Tanapa, Tasac zang’ara tuzo za mahesabu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Zanzibar Jamal Kassim Ali, akitoa tuzo za Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), kwa Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) Pascal Maromba.

Muktasari:

  • Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), imetoa tuzo kwa mashirika mawili kwa kile lilichosemwa ni uandaaji mzuri na bora wa mahesabu.

Dar es Salaam. Shirika la Uwakala wa Meli nchini (Tasac) na Shirika la Uhifadhi Tanzania (Tanapa) yametangazwa kuwa mashirika bora ya umma yameandaa hesabu katika vingo bora kimataifa kwa mwaka 2022.

Tuzo hizo zimetolewa Desemba 2, 2023 jijini Dar es Salaam na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), ambapo Tasac ikishika nafasi ya kwanza ya uwasilishwaji bora wa hesabu mwaka 2022.

Akipokea tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Fedha Tasac Pascal Karomba amesema ushindi huo umewapa chachu ya kuendelea kuboresha utendaji wake katika maeneo wanayosimamia.

“Ushindi huu unawapa wananchi ujumbe kuwa tunanachosimamia kipo salama na fedha zao hakuna zilizopotea, tutaongeza nguvu zaidi kuhakikisha tunakuwa kioo bora kwa wananchi, mtu sasa akiagiza mbolea au mchele kutoka nje kupitia bandari zetu awe na uhakika itafika salama,” amesema.

Si mara ya kwanza kwa shirika hilo kuibuka kidedea ambapo kwa mujibu wa Kairambo mafanikio hayo yameendelea kuchochea kuimarika kwa utendaji ndani ya taasisi hiyo.

Amesema Tasac imewezesha kuongezeka kwa idadi ya watoa huduma wanaodhibitiwa na ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/22 idadi ya leseni na vyeti vya usajili imefikia 1,195 ikilinganishwa na leseni na vyeti vya usajili 941 katika mwaka wa fedha 2018/19 sawa na ongezeko la asilimia 79.

Pia amesema Tasac inajivunia kuimarisha usimamizi wa usalama, ulinzi na utunzaji wa mazingira dhidi ya shughuli za meli kwa lengo la kupunguza matukio ya ajali za vyombo vya majini,

Kwa upande wa Tanapa, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi, Juma Kuji amesema ushindi huo unaonyesha utoaji wa taarifa za fedha na utunzaji kumbukumbu unatekelezwa vyema.

“Watanzania waendelee kuwa na imani na Tanapa kwa kutembelea hifadhi zilizopo nchini, tutumie mapumziko ya Desemba kutembelea vivutio vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini,” amesema.

Katika hatua nyingine Kuji amemshukuru Rais Samia kutokana na juhudi zake za kuendelea kukuza utalii nchini.

Amesema takwimu za Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), zinaonyesha watalii wanaoingia nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (KIA), kutembelea hifadhi za taifa, wameongezeka kutoka watalii 780,000 hadi kufikia watalii 927,000 kwa takwimu za Agosti mwaka huu.