kama Tamisemi na kwenye mashirika na amefanyia kazi jambo hilo mara moja,” aliongeza Ismail.

Naye mkazi wa Bagamoyo Mkoa wa Pwani, Erasto James alieleza kuwa mabadiliko hayo yamelenga kushughulikia kero za wananchi.

“Umeona ndugu mwandishi mabadiliko yamefanyika sehemu kama Tamisemi, Wizara ya Fedha na kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF; haya ni maeneo machache yanayogusa wananchi moja kwa moja,” aliongeza Erasto.

Wakizungumzia mabadiliko hayo, wakazi wa Dodoma walilieleza Mwananchi kuwa Rais ameona mbali kutokana na ukweli kuwa wengi walijisahau na kujiona kama miungu watu.

Mmoja wa wakazi hao, Rashid Suleiman alisema mabadiliko hayo yatawafanya viongozi hao kutozoea nafasi hizo hata kama wataongoza kwa muda mrefu bila kubadilishwa.

“Namuomba Rais wetu asiwaache viongozi kwenye nafasi hizo kwa muda mrefu, awe anawabadilisha kama anavyofanya sasa, hili litasaidia mtu asifanye kazi kwa mazoea na kuwa mungu mtu,”alisema Suleiman.

Julieth Simon, alisema kasi aliyoanza nayo Rais Samia katika kuwabadilisha makatibu wakuu wa wizara na manaibu wao pamoja na taasisi nyingine, inawafanya baadhi yao kukaa mguu sawa kiutendaji.

Alisema ikiwa mtu alizembea kazini kwa sababu ya kuwa kwenye nafasi hiyo muda mrefu, ataacha tabia hiyo akihofia kutumbuliwa.

Kwa mujibu wa Julieti, kutokana na kasi hiyo ya Rais, wataendelea kumuungaa mkono katika kila hatua ya kuleta mabadiliko chanya kwa jamii na Taifa kwa ujumla