Tanzania kuchenjua kilo 970 za dhahabu kwa siku

Muktasari:

  • Kiwanda cha kuchenjua dhahabu cha Mwanza Precious Metal Refinery (MPMR), kilichojengwa kwa zaidi ya Sh12.2 bilioni kinamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (Stamico) na sekta binafsi.

Mwanza. Tanzania itakuwa na uwezo wa kuchenjua kiko 960 za dhahabu kwa siku ujenzi wa viwanda vitatu vya kuchenjua madini utakapokamilika.

 Akizungumza jijini Mwanza leo Juni 13, wakati wa hafla ya kuzindua kiwanda cha kuchenjua madini cha Mwanza Precious Metal Refinery (MPMR), Waziri wa Madini, Dotto Biteko pamoja na kiwanda hicho kilichopo eneo la Sabasaba jijini Mwanza chenye uwezo wa kuchenjua kilo 480 kwa siku, kiwanda kingine chenye uwezo wa kuchenjua kilo 450 kiko mkoani Geita.

Waziri Biteko aliyejivunia kukua kwa sekta ya madini nchini amesema kiwanda kingine chenye uwezo wa kuchenjua kilo 30 kinajengwa mkoani Dodoma.

Amesema ujenzi wa viwanda hivyo, utekelezaji wa sheria na sera ya madini pamoja na usimamizi makini wa Serikali katika shughuli za madini umeongeza mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa kutoka asilimia 5.2 hadi kufikia asilimia 6.7 mwaka 2021.

Waziri huyo amesema Wizara yake imekusanya zaidi ya Sh5444 bilioni sawa na asilimia 103 ya malengo ya kukusanya Sh526 bilioni kwa mwaka wa fedha wa 2020/21.

“Ni malengo yetu kuwa tutakuwanya zaidi ya Sh650 bilioni kwa mwaka wa fedha ujao 2021/22,” amesema Waziri Biteko.

Kutokana na mafanikio yanayopatikana tangu marekebosho ya sheria na sera ya madini, Waziri Biteko amesema lengo la kuongeza mchango wa sekta kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025 itafikiwa.