Somo la historia ya Tanzania kuanza kufundishwa Machi 2021

Tuesday February 23 2021
Historia pic
By Fortune Francis

Dar es Salaam. Somo la historia ya Tanzania litaanza kufundishwa katika shule za msingi kuanzia Machi, 2021 baada ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kukamilisha uandishi wa rasimu na mihtasari.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa  agizo la Rais John Magufuli alilolitoa wakati akiwaapisha mawaziri Desemba 9, 2020 Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

Katika hafla hiyo Magufuli alimtaka Waziri wa Elimu nchini, Profesa Joyce Ndalichako kuanzisha somo la historia ya Tanzania na liwe la lazima kusoma.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumanne Februari 23, 2021 mwenyekiti wa bodi ya TET, Profesa Bernadeta Killian amesema baada ya kukamilisha uandaaji wa rasimu za mihtasari, shughuli inayoendelea ni kukamilisha kazi ya uandishi wa vitabu inayotarajiwa kumalizika Machi.

“Kutokana na mkakati tuliouandaa, shule za awali hadi darasa la saba masomo yataanza mwezi wa tatu na sekondari wataanza Mei. Vitabu vinaendelea kuandaliwa kwa uharaka na makini.”

“Katika utaratibu mzima wa uandishi wa muhtasari na vitabu TET hufuata hatua mbalimbali, moja ni kuwashirikisha wadau wa elimu, hivyo tumeandaa mkutano wa wadau. Baadhi yao ni taasisi za elimu ya juu, vyuo vya ualimu, asasi zisizo za kiserikali, wizara, mashirika mbalimbali na watekelezaji wa mwisho wa mtaala ambao ni walimu,” amesema.

Advertisement

Profesa Killian amesema wadau wengine ni taasisi za dini na viongozi wa kijadi wakiwemo machifu na mangi kutoka mikoa mbalimbali Tanzania Bara na wataalamu wa historia kutoka Zanzibar  na chama cha historia Tanzania.

Advertisement