Tanesco kuwaunganishia umeme waliolipia Sh27,000 Shinyanga

Meneja waTanesco mkoa wa Shinyanga, Grace Ntungi

Muktasari:

  • Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Grace Ntungi amesema wananatarajia kuanza kuwaunganishia umeme wananchi 3200 waliokuwa wamelipia Sh27, 000 kabla ya kutangazwa bei mpya hivi karibuni.

Shinyanga. Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Grace Ntungi amesema wananatarajia kuanza kuwaunganishia umeme wananchi 3200 waliokuwa wamelipia Sh27, 000 kabla ya kutangazwa bei mpya hivi karibuni.

Mhandisi Ntungi amesema hayo Jumatatu Januari 17, 2022 wakati akitoa ufafanuzi kuhusu gharama za kuunganisha huduma ya umeme kwa wananchi wa mkoa wa Shinyanga, ambapo amesema katika maeneo ya vijijini wataendelea kulipia Sh27, 000 kama kawaida na maeneo ya mjini na miji wataunganishiwa kwa gharama zilizotolewa hivi karibuni.

Amesema mpango huo wa kuwaungishia umeme wananchi hao ambao walikuwa wamelipia Sh27, 000 unatarajiwa kukamilika Machi 31, 2022.

"Zoezi hili la kuwaunganishia huduma ya umeme wananchi wa maeneo ya miji na vijiji waliokuwa wamepewa control namba ya kulipia Sh 27,000 mwezi Septemba 2021,  na mpaka kufikia Januari 16, 2022 walikuwa takribani 3200 lilikwama kwa baadhi ya maeneo kutokana na changamoto ya upatikanaji wa vifaa, hivyo kwa sasa vifaa vipo tutaendele kuwaunganishia wananchi waliolipia" amesema Ntungi.

Meneja Ntungi amesema Tanesco imeanza kutumia bei mpya za kuunganisha umeme Januari 5 mwaka huu huku ikisema Sh 27,000 itatumika kwenye maeneo ya vijijini

“Katika maeneo ya miji midogo itakayolipia gharama halisi za kuunganisha umeme ni Iselamagazi, Salawe na Tinde katika Wilaya ya Shinyanga, Nyamilangano, Lunguya na Chela wilayani Kahama na Kishapu (Mhunze) wilayani Kishapu”, amesema Mhandisi Ntungi.

Amesema maeneo yatakayolipia gharama halisi za kuunganisha umeme kwa umeme wa njia moja yaliyo ndani ya miji na Manispaa gharama ni Sh 272,000 kwa eneo ndani ya mita 30 (bila VAT na VAT ikiongezwa jumla ni Sh 320,960, eneo ndani ya mita 70 Sh 436,964 bila VAT na eneo ndani ya mita 120 ni Sh 590,398  bila VAT.