Spika Ndugai aendelea kutetea tozo miamala ya simu

Muktasari:

Spika Ndugai amewataka wanaopinga tozo miamala ya simu waje na mkakati mwingine wa Serikali kupata fedha za maendeleo.

Dodoma. Wakati Serikali ikiunda kamati ya kupitia tozo za miamala ya simu zinazolalamikiwa na wananchi, Spika wa Bunge Job Ndugai ameibuka hadharani kusema lazima tozo hiyo iwepo ili kufikia malengo ya nchi.

Kamati hiyo imeundwa kufuatia kikao cha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile na wataalamu wa Serikali kujadili tozo hizo na kupewa wiki moja kuleta mapendekezo. 

Tozo hizo zilizowekwa katika bajeti ya Serikali iliyopitishwa na Bunge mwishoni mwa Juni, ilianza kutumika rasmi Julai 15 na kuzua malalamiko ya wananchi, ambapo Julai 20 Rais Samia Suluhu Hassan aliwaagiza mawaziri husika kufanyia kazi malalamiko hayo.

Lakini akizungumza leo Julai 23, kwenye mkutano wa mpango wa maendeleo wa mkoa wa Dodoma ulioitishwa chini ya Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, Spika Ndugai amesema, Serikali imeazimia kufikia malengo makubwa ya maendeleo, hiyo itasaidia kuinua uchumi.

Huku akihoji wanaopinga suala hilo, Ndugai amewataka kutoa njia mbadala za Serikali kupata fedha za miradi yake.

"Haya ni malengo makubwa sasa unadhani tutayafikiaje? Ndio maana sisi wabunge tukaamua tuweke tozo kwenye miamala.

“Ukinuna sawa, ukifanyaje sawa tunakwenda kwenye miamala na tutatoza kitu fulani ambacho kitakwenda kwenye mfumo ambao utawanufaisha wananchi wenyewe kupitia afya, maji, umeme, ujenzi wa madaraja na barabara,” alisema Ndugai.


Ameendelea kusisitiza kuwa walipitisha na kutunga sheria wenyewe hivyo hakuna namna kwenye hilo.

“Anayepinga asipinge kwa mdomo bali aonyeshe njia wapi wanakwenda kupata fedha za maendeleo hayo.

wewe unaepinga tupe mbadala tutawezaje kuyafanya hayo.”

Amesema wazo kama hilo liliazimiwa miaka 10 iliyopita kwenye sekta ya umeme ambapo iliwekwa tozo inayokwenda Wakala wa kusambaza Umeme Vijijini (REA) na sasa kufikia mwaka 2025 nchini Tanzania pasiwepo kijiji ambako hakitakuwa na umeme.

Pia aliwataka wananchi kushirikiana na viongozi kwenye swala la maendeleo kwani swala hilo linaletwa na juhudi za Serikali na wananchi  kushirikiana kwa pamoja badala kuisubiri Serikali pekee.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amesema katika kuchochea maendeleo ataandaa kikao maalumu kuhusu sekta ya elimu, kufuatia hali mbaya ya elimu mkoani humo.

Naye Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini, Anthony Mavunde amesema katika suala la maendeleo mkoa unahitaji miundombinu rafiki ikiwemo huduma muhimu kama Barabara ili kuwavutia wawekezaji na kuleta tija katika mkoa huo ambao unabeba sura ya nchi.