Somo la uraia chanzo kupungua uzalendo kwa vijana

Muktasari:

Utafiti waonyesha ufundishaji wa kina wa somo la uraia katika shule za sekondari unahitajika kujenga ari ya uzalendo na ushiriki wa vijana katika mchakato wa demokrasia

Dar es Salaam. Wakati dhana ya uzalendo ikionekana kupungua nchini Tanzania hususani kwa vijana, kukosekana kwa elimu ya kina ya uraia kwa kundi hilo kumetajwa kuchangia hali hiyo.

 Hayo yamebainika leo Alhamisi, Septemba 22, 2022 katika utafiti uliofanywa na Shirika la Hakielimu uliolenga kuangalia mchango wa elimu ya uraia katika shule za sekondari na ushiriki wa vijana katika kujifunza na kuiishi demokrasia.

Katika utafiti huo imebainika mfumo mzima wa ufundishaji wa somo la uraia hauwapi nafasi wanafunzi kuishi katika misingi ya kidemokrasia na uzalendo.

Akiwasilisha ripoti ya utafiti huo, mtafiti Dk Perpetua Kalimasi amesema wamebaini wapo walimu wanaofundisha somo la uraia wakiwa hawana uelewa wa kutosha wa somo hilo hivyo wanashindwa kufundisha kwa undani.

Pamoja na hilo, Dk Perpetua amesema muda uliotengwa kwa ajili ya kufundisha somo la uraia ni mchache ikilinganishwa na masomo mengine hali inayosababisha ufundishaji usiwe mpana.

“Wahojiwa wameeleza mambo mbalimbali yanayosababisha somo hili lisiingie ndani ya vijana wengi wa kitanzania, changamoto zipo kuanzia kwa walimu, si wote wanaofundisha uraia wamebobea.

“Walimu na wanafunzi wamesema ipo haja ya somo hili kufundishwa na walimu waliobobea kama somo lao la kufundisha, yani kuanzia vyuoni walimu waandaliwe,” amesema na kuongeza:

“Pia muda wa kufundisha somo hili uongezwe kama masomo mengine sio kama sasa baadhi ya shule inafundishwa mara   moja kwa wiki.”

Akizungumzia katika hafla ya uzinduzi wa ripoti hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Hakielimu, Godfrey Boniventure amesema utafiti huo umelenga kuongeza ushiriki wa vijana katika shughuli za kidemokrasia.

“Ushiriki wa vijana katika shughuli za kidemokrasia ni mdogo, zipo changamoto zinazosababisha hali hii, imeonekana kuanzia shuleni kule kuna shida, ufundishaji ni mdogo na hata zile shughuli ambazo zinafanyika ushirikishaji wao ni mdogo,” amesema Boniventure.