Tanesco yasema uzalishaji umeme bado hautoshi

Muktasari:

  • Shirika la Umeme (Tanesco), limesema ni vigumu kutoa hakikisho la kutokuwepo kwa mgawo wa nishati hiyo kwa siku zijazo.

Dar es Salaam. Shirika la Umeme (Tanesco), limesema licha ya kuimarika kwa upatikanaji wa umeme kwa sasa, ni vigumu kueleza juu ya kukoma kwa mgawo.

Limesema kukoma kwa mgawo wa nishati hiyo kutatokana na kuimarika kwa uzalishaji utakaowezesha hata mtambo mmoja ukizimwa mwingine uwe na uwezo wa kuhudumia.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam leo, Januari 31 na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Maharage Chande wakati akitoa taarifa ya hali ya umeme nchini.

Kwa mujibu wa Chande, katika kipindi cha Desemba na Januari hakukuwa na mgawo wa umeme, lakini ni vigumu kulitabiri hilo katika mwezi Februari.

"Kutokuwepo kwa mgawo kunatokana na moja kuimarika kwa uzalishaji wa umeme na uhakika kwamba mitambo yetu haitasumbua.

"Kwa sababu kwa sasa hatuna uwezo wa kuzalisha kiasi kinachowezesha mtambo mmoja ukizimwa mwingine uendelee kuzalisha kwa kutosheleza," amesema Chande.

Lakini, ameeleza katika kipindi hicho shirika hilo limechukua hatua mbalimbali kuimarisha uzalishaji wa umeme, huku matengenezo ya mitambo yakiendelea.

Kuhusu kuimarika kwa uzalishaji, amesema mtambo mmoja wa Kituo cha Kinyerezi II umeanza kuzalisha megawati 45 kwenye gridi ya Taifa.

Matengenezo ya mitambo miwili iliyopo katika Kituo cha Ubungo imekamilika na ameeleza imeanza kuzalisha megawati 30 na 40 za umeme.

Kulingana na Chande, mtambo wa Kituo cha kidatu umetengenezwa na umeanza kuzalisha megawati 50 za umeme kwenye gridi ya Taifa.

Amesema mitambo mitatu katika Kituo cha upanuzi Kinyerezi I imeshafungwa na inaingiza megawati 120 kwenye gridi ya Taifa.