Sugu: Dhamira ya Rais Samia inaturudisha nyuma

Monday May 03 2021
sugu pc
By Fidelis Butahe

Mbeya. Mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chadema, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu amesema dhamira ya Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan imewafanya watu wa kada mbalimbali kuweka pembeni nyakati ngumu walizopitia kwa takribani miaka minne na kuwa na imani kuwa, sasa mambo yatakuwa mazuri na furaha kurejea.

Sugu, aliyekuwa mbunge kuanzia mwaka 2010 hadi 2020 alieleza hayo katika mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita mkoani Mbeya.

Huku akitolea mfano uamuzi wa kusitisha kuhamishia biashara zake nchi jirani, Sugu alisema Rais Samia ni sawa na mtu aliyenyanyua tawi la mti wa mzaituni na walionaye karibu nao wanatakiwa pia kunyanyua tawi hilo, si kunyanyua bunduki ya kivita aina ya AK 47.

“Samia anacheza kete za siasa za Kiafrika, lakini sisi tunaangalia dhamira yake, ameonyesha nia ya kubadilisha hali iwe tofauti na kule tulipokuwa.

“Sisi kama Watanzania lazima tumuunge mkono na hii haina maana ya kujipendekeza, tunafanya hivi kwa ajili ya mustakabali wa nchi yetu, kama kasema mema na sisi lazima tuyaishi. Haiwezekani mtu amenyanyua tawi la mzaituni wewe unanyanyua AK47, hapana, unatakiwa na wewe unyanyue tawi la mzaituni,” alisema Sugu.

Sugu, ambaye pia ni msanii wa muziki wa hip hop, alipitia masahibu kadhaa, ikiwa ni pamoja na kufungwa jela na hoteli yake kunusurika kuvunjwa kati ya mwaka 2015 hadi 2019, alisema nchi ilipitia kipindi cha mpito ikiwa ni pamoja na biashara kudorora, akitaja sababu mbalimbali alizoeleza kuwa sasa zimewekwa sawa na ndio maana ameghairi kuhamishia shughuli zake nje ya Tanzania.

Advertisement

“Kwenye uongozi wa nchi kuna sauti ya kiongozi mkuu wa nchi, tangu Samia ameingia kitu cha kwanza alichokuja nacho amefanya mabadiliko ya mtazamo, ni kitu cha msingi sana, hasa ukizingatia kama mlikuwa katika nyakati ngumu za utawala.

“Hatukuwa na demokrasia kwa kweli, watu hawawezi kuongea lakini ghafla inakuja sauti inasema nikosoeni, tena kutoka enzi za ukikosoa wewe ni msaliti, si mzalendo na huitakii mema nchi,” alisema Sugu, ambaye jana Jumamosi alikuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa.

Alisema wakati watu wakianza kufunguka kwa kueleza yanayowakabili na upungufu wa masuala mbalimbali, Rais Samia alieleza ukweli kuhusu yanayowakumba wafanyabiashara na kutaka yawekwe sawa. Aprili 6, mwaka huu wakati akiwaapisha makatibu wakuu na manaibu wao, Samia aliitaka Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kuangalia namna bora ya kuwarudisha wafanyabiashara waliofunga biashara zao kutokana na mabavu yaliyotumika kwenye ukusanyaji kodi.

Alisema ukusanyaji wa kodi kwa kutumia nguvu na mabavu hausaidii na umesababisha wafanyabiashara wengi kufunga biashara zao kwa kuhofia kubambikiwa kesi na wengine kutimkia nje ya nchi.

“Hata kama kuna mambo kadhaa ambayo nayaona hayakuwa sawa, lakini naona kuna vitu vinne havikuwa sawa na anakuja rais anavitaja viwili, hilo ni lengo jema. Nataka kuamini kwamba kwa sababu hili lilikuwa ni tatizo la wafanyabiashara na kuathiri uchumi na ajira, ilikuwa na uzito uleule kama tatizo la kisiasa na demokrasia na mikutano.

“Sasa kama amefungua njia hapa nikaamini lazima na kwingine kutafunguka. Tumepata taarifa kuwa ametuandikia barua ya kuonana na sisi (Chadema), hayo ni mabadiliko, lazima tukubaliane na hilo, kwanza kuhusu utekelezaji hilo ni suala jingine. Nimesitisha kuondoka nchini kwa sababu aliyeingia amebadili mwelekeo,” alisema Sugu.

Alipoulizwa ana uhakika gani na yanayofanyika alisisitiza: “Mama (Samia) alisema leo na rafiki zangu wakaniambia akaunti zao zimefunguliwa, suala la akaunti zao kutokuwa na hela au vipi hilo ni suala jingine..., haiwezekani kila kitu kikakaa sawa kwa siku moja. Wapo wanaosema tunaridhika haraka, lakini ukweli ni kwamba hali ilivyo sasa Taifa limepata nafuu.”

Akizungumzia mazingira aliyopitia kwenye biashara, mbunge huyo wa zamani alisema: “Mfumo mzima wa ufanyaji biashara uliharibika, unajua biashara zinaanguka, wanasema ukiona mwenzako ananyolewa tia maji, sasa mimi siwezi kusema kama nina wageni wawili au watatu inatosha, lakini unaangalia hoteli kongwe zinaanguka huwezi kufurahia hayo mazingira kwa sababu unajua hali ikiendelea hadi wewe utafikiwa. Kuna muda niliwaza kubadili hoteli iwe hosteli au vinginevyo.”

Alisema ilifikia wakati maofisa wa TRA wanadai kodi kama polisi.

“Unaweza kukaa TRA wakaja mara nane na nikawauliza kuna shida wanasema hawana shida, ila nikiachana nao wanamfuata meneja (wa hoteli yake ya mjini Mbeya) na kumuuliza ‘Sugu amepata wapi fedha za kujenga hoteli’, sasa meneja nimemuajiri baada ya hoteli kukamilika why aulizwe meneja?

“TRA wamekuwa tume ya maadili au Takukuru, vyombo vya Serikali vilikuwa vinafanya kazi hadi ambazo si majukumu yao, kulikuwa na mazingira ya vurugu na baadhi ya rafiki zangu wamekwenda Zambia na Malawi. Watu ninaowafahamu wamehama, wapo waliokuwa na biashara Tunduma walihamishia Zambia kwa sababu huku kuna mambo ya ujanja ujanja, kuviziana,” alisema.

Sugu alibainisha kuwa wapo wanaodhani kuwa wakieleza ukweli wanataka kuponda utawala uliopita, jambo ambalo si kweli.

“Hata Samia alipoingia madarakani alisema wazi kuhusu mapungufu mbalimbali, sasa atasemaje vitu wakati havipo. Samia siku ya kwanza alisema tusahau yaliyopita tugange yajayo,” alisisitiza Sugu.

Akieleza zaidi kuhusu kuathirika kwa biashara zake, Sugu alisema: “Rais (Hayati John Magufuli) alisema hoteli ya Sugu isivunjwe, sasa nani alitaka ivunjwe, ile hoteli haikuota kama uyoga, ina mikopo ya benki..., benki haiwezi kukupa mkopo kwa hati za mashaka.

“Tujiulize huyo aliyetaka kuvunja hoteli yangu alichukuliwa hatua gani kwa sababu alitaka kuvunja kinyume na utaratibu.”

Aliongeza kuwa vitu vingi vinavyozungumzwa na Rais Samia kwa sasa vinawaacha wengi katika mshangao na wanatamani iwe tofauti na wanayoyasikia.

“Nawasikitikia wabunge wapo kwenye mshangao, hawaamini kinachotokea, mama wakati anahutubia bungeni na kusema atakutana na wapinzani makofi yalikuwa machache kwa sababu wale ni wanufaika kwa yaliyotokea, mama aliwaambia ongeeni ya kujenga nchi maana anajua,” alisisitiza Sugu.

Akieleza nini kifanyike kuhakikisha uchumi wa nchi hauporomoki, Sugu alisema: “Mama amesema hataki kuvuruga biashara za watu, marufuku kufunga biashara za watu. Mama amesema anasimamia sekta binafsi ambayo ndio msingi wa ajira dunia nzima. Biashara ndogo na za kati zinaajiri watu kati ya watatu hadi 100, sasa hizi biashara ukiziondolea kodi za tozo nyingi unatengeneza uhuru wa kufanya biashara.”

Advertisement