Songwe kupiga msako wanafunzi wasioripoti shuleni

Baadhi ya Madiwani Halmshauri ya Wilaya ya Songwe wakiwa kwenye kikao cha baraza la hilo. Picha na Mary Mwaisenye

Muktasari:

  • Madiwani wa Halmshauri ya Wilaya Wilaya ya Songwe wameazimia kufanya msako wa muda wa wiki moja nyumba kwa nyumba ili kuwarejesha wanafunzi watoro zaidi ya 1000.

Songwe. Baraza la Madiwani la Halmshauri ya Wilaya ya Songwe Mkoa wa Songwe, limeazimia kuwarejesha shuleni wanafunzi watoro zaidi 1000 wa shule za msingi za halmshauri hiyo ambao hawapo shuleni tangu shule zingunguliwe January 9 2023.

Madiwani wameelezea hayo January 20 2023 katika kikao cha kawaida cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2022/2023 wakati wakijadili taarifa mbalimbali za kamati za maendeleo.

Wamesema wamejipanga kuhakikisha wanatembea nyumba kwa nyumba kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji na kata ili wanafunzi hao waendelee na masomo.

Akizungumzia hilo kwa niaba ya madiwani, Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Songwe, Abraham Sambila ametaja baadhi ya sababu zinazosababisha wanafunzi kuwa watoro shuleni.

Amesema kutokuwepo kwa chakula cha mchana kwa baadhi ya shule inaweza kuwa sababu ya wanafunzi kuwa watoro na kukimbilia shughuli zinazozunguka maeneo yao ambazo ni uvuvi, uchimbaji wa madini na ufungaji.

Akizungumzia upande wa shule za sekondari, Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Songwe alisema kwa shule za sekondari pia kumekuwa na changamoto ya wanafunzi wa kidato cha kwanza kutoripoti shule walizopangiwa ambapo asilimia 24.2% ya waliopangiwa kidato cha kwanza bado hawajaripoti ambapo mpaka January 20, 2023 ni asilimia 75.8% pekee ndio wameripoti shuleni.

Diwani wa kata ya Mbuyuni, Kassimu Omboka akizungumzia suala hilo alisema pamoja na wao kuwasaka wanafunzi hao pia wamejipanga kuhamasisha wazazi kujitolea chakula kwenye shule ili kuleta chachu ya wanafunzi kuhudhuria shuleni na kupunguza utoro.

Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Songwe, Simon Simalenga alisisitiza Madiwani kuhakikisha wanashirikiana na viongozi wa kata na vijiji katika maeneo yao ili kuhakikisha wanafunzi hao wanarudi shuleni mara moja.

"Naomba madiwani kwenye suala la elimu tusiingize siasa kwani watoto hao ni taifa la kesho tukiwaandalia mazingira mabaya leo tutakuwa  tunatengeneza taifa ambapo baadaye hatutapata wawakilishi walio Bora," alisema Simalenga.