Stendi mpya ya Mbezi itakavyofungua fursa lukuki za kiuchumi
Muktasari:
- Wakati stendi ya kisasa ya mabasi ya mikoani iliyopo Mbezi Luis, jijini Dar es Salaam yenye thamani ya Sh50.9 bilioni ikitarajiwa kuanza kazi leo, uwepo wake unatazamiwa kuchochea fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi wa eneo hilo na wageni.
Dar es Salaam. Wakati stendi ya kisasa ya mabasi ya mikoani iliyopo Mbezi Luis, jijini Dar es Salaam yenye thamani ya Sh50.9 bilioni ikitarajiwa kuanza kazi leo, uwepo wake unatazamiwa kuchochea fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi wa eneo hilo na wageni.
Miongoni mwa fursa hizo ni pamoja baadhi ya watu kujenga nyumba za kulala wageni karibu na kituo hicho, huku wengine wakiziboresha hoteli zao ili kuvutia wateja pindi stendi hiyo itakapoanza kufanya kazi.
Pia, stendi hiyo iliyojengwa na kampuni ya Hainan ya China, imechangia ongezeko la watu kuhamia Mbezi kwa ajili ya shughuli mbalimbali, ikiwamo ujasiriamali.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge anasema ujenzi wa stendi ulioanza Februari 2019 umeshakamilika na Alhamisi ya wiki hii kitaanza kufanya kazi, huku akiwataka wamiliki wa mabasi kujiandaa na mchakato huo.
Hata hivyo, mjumbe wa kamati ya utendaji ya Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustafa Mwalongo alisema wapo tayari na hawana sababu yoyote ya kutoondoka stendi ya Ubungo.
“Tupo tayari kuhamia Mbezi, hatuna tatizo kwa sababu Ubungo kwa sasa ni eneo finyu na hatufanyi shughuli zetu kwa ufanisi,” alisema na kuongeza: “Changamoto zetu tulizokuwa tukilalamika ni barabara ya kuingilia, ofisi za tiketi na eneo la maegesho ya magari kwa ajili ya usiku ambalo lipo katika stendi mpya,” alisema.
Katika maelezo yake, Kunenge alisema kuanza kutumika kwa kituo hicho kutahitimisha shughuli katika stendi ya zamani ya Ubungo ambayo hivi sasa imekuwa finyu baada ya ujenzi wa mradi wa mabasi ya mwendokasi kuanza eneo hilo.
Mbali na hilo, Kunenge alisema uwepo wa stendi hiyo ya kimataifa utatoa fursa na kuboresha maisha ya wananchi, huku akisisitiza huduma zote zitapatikana.
Stendi ya Mbezi ikianza kufanya kazi huduma mbalimbali zitakuwa zikipatikana, zikiwamo huduma za pamoja (one stop center), taasisi za Serikali za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Uhamiaji na Polisi.
Katika stendi hiyo kutakuwa na shughuli za biashara, zahanati, fremu za maduka makubwa yatakayouza nguo na viatu, migahawa, eneo la kuegeshea magari binafsi. Pia kutapatikana huduma za taxi kama vile Uber na Bolt.
Pembezoni mwa stendi hiyo yenye sehemu ya juu na chini kumejengwa eneo maalumu kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo, maarufu kama machinga, pia watakuwapo akina mama na baba lishe.
Pia madereva wa bajaji na pikipiki watakuwa na eneo lao maalumu kwa ajili ya kufanya shughuli zao.
Wakati stendi ikitarajiwa kuanza kazi kesho, baadhi ya wamiliki wa hoteli na nyumba za kulala wageni zilizopo karibu ya kituo hicho kilichopo Mtaa wa Mshikamano, walisema wanasubiri kwa hamu kituo hicho kianze kutoa huduma ili kunufaika na wateja.
“Natamani hata kesho ianze kufanya kazi kwa sababu nimejiandaa kupokea wageni. Nimefanya maboresho mbalimbali, ikiwamo kupaka rangi, kufanya matengenezo ya vyumba sambamba na kununua vitanda vipya,” alisema Elizabeth Iteba, ambaye ni meneja wa hoteli ya FM iliyopo mita 200 kutoka ilipo stendi hiyo.
Elizabeth alisema huduma zote muhimu zimeandaliwa katika hoteli hiyo kutokana na maboresho yaliyofanyika.
“Kila mtu anayeishi maeneo haya ana shauku ya kujua stendi itaanza lini? Bodaboda wameshaanza kuchukua namba zetu kwa ajili ya abiria na wao wametueleza kuwa watakuwa tayari kuleta wateja. Hapa kila mmoja anamtegemea mwenzake,” alisema Elizabeth.
Mmoja wa madereva bodaboda wa Mbezi, Hamis Hamis alisema kumekuwa na kasi kubwa ya watu kuboresha na kujenga nyumba za kulala wageni zinazotarajiwa kukamilika kabla ya kufunguliwa kwa stendi hiyo.
“Siyo upande wa stendi tu, bali hata huku ng’ambo (kituo cha daladala cha Mbezi) kama unakwenda Kinyerezi watu wanafanya ukarabati wa nyumba zao ili kukidhi mahitaji ya wageni,” alisema Hamis.
Mkazi wa eneo hilo, Elisha John alisema ana fremu tatu za biashara mbalimbali ambazo zimeshapata wapangaji wanaosubiri stendi hiyo ianze kufanya kazi ili na wao watoe huduma.
“Baadhi yao wanataka kufanya biashara ya kutoa huduma za fedha kwa njia ya mtandao kwa sababu wana imani mzunguko wa watu utakuwa mkubwa.
Bado hawajafungua ila wameshalipia kodi zao,” alisema John.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mshikamano, Awadh Simba alisema kuna ongezeko kubwa la wageni katika mtaa wao ambao walikwenda baada ya Rais John Magufuli kutoa maelekezo kuhusu ukomo wa ujenzi wa stendi hiyo mwaka jana.
Simba alisema kuna nyumba za kulala wageni zimeshaboreshwa kwa ajili ya stendi hiyo, huku wawekezaji wengine wakijenga hoteli za kisasa za ghorofa katika mtaa huo.
Mbali na hilo, Simba alisema kwa tamko la Kunenge wakati wowote wafanyabiashara waliopanga kwenye fremu zilizopo katika mtaa huo wataanza mchakato wa kuzifungua ili kuanza kutoa huduma.
“Walikuwa wanasikilizia lini stendi itafunguliwa, lakini kwa tamko la jana wakati wowote watakuja kufungua fremu zao na kuanza kazi.
Walikuwa hawana uhakika stendi itaanza kufanya kazi lini,” alisema Simba.
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk Anna Makakala alipotembelea stendi hiyo, alisema taasisi yake ipo tayari kutoa huduma pindi kituo hicho kitakapofunguliwa, akisema miundombinu yote imekamilika, kilichobaki ni kuingiza samani.
Dk Makakala alisema miongoni mwa huduma zitakazotolewa na uhamiaji ni pamoja na vibali vya muda vya kusafiria kwenda nchi za jirani ili kurahisisha huduma hiyo kwa Watanzania.
“Kabla ya hapo mtu anayetaka kibali cha muda cha kusafiria kwenda nchi jirani alitakiwa kwenda ofisi ya uhamiaji ya mkoa au wilaya kwa ajili ya kupata kibali cha dharura. Ofisi yetu hapa itakuwa karibu na Jeshi la Polisi,” alisema Dk Makakala.
Wakati huohuo, Mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana alisema mchakato wa ugawaji wa vizimba katika stendi hiyo umeshafanyika na leo wataanza shughuli zao.
Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Magari Tanzania, Ibrahim Samwix alisema kwenye stendi hiyo mpya kutakuwa na eneo maalumu la ukaguzi wa mabasi.