Tanga yaanda sheria kuwabana watupa uchafu

Thursday December 23 2021
usafipic
By Raisa Said

Tanga. Jiji la Tanga linaandaa sheria itakayomlazimisha mtu anayetupa takataka katika mitaa ya jiji hilo kulipa faini ya Sh50,000 ili kulinda ubora na usafi wa mazingira.

Akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake baada ya kupata ushindi wa kwanza wa usafi wa mazingira leo Alhamisi Desemba 23,2021 Meya wa Jiji hilo Abdulhaman Shilow, amesema katika kukabiliana na watupa taka hovyo katika mitaa, wataajiri vijana 50 ambao watakuwa mitaani kusimamia watu wanaotupa taka.

Hata hivyo, jiji hilo limepata ushindi wa kwanza wa usafi wa mazingira ambapo wamepokea cheti, kombe pamoja na Sh20 milioni.

"Januari 2022 tutaanza kusimamia sheria ya kuwakamata watu wanaotupa takataka ovyo na kuwapiga faini ya Sh50,000 papo hapo...Na tutatoa ajira kwa vijana 50 ambao watahusika katika ukamataji huo," amesema  Meya

Hata hivyo, Meya amesema ushindi wa kwanza kwa Jiji hilo imetokana na kushirikiana na viongozi, wananchi na wadau mbalimbali ambao wamefanikisha suala la usafi wa mazingira katika mitaa mbalimbali.

Alisisitiza kwakuwataka wananchi washirikiane na viongozi katika kuhakikisha wanatunza maeneo yao na kiasi cha Sh2,000 wanacholipia kwa mwezi kwa kila kaya, waendelee kulipa ili kazi ya kusafisha mitaa iwe rahisi.

Jiji la Tanga limekuwa la kwanza kwa usafi wa mazingira likifuatiwa na Arusha huku Jiji la Mwanza likishika nafasi ya tatu.

Advertisement
Advertisement