Siri ya ushindi kidato cha nne 2020

Wanafunzi wa Shule ya Feza Boys ya jijini Da es Salaam, wakishangilia baada ya matokeo ya kidato cha nne kutangazwa na shule hiyo kuwa miongoni mwa shule zilizofanyika vizuri kitaifa.

Dar es Salaam. Matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa juzi na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), yameonyesha ongezeko la ufaulu kwa wahitimu waliopata daraja la kwanza kwa alama saba.

Daraja hilo maana yake ni mtahiniwa kufaulu masomo saba kwa alama A. Daraja la kwanza lina alama saba hadi 17, huku daraja la pili likiwa na alama 18 hadi 21 na daraja la tatu likiwa na alama 22 hadi 25 na daraja la nne linaanzia alama 26 hadi 33, huku sifuri ni alama 34 hadi 35.

Uchambuzi wa Mwananchi umebaini kuwapo kwa ongezeko la watahiniwa wanaopata daraja la kwanza la alama saba, kuanzia mwaka 2016 kwa baadhi ya shule hasa zile zinazochuana katika orodha ya shule kumi bora.


Shule na ufaulu wa alama saba

Shule ya St. Francis Girls ya mkoani Mbeya ambayo ndiyo ya kwanza kitaifa ina watahiniwa 79 waliopata daraja la kwanza la alama saba kati ya wanafunzi 90.

Ufaulu wa shule hiyo umekuwa ukipanda kila mwaka, ambapo katika matokeo ya mwaka 2015, kulikuwa na wanafunzi saba tu waliopata daraja la kwanza kwa alama saba, mwaka 2016 walikuwa wahitimu sita, mwaka 2017 walikuwa wanafunzi 13, mwaka 2018 walikuwa wanafunzi 40 na mwaka 2019 walikuwa wanafunzi 53.

Shule ya sekondari ya Ilboru ya mkoani Arusha iliyoshika nafasi ya pili kitaifa, ina wanafunzi 53 waliopata daraja la kwanza kwa alama hizo. Mwaka 2015 shule hiyo ilikuwa na wanafunzi watatu wenye daraja hilo mwaka 2016 alikuwapo mwanafunzi mmoja, 2017 walikuwapo watatu, mwaka 2018 walikuwa wanane na mwaka 2019 walikuwe wanafunzi 11.

Shule ya sekondari ya Canossa ya jijini Dar es Salaam ina wanafunzi 42 wenye daraja hilo 2020. Shule hiyo pia imekuwa ikipanda ambapo kwa miaka ya 2015 na 2016 ilikuwa na wanafunzi wenye daraja hilo watano kila mwaka.

Mwaka 2017 walishuka na kufikia wanafunzi wawili na mwaka 2018 walifika watatu na mwaka 2019 walipanda na kufikia 13,

Shule ya sekondari ya ya wavulana ya Feza ya jijini Dar es Salaam ambayo pia mwaka huu imeingia 10 bora, imepata wanafunzi 24 wenye daraja hilo ikiwa imepanda kutoka mwanafunzi mmoja mwaka 2015, wanafunzi 10 mwaka 2016, wanafunzi watano mwaka 2017, wanne mwaka 2018 na 14 mwaka 2019.

Nyingine ni Marian Boys ya Pwani ambayo mwaka 2020 ina wanafunzi 28 wenye daraja hilo, wakiongezeka kutoka 20 mwaka 2019. Mwaka 2015 walikuwa wanafunzi watano sawa na mwaka 2016 kisha wanne mwaka 2017 na kisha 19 mwaka 2018.


Wazungumzia sababu ya ufaulu huo

Akizungumzia ongezeko hilo la ufaulu, Katibu mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde licha ya kupongeza shule zilizofanya vizuri, alisema lengo ni kufikisha ufaulu wa asilimia 50.

“Ongezeko la ufaulu unatokana na juhudi za shule za Serikali na za binafsi. Kwa mfano ukiangalia shule ya sekondari ya Ilboru, imetoka huko ilikokuwa imekuwa ya pili,” alisema Dk Msonde alipokuwa akizungumza na Mwananchi jana kwa simu.

Alitaja miongoni mwa jitihada hizo kuwa ni ukarabati wa miundombinu na kuongeza vifaa vya kufundishia.

“Kwa hiyo shule nyingi zimefanya jitihada kubwa na zimejivuta kwenda juu zaidi. Ndiyo maana shule za Serikali zilizokarabatiwa, zimeanza kupanda juu na hilo ndilo ongezeko la asilimia tatu.

“Kilichopo hapa, tuwapongeze sana walimu, wamefanya kazi kubwa sana.

Kuhusu utungaji wa mitihani, Dk Msonde alisema tangu mwaka 2018, Necta imebadilisha mfumo wa mitihani ya shule za msingi kuanzia darasa la nne na la saba na sekondari kidato cha pili, cha nne na sita pamoja na mitihani ya vyuo vya elimu ngazi za cheti na stashahada.

“Tumeondoa maswali ya kukaririshwa, badala yake maswali yanayoulizwa ni ya kupima ujuzi. Mtoto haulizwi tena habari ya kwamba nini maana ya kitu fulani, hicho anaweza akaeleza. Haulizwi tena taja faida za kitu fulani, anaweza kutaja hata kama hakijui.

“Sasa tunauliza maswali ya kumpa mtoto changamoto ya kwa nini jambo hili linatokea? Je, ili ufikie hapa ufanyeje? hayo ndiyo maswali yetu. Ukiangalia mitihani yetu, mtu aliyekaririshwa hawezi kuijibu, kwa sababu unapima umahiri wake,” alisema Dk Msonde. .

Kauli hiyo imeungwa mkono na Ibrahim Yunus, ambaye ni mkurugenzi wa shule za Feza akisema mtalaa wa ujuzi ndiyo umewawezesha wanafunzi wao kufanya vizuri zaidi.

“Kwa sasa kuna mtalaa tunaoutumia unaoitwa ‘Competence based’, yaani watoto wasiishie kukariri, bali waelewe muktadha. Kwanza inabidi walimu wafundishwe jinsi ya kuelewa malengo yanayotakiwa... ‘‘ alisema.