Tanzania kupima ubora wa maji kwa taarifa za anga

Mkurugenzi msaidizi huduma za ramani katika idara ya upimaji na Ramani kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Elizabeth Mrema

Muktasari:

Huenda siku chache zijazo Tanzania ikaanza kupima ubora wa maji katika mito na maziwa kwa kutumia taarifa za anga (njia ya picha za satellite).

Dar es Salaam. Huenda siku chache zijazo Tanzania ikaanza kupima ubora wa maji katika mito na maziwa kwa kutumia taarifa za anga (njia ya picha za satellite).

Jambo hilo litaiwezesha Serikali kujua ni kitu gani kinapaswa kufanyika kabla ya matumizi ya maji husika na kujua hali ya usalama wa maji.

Hilo linafanyika kwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na kituo cha Kituo cha Kanda cha Ramani cha Rasilimali na Maendeleo (RCMRD).

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi msaidizi huduma za ramani katika idara ya upimaji na Ramani kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Elizabeth Mrema ambaye alisema mradi huo unatoa taarifa zitakazosaidia kufanya maamuzi huku akieleza kuwa ni ngumu kufanya maamuzi kama hauna taatifa ya utafiti.

“Ukiwa hauna taarifa hizi hautajua kama maji ya mto huu nikiyatumia yatakauka baada ya muda gani lakini kama utapata utafiti unaweza kujua kuwa mto huu utumike vipi, maji yamefanyiwa uchafuzi kwa kiasi gani, yatibiwe vipi ili yafae kwa ajili ya matumizi,” amesema Elizabeth.

Amesema utafiti wa awali ulifanyika katika ziwa Victoria na majibu yake yametolewa huku akieleza kuwa kufanya hivyo kutasaidia kutoa majibu ya awali.

Calvince Wara ambaye ni Msimamizi wa Maji na Majanga kutoka RCMRD amesema mfumo huo utasaidia kufanya utafiti ili kuangalia mapengo yaliyopo ikijumuisha takwimu katika kusaidia usimamizi wa rasilimali maji, ubora wa maji, namna vyanzo vya maji vinavyoathiriwa.

Pia kupitia mfumo huo utasaidia kujua kina cha maji katika chanzo husika wakati wa mvua na baada ya msimu wa mvua jambo ambalo litasaidia katika kufanya maamuzi.