Taasisi 200 zathibitisha kushiriki Mara Expo

Friday August 05 2022
By Beldina Nyakeke

Musoma. Asilimia 50 ya Taasisi na kampuni zilizoalikwa tayari zimethibitisha kushiriki maonyesho ya Kimataifa ya Biashara mkoa wa Mara (Mara International Business Expo) yanayotarajiwa fanyika kuanzia Septemba 11.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma, Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoa wa Mara, Boniface Ndengo amesema hadi sasa, kamati ya maandalizi imepokea uthibitisho kutoka kampuni na taasisi 200 kati ya 400 zilizoalikwa kushiriki maonyesho hayo ya siku 10.

Ametaja Wizara ya Madini, Wizara ya maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Kilimo kuwa miongoni mwa washiriki waliothibitisha ushiriki wao.

"Tunatarajia kupokea uthibitisho kutoka wizara na taasisi nyingi za Serikali za kisekta," amesema Ndengo

Amesema TCCIA inaendelea kuwasiliana na Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha wizara na taasisi nyingi za Serikali zinashiriki maonyesho hayo yanayoshirikisha taasisi, mashirika ya umma na kampuni binafsi kutoka ndani na nje ya nchi ili kufungua fursa za kibiashara na kiuchumi za mikoa ya Kanda ya Ziwa na Taifa kwa ujumla..

"Pamoja na kukuza biashara, maonyeso haya pia yanatumika kuvuta mitaji na uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi," anasema

Advertisement

Yohana Mwikwabe, mjasiriamali mjini Musoma ameipongeza TCCIA kwa kuandaa maonyesho hayo na kuomba Serikali kuyaunga mkono kuongeza fursa za kiuchumi kwa wafanyabiashara wadogo, kati na wakubwa.

"Kupitia maonyesho haya, tunaamini tutakuwa biashara zetu kwa kuuza bidhaa na huduma kwa wageni; hii ni fursa muhimu inayostahili kuungwa mkono na kutumiwa na kila mwana Mara na mikoa ya jirani," amesema Mwikwabe

Kauli hiyo imeungwa mkono na Megabe Mwita akiwataka viongozi wa Serikali na sekta binafsi mkoani Mara kuunganisha nguvu kutangaza fursa za uwekezaji zilizoko mkoani humo ikiwemo eneo la utalii, usafirishaji, biashara na huduma za kijamii.

Advertisement