Spika Ndugai amtaja Mbowe akidai ripoti ya CAG inapotoshwa

Spika Ndugai amtaja Mbowe akidai ripoti ya CAG inapotoshwa

Muktasari:

  • Spika wa Bunge nchini Tanzania Job Ndugai amesema uchambuzi wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkuguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) utawasilishwa bungeni katika mkutano wa nne badala ya mkutano wa tano.

Dodoma. Spika wa Bunge Job Ndugai amezitaka kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zichambue ripoti ya Mdhibiti na Mkuguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuiwakilisha bungeni katika mkutano wa nne badala ya mkutano wa tano, kwa kuwa inapotoshwa.


Akizungumza leo Jumatatu Aprili 12 2021, Ndugai huku akimtaja Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amedai kuwepo upotoshaji wa ripoti hiyo.


Kauli ya Spika imekuja siku moja baada ya Mbowe kuhutubia kupitia mitandao ya jamii, ambapo pamoja na mambo mengine alilituhumu Bunge kwa vitendo vya rushwa.


 “Watu wanabeba tu mabilioni yameibiwa sasa huyo rafiki yangu Freeman Mbowe alikuwa Ulaya huko sasa katumwa na watu wake huko anapotosha mambo,” amesema.


Amesema sio watu wengi wenye uelewa wa kuchambua taarifa za kihasibu na hivyo kunaweza kukawa na ujenzi wa kituo cha afya wa Sh 500milioni lakini Sh 499milioni  zimetumika vizuri kabisa.


Hata hivyo, amesema lakini kati ya fedha hizo Sh1milioni ikikosa kiambatanisho fulani ni kawaida wakaguzi wanahoji fungu zima la Sh 500milioni.


Amesema kwa hiyo unaposoma mtaani unaona sh 500 zimeibwa lakini kumbe pale ni Sh milioni moja ndio hazina risiti.


Amesema kamati hizo zitaanza mapema kuchambua ripoti hizo ili waangalie ratiba yao na kuwaelimisha watu kuhusiana na ripoti ya CAG ambayo ni taarifa nzuri lakini baadhi ya watu wanabeba na kupotosha tu.