Takukuru Mwanza yaokoa Sh477.1 milioni ushuru wa madini ujenzi

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, James Ruge akitoa taarifa ya taasisi hiyo kwa kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu.

Muktasari:

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Ruswa mkoani Mwanza (Takukuru) imeokoa zaidi ya Sh477.1 milioni katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu kwa kudhibiti mianya ya rushwana upotevu mapato kwenye ukusanyaji wa ushuru wa madini ujenzi.

Mwanza. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Ruswa mkoani Mwanza (Takukuru) imetangaza kuokoa zaidi ya Sh477.1 milioni katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu kwa kudhibiti mianya ya rushwa na upotevu mapato kwenye ukusanyaji wa ushuru wa madini ujenzi.

Akizungumza leo Alhamisi Desemba 8, 2022 Muu wa Takukuru mkoani humo, James Ruge amesema katika kipindi hicho Halmashauri ya Misungwi, Kwimba na Sengerema zimekusanya Sh477.1 milioni mapato ambayo awali hayakuwahi kukusanywa kutokana na ushuru wa madini hayo.

“Tumedhibiti kutokuwepo kwa maeneo maalum ya uchimbaji wa madini ya ujenzi na kusababisha uwepo wa machimbo holela usiofuata utaratibu na tumesaidia baadhi ya halmashauri kutenga maeneo kwa ajili ya uchimbaji.

“Pia tulibaini wafanyabiashara wengi wa madini ujenzi kutokuwa na lesseni wala vibali vya uchimbaji, tumedhibiti na sasa vibali na leseni kwa ajili ya uchimbaji madini ujenzi sasa vinatolewa kwa mujibu wa utaratibu,” amesema.

Amesema waligundua shida ya kutokuwepo kwa kumbukumbu sahihi ya idadi za vifusi vya mchanga, mawe na kokoto zinazotolewa kwenye maeneo ya machimbo kwa siku ambapo walihakikisha taratibu za kuwepo kumbukumbu hizo zinawekwa.

“Tuligundua wakandarasi kutolipa ushuru wa madini ujenzi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo tukafanya ufuatiliaji na baadhi ya wakandarasi wameshaanza kulipa kwa mujibu wa utaratibu,” amesema.

Ruge amesema katika kipindi hicho taasisi hiyo kupitia dawati la uzuiaji rushwa imefuatilia utekelezaji wa miradi 27 ya Afya, Elimu, Maji na ujenzi yenye thamani ya Sh16.2 bilioni ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

“Kwa upande wa kazi za uchunguzi katika kipindi hicho, tumepokea taarifa 126 kati ya taarifa hizo, taarifa 106 zinahusu vitendo vya rushwa na taarifa 20 hazihusu vitendo vya rushwa,” amesema.