Tamu, chungu miaka 20 ya Kikeke BBC

Dar es Salaam. Ijumaa Aprili 28, 2023 usiku, mtangazaji kinara wa Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Salim Kikeke aliwaaga wafanyakazi wenzake na watazamaji wa kipindi maarufu cha Dira ya Dunia.

Kwa tangazo hilo, Kikeke amehitimisha safari ya miaka 20 ndani ya shirika hilo kongwe duniani.

Bila kuweka wazi sehemu anayokwenda, Kikeke amesema anakwenda kufanya majukumu mengine na kwamba katika kipindi chote alichokuwa hapo London baada ya kujiunga na BBC Swahili amekuwa na wakati mzuri tangu akiwa katika redio na kisha kwenye televisheni.

“Mimi ni Salim Kikeke na leo (Aprili 28, 2023) ni siku yangu ya mwisho kama mtangazaji kinara wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC.

“Nimekuwa BBC kwa miaka 20, miaka 10 nikiwa kama mtangazaji wa redio na mhariri wa tovuti yetu ya BBC Swahili na miaka 10 kama kinara wa Dira ya Dunia TV, mara moja moja nilikuwa nadonoa matangazo ya Kiingereza katika matangazo yetu ya BBC Focus on Afrika,” alisema.

Akieleza sababu ya kuondoka, Kikeke alisema hata mtu awe na uwezo kiasi gani, hawezi kukaa mahali pamoja kwa muda mrefu.

“Binadamu tumeumbwa na miguu ili tutembee, nimesimama hapa kwa takribani miongo miwili, nadhani ni wakati muafaka wa mimi kupiga hatua za matembezi na isingekuwa vyema kuondoka kimyakimya,” aliongeza.

Kufuatia tangazo hilo, Mwananchi imefanya mahojiano na Kikeke kwa njia ya mtandao akiwa nchini Uingereza, ambapo ameeleza sehemu ya maisha yake katika miaka 20 akifanya kazi na BCC.

Alipoulizwa sababu za kuondoka BBC, Kikeke anasema alishapanga kuondoka katika shirika hilo miaka sita iliyopita ili afanye mambo mengine.

“Wazo la kurudi Tanzania lilikuwepo tangu mwaka 2017, ambapo nilitaka kuacha kazi BBC, lakini wakaniomba niendelee, hivyo naweza kusema mafanikio yanahitaji kujituma na ubunifu hasa tunapotizama dunia ya kisasa,” anasema.

Katika kipindi hicho, pamoja na kazi mbalimbali alizozifanya, Kikeke anasema alishafanya mahojiano na watu mbalimbali maarufu, wakiwemo marais 11.

Kati ya marais hao wamo Jakaya Kikwete, Ali Hassan Mwinyi, Samia Suluhu Hassan, hayati Benjamin Mkapa na Amani Abeid Karume (Zanzibar) wote wa Tanzania.

Wengine ni aliyekuwa Rais wa Burundi hayati Pierre Nkuruzinza, Yoweri Museveni (Uganda), Joseph Kabila (DR Congo), Paul Kagame (Rwanda), Filipe Nyusi (Msumbiji) na William Ruto (Kenya) aliyezungumza naye muda mfupi kabla ya kutangazwa kuwa rais.

Mahojiano magumu

Miongoni mwa marais hao, Kikeke anakumbuka jinsi alivyopambana kumhoji Rais Nkuruzinza mwaka 2015 alipokuwa katika mvutano wa kutaka kugombea urais kwa awamu ya tatu.

Anasimulia jinsi wahariri wake walivyotumia saa nne kujadili kuhusu mahojiano na Rais Nkurunzinza wakati kiongozi huyo alikuwa akikataa baadhi ya maswali.

“Tulizungumza na watu wake wakati niko London, tukakubaliana tutakwenda kufanya mahojiano na wakati huo ndiyo alikuwa anataka kuwania muhula mwingine.

“Kwa hiyo tukakubaliana tukaenda na timu yangu. Ilikuwa tufanyie Bujumbura, lakini baadaye watu wake wakasema Rais anataka tukamfanyie mahojiano nyumbani kwake Ngozi, Kaskazini mwa nchi hiyo.

Hata hivyo, anasema wakati akielekea Ngozi, wasaidizi wa Rais walimpigia simu na kumweleza kuwa mahojiano yapo ila Rais hatajibu swali la iwapo atawania muhula mwingine.

“Sasa safari yangu yote kutoka Uingereza hilo ndilo lilikuwa swali la kumuuliza, dunia nzima ilikuwa inataka ijue, kwa hiyo kwa wakati ule nikaambiwa, tukubaliane kabisa hilo swali kama halipo mahojiano yatakuwepo na kama hilo swali lipo basi mahojiano hayatakuwepo,” anasema.

Baada ya kupewa sharti hilo, Kikeke anasema ilibidi apige simu ofisini kwake London, Uingereza kumpa taarifa mhariri wake iwapo waendelee na mahojiano au waache.

“Baadaye mhariri wangu alikuwa anaitwa Stephano Mayoux aliniambia kwa kuwa tumeshafika Bujumbura itabidi ukazungumze naye ingawa sisi (BBC) huwa hatupewi masharti, pengine tungeweza kuondoka, lakini tulifanya mahojiano.

“Tulipotoa habari hiyo tuliweka wazi kwamba swali hilo ambalo ni nyeti na kila mtu anataka kusikia jibu lake, lilikataliwa na Rais. Badala yake tulikwenda kuzungumza na mwenyekiti wa chama CNDDF ambaye alisema suala la kuwania nafasi hiyo au kutokuwania ni suala la chama, hivyo hatukupata jibu la moja kwa moja, ingawa baadaye Nkuruzinza alikuja kuwania urais muhula wa tatu na akashinda,” anasema Kikeke.

Alipoulizwa kuhusu kitu ambacho hakisahau katika miaka hiyo ya utumishi BBC, Kikeke alisema ni pamoja na watu aliokutana nao na timu aliyofanyanayo kazi kwa kipindi chote alichokuwa BBC.

“Siwezi kuisahau kwa sababu tuliishi kama familia kwa kusaidiania katika shida na raha.

“Unajua kwenye hizi kazi zetu kuandaa taarifa na kwenda hewani si jambo rahisi, ukiangalia Kombe la Dunia la kwanza kufanyika katika bara la Afrika mwaka 2010 nilikuwepo Afrika Kusini.

“Pia kwenye msiba wa Nelson Mandela, ambayo ilikuwa ni taarifa ya kimataifa nashukuru Mungu nilikuwepo hapo Afrika Kusini, hivyo unaweza kuona kabisa kwenye matukio mengi na makubwa ya kimataifa nilikuwepo na siwezi kuyasahau,” anasema.

Kikeke anasisitiza kuwa uhusiano mzuri na ushirikiano uliokuwepo baina yake na wafanyakazi wenzake ni jambo kubwa ambalo atalienzi.

“Kitu kingine kikubwa ambacho sitakisahau ni kupata mafunzo kila mwaka, unakuwa unanolewa namna ya kufanya kazi na kuendelea na jinsi mabadiliko ya habari yanavyotokea, kwa hiyo mnakuwa tayari, hivyo mafunzo hayo kwangu ni kitu kikubwa kabisa, ukiacha hivyo vitu vingine,” anasema.

Pamoja watumishi wenzake wengine, Kikeke hawezi kumsahau Tido Mhando.

“Siwezi kumsahau Tido Mhando, wakati najiunga BBC alinipokea pale akiwa mkurugenzi wa Idhaa ya Kiswahili na nilipoenda ofisini kwake nilimwambia siwezi kurudi tena Tanzania na yeye alicheka sana, kwani nilikuwa nimedhamiria kufanya kazi kwa muda mrefu BBC na baadaye nilipewa mkataba wa muda mrefu kutoka mkataba nilioanza nao wa miezi mitano,” anasema.

Anakwenda wapi?

Alipoulizwa kama kuna mahali amepanga kwenda kufanya kazi baada ya kutoka BBC, Kikeke alisema:

“Nimeondoka tu BBC, lakini kwenye field ya uandishi wa habari nitaendelea kuwepo. Unajua uandishi wa habari ni kama mwanajeshi, huwezi kuacha, utakuwa mwandishi maisha yote.

“Kwa hiyo si kwamba naondoka BBC na nimeacha uandishi wa habari, bila shaka nitakuwa nafanya uandishi kwa njia moja au nyingine, lakini fani hii naipenda na hata kama nitakuwa sifanyi kazi moja kwa moja kwa kuripoti matukio, lakini nitakuwa hata nasaidia kutoa mafunzo kwa vijana ambao wanaingia katika faini ya uandishi wa habari,” anasema.

Anabainisha kuwa ni vigumu kusikia mwandishi wa habari amestaafu, hivyo ataendelea kuwa mwandishi wa habari na mtangazaji wa habari kwa sababu ni kitu ambacho anaweza kukifanya akiwa popote duniani na katika hali yoyote ile.

“Kitu nilichokifanya ni kuondoka katika Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC) kwa hiari yangu mwenyewe na nilikuwa nataka kuondoka muda kidogo, lakini sasa shirika likaniomba nibaki kidogo, lakini kwa sasa nitapumzika kidogo, nataka niende mahali kidogo nitulie kwa sababu hii miaka 20 ilikuwa ya mchakamchaka.

“Nakumbuka mwaka 2013 nilichukua likizo nikaenda kumsalimia mzee wangu kule Mbeya, nikiwa katikati ya likizo nikapigiwa simu na ofisi kuwa kuna shambulio la bomu limetoke West Gate kule Nairobi, Kenya, hivyo nikakatisha likizo.

“Kwa hiyo unaweza kuona hata kipindi cha likizo mtu huwezi kupumzika vizuri ila kwa sasa naweza kwenda sehemu nikatulia na kuzima simu yangu na kupumzika,” anasema.

Mbali na mchakamchaka anaouelezea, Kikeke anasema anapendelea kusikiliza muziki hususani mziki wa kizazi kipya, yaani Bongo Fleva.

“Pia napenda kilimo, napenda kulima na siku moja natarajia kuwa mkulima kwa sababu nina stashahada ya umwagiliaji. Vilevile napenda kusafiri na kukutana na watu tofauti tofauti kwa ajili ya kubadilishana mawazo.”

Wanavyomzungumzia

Miongoni mwa wanahabari waliofanya kazi na Kikeke BBC ni Charles Hilary, ambaye kwa sasa ni Msemaji Mkuu wa Serikali ya Zanzibar anayesema, “Salim ni mtu wangu wa karibu sana. Mimi na Salim kabla ya kukutana London, tulifanya kazi pamoja ITV.

“Salim alikuwa akisoma habari kwa Kiingireza na kwa kiasi kikubwa mimi nilichangia yeye kuingia ITV.”

Hilary, ambaye aliondoka BBC mwaka 2017 akiwa mtangazaji wa kwanza wa michezo katika Dira ya Dunia, anasema Kikeke alimtangulia kwenda BBC na yeye (Hilary) alipokwenda mwaka 2006 alimkuta na kuendeleza mahusiano yao ya kikazi.

“Unajua Salim ni mbunifu, kichwa chake kinafanya kazi haraka sana. Unaweza kwenda sehemu kufanya kazi, anakwambia tufanye hivi na matokeo yake yanakuwa mazuri. Kwa kuondoka BBC watakuwa wamepoteza mtu muhimu sana,” alisema.

Akikumbusha kisa cha mwaka 2010 katika Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini, Hilary alisema walikwenda kutangaza matangazo hayo.

“Katikati ya mashindano Salim akampoteza mama yake huku Tanzania. Akaondoka na kuniacha peke yangu. Nikaletewa mtu kutoka Nairobi na mmoja kutoka London.

“Niliona tofauti ya kuondoka kwa Salim, ile kuondoka ilininyong’onyesha kidogo...ni kipindi ambacho siwezi kukisahau baina yetu,” alisema Hillary.

Mwingine aliyefanya kazi naye ni Zuhura Yunus, ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, aliyesema “tulikuwa tukielewana sana. Nilimkuta BBC na kufanya kazi vizuri sana.”

Zuhura, aliyeondoka BBC mwaka jana alisema: “Salim ni mchapa kazi sana na ni mbunifu sana na vilevile unajua ana vituko vya kutosha na vinaongeza raha kwenye kazi, na kingine anajituma kweli kweli”.

Alisema kutokana na ubunifu na juhudi zake kwenye kazi, kulimfanya kuwa mtangazaji kinara. “Unajua anapenda michezo na anaweza mambo mengi kwa mpigo. Anatangaza soka kwa Kiingereza na Kiswahili kwa ufasaha. Kwa kweli ni raha kufanya naye kazi.”

Zuhura alisema kutokana na kuelewana kwenye kazi, Salim alikuwa miongoni mwa watu aliowaeleza mapema kuondoka kwake BBC, “mimi (Zuhura) nasepa, hapa inatosha nataka kurudi nyumbani,” anasema akikumbuka walivyoagana.

Pia yupo Hassan Mhelela anayesema alimpokea Kikeke mwaka 2003 wakati BBC Swahili ikiwa jengo la Bush House, London wakifanya kazi chini ya Tido Mhando.

“Mimi na Salim tulifanya mengi, ikiwa pamoja na kuimarisha mtandao wa BBC Swahili, wakati huo ilikuwa ni kujitolea kwa sababu wasikilizaji walitaka habari zaidi mitandaoni.

“Ni mbunifu na ni miongoni mwa watangazaji wenye wafuasi wengi mitandaoni, ikiwemo Instagram,” alisema Mhelela, aliyehamishwa kutoka London kuwa mkuu wa BBC Swahili Tanzania mwaka 2011 hadi mwaka 2015 alipohamia Azam Media hadi sasa.