Sumaye: Viongozi hawataki kukosolewa
Muktasari:
- Sumaye alisema hayo juzi jijini hapa, wakati wa mahafali ya pili na kongamano la Shirikisho la Wanafunzi wa Elimu ya Juu ambao ni Wafuasi wa Chadema (Chaso) kutoka vyuo vikuu vilivyopo mkoani hapa chini ya Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha).
Mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema, Frederick Sumaye amesema nchi inaendeshwa kishabiki badala ya uhalisia na viongozi waliopo madarakani hawataki kukoselewa wala kuambiwa ukweli hata kwenye mambo ya msingi jambo linalohatarisha mustakabali wa maendeleo.
Sumaye alisema hayo juzi jijini hapa, wakati wa mahafali ya pili na kongamano la Shirikisho la Wanafunzi wa Elimu ya Juu ambao ni Wafuasi wa Chadema (Chaso) kutoka vyuo vikuu vilivyopo mkoani hapa chini ya Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha).
Alisema kutokana na nchi kuendeshwa kishabiki, katu Tanzania haiwezi kufika popote kwa kuwa watawala hawako tayari kuona wanakosolewa.
“Juzi juzi tu bajeti imesomwa, tungelitegemea vijana wa vyuo vikuu wanaitisha makongamano kujadili na kuchambua kwa masilahi mapana ya Taifa na kutoa maoni yanayohitaji kurekebishwa,” alisema na kuongeza:
“Lakini wakuu wetu hawataki kufanya hivyo kwa sababu wanaona maeneo yenye makosa yatatoka kwa wananchi na hii yote ni kutokana na kwamba nchi tumeingiza kwenye ushabiki, kwa hiyo hatutaki tena kufikiri au haturuhusiwi kufikiria.”
Sumaye ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu alisema kongamano sio upinzani hata kidogo, bali ni eneo ambalo wanataaluma wa kada tofauti wanatoa mitazamo na dira ya maendeleo kwa utaalamu.
“Hivyo ukiona mtu anasema hili halijakaa vizuri na inapaswa likae hivi usione huyo ni mpinzani anataka kuisaidia dola,” alisema.
Akizungumzia mkakati wa Chadema kushika dola mwaka 2020, Sumaye alisema kwa kutumia Katiba na Tume ya Uchaguzi iliyopo sasa zitafanikisha chama chake kuingia madarakani kwa kuwa wameshajua njia watakazopitia. Sumaye alisema sababu ya upinzani kuminywa kila kona inatokana na nguvu iliyopo na kuona chama tawala kinazidiwa, lakini Watanzania wameshajua kwamba ukombozi pekee uliopo kwao ni Chadema kuingia madarakani.
Katibu Mkuu wa Chaso, Julius Mwita alisema kufanya maandamano kwa kuingia barabarani kupambana na dola kutumia nguvu vimepitwa na wakati na badala yake aliwataka vijana kutumia akili na kufanya mabadiliko ya kimfumo katika kudai haki zao kwa kutumia mbinu za kisayansi.