Taasisi ya AWF yaanzisha tuzo za Benjamin Mkapa

Mke wa Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, Anna Mkapa akipokea zawadi ya kinyago cha tembo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wanyamapori Africa (AWF), Kaddu Sebunya baada ya kuzinduliwa kwa tuzo ya picha za wananyama ya Benjamin Mkapa huko Nairobi, Kenya. Picha na AWF.

Muktasari:

Taasisi ya Wanyamapori Afrika (AWF) na kampuni ya Nature’s Best Photography (NBP) zimetangaza rasmi kuanza kutoa tuzo mpya ya picha za wanyamapori ya Benjamin Mkapa.

Dar es Salaam. Taasisi ya Wanyamapori Afrika (AWF) na kampuni ya Nature’s Best Photography (NBP) zimetangaza rasmi kuanza kutoa tuzo mpya ya picha za wanyamapori ya Benjamin Mkapa.

Tuzo hiyo imepewa jina la Rais mstaafu Benjamin Mkapa aliyefariki dunia  Julai 24, 2020 ili kutambua uongozi wake katika  kuhifadhi wanyamapori, kutoa elimu na msaada wake wa dhati kwa taasisi ya AWF.

Katika kusherehekea siku ya wanyamapori duniani, AWF na NBP zimezindua tuzo hizo kama utangulizi wa maadhimisho ya miaka 60 ya AWF tangu kuanzishwa kwake mwaka 1961.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika kwenye makao makuu ya AWF jijini Nairobi, Kenya, mkurugenzi mtendaji wa AWF, Kaddu Sebunya amesema wanathamini teknolojia ya kidigali katika ulimwengu huu.

“Tunathamini ubunifu na mifumo ya kiteknolojia. Taratibu zinazoweza kuongeza kazi na athari za AWF, kama teknolojia za dijitali ambazo zinaweza kuunda uzoefu mpya kwa kuwaunganisha watu moja kwa moja na nyikani na wanyamapori.”

“Kuvunja viwango vya utengano kati ya watu na mazingira na kutengeneza umiliki, uwazi, kuonyesha athari na ubinafsishaji. Hii ndiyo tuzo ya Benjamin Mkapa ya picha za wanyamapori Afrika,” amesema Sebunya.

Sambamba na dhamira ya AWF ya kuhakikisha wanyamapori na hifadhi zinastawi katika Afrika ya sasa,  amesema lengo la mashindano ni kuwashirikisha, kuwahusisha na kuwavutia wapiga picha katika ngazi zote wakati wakihamasisha vipaji vichanga kuwa watetezi wa mabadiliko ya tabia ya jamii katika uhifadhi wa wanyamapori.

Kwa upande wake Rais wa NBP, Stephen Freligh amesema, “katika miaka yangu zaidi ya 30 katika kuchapisha picha, nimeshuhudia athari chanya za kuchanganya picha kwa ubunifu, utaalamu na wapigapicha wachanga.”

Wataalamu wa picha wanaochipukia na vijana wote wanaopiga picha kuanzia umri wa miaka 18, wanaalikwa kushiriki kwenye shindano hilo litakalofunguliwa rasmi Aprili 5 hadi Juni 2021.

Matokeo yamepangwa kutangazwa katika hafla ya utoaji wa tuzo hiyo Novemba, 2021. Washiriki watapata fursa ya kujishindia fedha taslimu, zawadi mbalimbali na tuzo, vyote vikiwa na thamani ya  Dola 33,000 za Marekani (Sh72.6 milioni).

Mshindi wa jumla wa tuzo hiyo atapata Dola 5,000 (Sh11 milioni), atafanyiwa mahojiano katika jarida la Nature’s Best Photography, kuchapishwa katika toleo maalumu la Tuzo ya Picha ya Mkapa. Washindi wa vipengele (category) kila mmoja atapata Dola 1000 (Sh2.2 milioni).